Healthy
Stories
Life-Style

More News

*My Past.* Sehemu ya 18.

*My Past.*
Sehemu ya 18.

 “Mmekula lakini?” “Tulikula kabla yakutoka nyumbani.” “Basi twendeni huko nyuma
ya hii nyumba, ili siku ianze.” Bella alidhania wanatoka nje kabisa. Kumbe ni ndani ya ile ile nyumba kwa mwisho kabisa, katikati paliachwa nafasi kubwa iliyokuwa na sehemu nzuri yakuogelea na michezo ya kisasa ya Toby, pembeni ya bwawa hilo. Bella alibaki ametoa macho. Alijua pale kwao ndio kuna michezo ya watoto ya kisasa na amemtoa ushamba Toby na baba yake, kumbe hata robo ya michezo anayomiliki Toby, mwanae hajafikia. Lewis alianza kucheka. “Wewe unaonekana ni mtundu sana Enabella.” “Kwa nini?” “Sasa ushangaaji gani huo?” Bella alianza kucheka. “Tunaruhusiwa kupiga picha?” “Ric anaruhusiwa kuogelea?” Lewis naye akauliza swali. “Hapana.” Bella alijibu kana kwamba anaokoa kitu kilichotaka kuanguka akaenda kumbeba mtoto wake kwa haraka sana. “Hapana!” Akabaki amemkumbatia mwanae kwa nguvu sana, huku amemtolea macho ya mshtuko Lewis.

“Upo sawa? Mbona unanitisha?” Ikabidi Bella ajirudi taratibu. “Samahani. Daah!” Bella alijishika moyoni. “Nitakuwa nao ndani ya maji na watavaa ‘life jackets’ hawawezi kuzama.” Uso wa Bella ulishabadilika, ulijaa wasiwasi sana. Lewis aliona. “Au wanaweza kucheza mchezo mwengine.” Ilibidi Lewis abadilishe mchezo maana Bella alibadilika uso, akabaki amemng’ang’ania mwane tena amemkumbatia kwa nguvu sana, huku ameficha uso wa mtoto wake. Lewis alibaki akimshangaa.

“Basi, ngoja nikalete matunda.” “Hapana, usituache hapa peke yetu.” Lewis alisimama akimwangalia. “Hapa ni ndani ya nyumba Enabella, hakuna atakayewafikia nyinyi kabla yangu mimi huko ndani.” “Maji! Hayo maji hapo.” Lewis aligeukia ile pool. “Namanaisha mtoto akitumbukia humo ndani, nani atamuokoa?” “Sitachelewa. Nilisha yatayarisha hayo matunda. Yapo tayari. Naenda kuyatoa tu kwenye friji.” “Mimi naona twende wote tu.” Lewis alifikiria kidogo. Akaenda kubeba watoto wote akaingia nao ndani huku akinguruma kama simba, nao walikuwa wakicheka sana. Waliingia jikoni Bella akiwafuata nyuma.

“Unaweza kufungua hiyo friji na kuchukua bakuli ya matunda? Lipo juu kabisa.” Bella alisogelea ile friji, ilikuwa kubwa sana. Alivuta mlango. “Vuta mlango wa upande wa kulia, kushoto ni friza.” Bella alifunga na kufungua mlango mwingine. Akatoa hilo bakuli la matunda. “Tunaweza kwenda kula kule kule kwenye pool.” “Hapana.” Lewis alitoa macho. “Basi twendeni ndani kuna chumba ambacho Toby huwa anacheza nikiwa naandaa kazi zangu.” Lewis aliongoza njia mpaka kwenye chumba kingine, kilikuwa kikubwa sana. Nusu kilionekana kama ofisi, nusu kilijaa matoi ya Toby na Tv kubwa sana ya ukutani. Bella alibaki amesimama katika ya kile chumba na bakuli lake la matunda.

Lewis aliwaweka watoto chini wakakimbilia michezo, akarudi kumpokea Bella lile bakuli. “Karibu sana. Naamini hapa patatufaa.” “Samahani sana Lewis. Najua ulishapanga mipango yako juu yetu, na nina elewa sio vizuri sisi kama wageni kuja nakuanza kukupangia kitu cha kufanya ndani ya nyumba yako.” “Kwa nini unaogopa maji?” Bella alikunja uso na kubaki akibabaika kama aliyekuwa akitafuta kitu cha kusema. “Au hujui kuogelea?” “Nafahamu sana kuogelea.” Lewis alibaki akimtizama.
Njoo basi tukae hapa wakati tukiangalia watoto wakicheza. Nitakufundisha game ya kucheza kwenye tv, huwa tunashindana na Toby.” “Hapana.” Lewis alishaanza kutangulia upande wenye hiyo game, ilimbidi amgeukie Bella kwa mshangao. “Na game nayo pia hapana?” Bella alitingisha kichwa kukataa. Lewis alirudi alipokuwa amesimama Bella. “Labda nimekuwa na haraka sana. Ungependa kufanya nini Enabella?” “Kuongea na mkeo.” Bella alijibu. “Kama nilikwambia kuwa nimeoa, basi leo siri imefichuka.” “Kwani vipi?” “Sijaoa.” “Sasa unaishi hapa na nani?” “Na Toby.” Lewis alibaki akimuangalia Bella machoni. “Mbona umeshtuka? Hebu ngoja niseme unachofikiria Enabella. Unafikiria hivi, ‘Kama ningejua mapema kama huyu jamaa na nyumba yake iliyojaa vitu nisivyovipenda, hana mke pia, nisingekuja.’ Niambie ukweli. Nimepatia kwa asilimia ngapi?” Bella alicheka. “Sema ukweli Enabella.” “Alisilimia 98.” “Haya. Umeshafika, na watoto wanacheza sasa hivi, huwezi kuondoka kwa haraka hivyo. Niambie kitu chochote unachotaka kufanya, tufanye ili tusogeze masaa wakati watoto na wao wanacheza.” “Unafanya kazi gani?” “Oooh! Kwa hiyo unataka tuongee tu?” Bella alicheka tena. “Haya njoo hapa kwenye kompyuta, nikujibu kwa vitendo. Naamini kompyuta sio adui. Ama?” Bella alimfuata nyuma mpaka upande wa ofisi yake.

“Umeshasikia kokote kule juu ya  ‘Computer programmer’?” “Ndiyo.” “Basi ndio kazi ninayoifanya, au ndio kazi inayotuweka mjini mimi na Toby.” Bella alitabasamu. “Na wewe unafanya kazi gani?” “IT.” “Safi sana.” “Lakini sikuisomea sana. Sehemu kubwa, nimekuwa nikijifundisha mimi mwenyewe.” “Hongera sana. Kwa namna nyingine umepunguza gharama ukaamua kuwa mwalimu wako wewe mwenyewe.” Bella alicheka. Lewis alifungua kompyuta moja lakini yenye screen mbili. Aliendelea kumuonyesha Bella vitu anavyofanya, na Bella aliendelea kuhoji. Katika hilo angalau walielewana kwa kuwa wote walifanya kazi angalau zinazofanana.

“Safi sana Bella. Tena unaweza kuajiriwa pale ofisini kwetu kama ungependa. Wanalipa vizuri sana.” Bella alicheka. “Kweli. Au unahofia cheti? Nimeona uelewa wako na mambo niliyokuonyesha, nafikiri utatufaa. Au hutaki kutengeneza pesa zaidi? Tutakuanzia juu ya mshahara unao lipwa sasa hivi.” “Unajua Lewis, katika maisha yangu niliyoishi hapa duniani, nimekuja kugundua maisha sio pesa peke yake.” Lewis aligeuza kiti na kubaki akimwangalia Bella kama anayemsuta. “Haya niambie mama. Maisha ni nini bila pesa?” Bella alicheka. “Sikatai kwamba pesa ni za muhimu sana katika maisha, lakini sio kitu pekee kinacholeta maana maishani.” “Nakusikiliza mrembo ambaye unanukia pesa tupu. Kila kitu chako kinaonekana cha gharama. Mwanao anasoma shule ya mamilionea hapa mjini, gari unayoendesha wewe mwenyewe, Mtanzania wa kawaida hawezi hata kugusa, yaani ukipita mjini unajulikana Bella amepita, jinsi mlivyo wachache wenye magari hayo. Umevaa dhahabu kuanzia masikioni, shingoni, mikononi, mpaka miguuni. Tena inaonekana sio dhahabu ya hali ya chini. Pafyumu yenyewe unayonukia ni mshahara wa mtu.” Bella alicheka kwa aibu. “Niambie Enabella. Umesema pesa sio…” “Bwana acha kukuza mambo Lewis. Najua umenielewa.” “Hapana. Unanilazimisha nielewe kitu kisicho cha kweli.” “Basi labda nibadilishe usemi, kuwa pesa pekee sio inayokamilisha furaha maishani.” “Ni yaleyale tu. Labda niulize swali, ni wapi huko unakofanya kazi na hutaki kuacha, tena kwa ahadi ya mshahara mkubwa?” Bella alitabasamu, akafikiria kidogo.

“Ni habari ndefu Lewis, lakini kwa kifupi nataka ujue nimeridhika na hapo nilipo.” “Hilo halina ubishi wala mjadala. Kweli unaonekana umeridhika. Lakini kwa kuwa hatuna kingine chakufanya leo zaidi ya kuongea, naomba tu usinifupishie habari. Niambie tu huko uliko kwenye neema hivyo, ni wapi? Labda na mimi nitakuja kuomba kazi.” “Ndio maana nakwambia sio pesa inayonifanya nipapende huko. Wala silipwi mshahara mkubwa sana.” “Ila ni nini Enabella?” Bella alitulia kidogo.

************************************************

“Kwa mama yetu tulizaliwa wawili tu, mimi na mdogo wangu Eric. Hatukuwa tukiishi na baba, na wala simfahamu baba yetu ni nani. Mama alipofariki aliniachia mdogo wangu. Tuliteseka sana tukihangaika hapa mjini, mpaka nilipoangukia kwa baba yake Ric. Hiyo ni habari nyingine tena. Ni ndefu sana, sitaweza kukusimulia leo, itaniharibia siku yangu nzima ya leo. Lakini nikaanza kuishi naye, ni baba ya aliyekuwa rafiki yangu kipenzi. Yeye ndio ana mali zote hizi. Nilipoondoka kwake, niliondoka nikiwa mjamzito wa Ric. Lakini wakati nikiishi naye alinitafutia kazi ya mambo ya IT kwenye kampuni ya wale watu ninao ishi nao sasa hivi, Mwasha. Wamenipokea sasa kama mtoto wao.” “Eric yuko wapi?” Bella aliinama kwa muda.

“Bella ampa Lewis nusu ya historia yake.”
“Siku moja tulikuwa mapumzikoni Bagamoyo, Mimi, Eric na mtoto mmojawapo wa Mzee Mwasha anaitwa Elvin, yeye hukumkuta siku ile, alishaoa akahama pale ndani. Wakati Elvin na Eric wamelala, mimi niliamka asubuhi kwenda kuogelea baharini, walikuja watu wawili wakanivuta kutoka kwenye maji, wakaniteka nyara. Sikumbuki kilichoendelea baada ya hapo kwani waliniziba pua na kitambaa, nahisi kilikuwa na dawa ya usingizi au sijui, lakini nilikuja kuzinduka baada ya miaka karibia minne, nimekaa mimi na Ric, kwenye chumba kilikuwa na giza sana, nikatoroka na Ric, tena hata sikuwa nikimjua hata kama Ric ni mwanangu. Ndipo niliporudi pale nyumbani kwa Mzee Mwasha, nikaambiwa nilikuwa nimepotea kwa muda wote huo na nilipotea nikiwa mjamzito. Yule mama alinigundua muda mrefu kuwa nilikuwa mjamzito, ndio wakawa wamemtuma Elvin aniambie wakati tulipofika Bagamoyo. Lakini siku Elvin aliyotaka kuniambia, ndio siku niliyotekwa nyara. Kwa hiyo nilipotea nikiwa sijijui hata kama ni mjamzito. Nilikuwa mtoto sana.” “Hata sasa bado unaonekana ni mdogo.” Bella alitabasamu.

“Nilimchukua Ric kule porini nilipokuwa naye, kwa kuwa alikuwa akifanana sana na Eric, na nilimuonea huruma kumuacha pale peke yake, maana tulikuwa peke yetu, kwenye kijumba kilichochoka sana. Cha matope na nyasi.” “Ni wapi?” “Hata sijui. Nilitoroka nikiwa na kumbukumbu za kutekwa nyara kule baharini, kwa hiyo nilikuwa nikikimbia nikijua ndio jana yake nilichukuliwa Bagamoyo kumbe ni muda mrefu sana ulishapita. Nilikuwa nikikimbia na mtoto mgongoni, mchana na usiku mpaka baada ya kama siku tatu ndipo nilipotokea barabarani, nikakuta abiria wa basi wanajisaidia vichakani na mimi nikajidai ni mmoja wao, nikarudi nao kwenye basi mpaka huku Dar. Sikutaka kuuliza kwa hofu ya kushushwa kwenye basi, na mimi sikuwa na nauli. Na kwa kuwa nilikuwa nimechoka, nilipoingia kwenye basi, tulibahatisha kiti, nilipokaa tu, nililala mpaka nilipokuja kuamshwa na konda, kuwa tumefika Ubungo na abiria wote wameshuka. Niliporudi nyumbani baada ya kutibiwa, ndipo nikauliza Eric alipo, nikaambiwa alifia majini akinitafuta. Alikuwa akitoka asubuhi sana na kwenda baharini kunitafuta. Kwa kuwa siku ile nilipokwenda kuogelea baharini peke yangu, niliwaachia ujumbe chini ya mlango wa chumba chao kuwa nilienda kuogelea baharini, na walionichukua pale baharini waliacha viatu na taulo langu pale pale mchangani. Kwa hiyo walijua labda nilizama, nikapotelea baharini. Eric alikuwa akishinda akiogelea baharini akinitafuta. Wanahisi mara ya mwisho alipoenda, alienda mbali sana, hakuonekana mpaka baada ya siku tatu, ndipo mwili wake ulipookotwa.” “Daah! Pole sana Enabella.” Bella alitabasamu huku ameinama. “Hizo games, alikuwa akicheza Eric mchana na usiku. Kila game mpya ikiingia, alikuwa anahakikisha anapata. Ni mchezo tulikuwa tukicheza naye sana, kama kitu cha kutuunganisha mimi na yeye. Kila game nikiiona namkumbuka Eric. Na kila nikiona maji ya kuogelea, naogopa na kuchukia. Naona ndio yaliyomuua mdogo wangu bila huruma. Sitaki Ric aingie majini kabisa. Naona ni kama na yeye ata…” Bella alinyamaza. “Nakuelewa Bella. Pole sana.” Bella alinyamaza.

“Sasa walishawakamata watu waliokuteka?” Bella alitingisha kichwa kuachiria kukataa. “Hamna hata watu unaowahisi, au angalau waliowekwa ndani kwa uchunguzi?” Bella alicheka kwa kujikejeli. “Nilikuwa nikiishi na mume wa mtu Lewis, na ninasikia ndoa ya huyo baba au baba yake Ric, iliyumba sana, na mimi nikionekana nimesababisha hayo yote,  halafu mbaya zaidi, Elvin mtoto wa Mzee Mwasha huyo wa mwisho tulikuwa karibu naye sana kitu kilichomuumiza sana mchumba wake wa wakati ule. Uchumba ulikuja kuvunjika, kwa sababu zao wenyewe, lakini yule dada alinilaumu sana mimi. Sasa sijui Lewis, yupi ni yupi na kama adui yangu ni wa upande wa baba yake Ric au mchumba wa Elvin wa zamani. Na najua sasa hivi ndiyo mbaya zaidi, kwa kuwa nimezaa naye na yeye huyo Mzee anampenda sana huyu mtoto kana kwamba ni mtoto wake wa pekee. Yaani yeye ndiye aliyemtafutia hiyo shule na ndiye anagharamia kila kitu. Hata hiyo gari unayosema naendesha ya gharama ni yake huyu mtoto. Na amempa nyumba ambayo ilikuwa na jina la mtoto wake mkubwa wa kiume. Ana watoto wawili mbali na Ric, na wote wanajua yupo mtoto mwingine niliyemzaa mimi ambaye nilikuwa ni rafiki kipenzi cha huyo binti yake mdogo. Kwao mimi ni adui na nimsaliti mkubwa sana. Kwa hiyo unaweza kuhisi ninazungukwa na maadui wa namna gani.” “Daah!” Lewis alielewa kwa upande mmoja wa maisha ya Bella, lakini alikuwa na maswali mengi sana.

Bella alicheka. “Najua una maswali mengi sana. Lakini ndio ujue wakati mwengine maisha tuliyoishi nyuma, na makosa tuliyofanya nyuma, matokeo yake yanaambatana na sisi mpaka tunapoingia kaburini. Na mbaya zaidi, gharama yake inakuwa kubwa, inawagharimu mpaka watu tunaowapenda. Lakini ukiangalia nyuma, ni kosa dogo tu ulilolifanya siku moja, iwe ilikuwa ndiyo’ yako au hapana’ yako uliyosema siku moja bila kufikiria, inaweza kuathiri maisha yako yote yaliyobaki hapa duniani. Huwa sijali maumivu ninayopata mimi, lakini naumia pale watu ninao wapenda wanapolipa gharama ya maamuzi yangu mabaya niliyoyaamua wakati fulani.” Lewis alikuwa akimwangalia Bella, aliyeonekana ni binti mdogo, mzuri na mrembo wa kuvutia, jinsi anavyoongea kwa masikitioko sana. Alionyesha amebeba mambo mengi sana moyoni mwake.

“Story upande wa Lewis.”
Walikaa pale wakila na kunywa huku wakiongea. “Sasa nani anakusaidia mtoto?” Bella alihoji. “Mimi mwenyewe sielewi. Yaani nikiangalia nyuma, nakumtizama huyu mtoto na hapo alipofika naona ni Mungu tu. Nahangaika naye huyo, mpaka namuhurumia. Leo yuko hapa, kesho kule, mara na huyu mara yule, lakini tunasogea hivyohivyo. Nilichoipendea ile shule, ni kwakuwa wanaanza kupokea watoto kuanzia saa 12 asubuhi. Kwa hiyo kila nikiamka asubuhi, namuandaa harakaharaka, naenda kumuacha pale shuleni kwao wakati naenda kazini, jioni saa 12 naenda kumchukua nakuja kumalizia kazi zangu hapa nyumbani.”  “Na siku za Jumamosi ambapo hawaendi shule?” Bella aliuliza. “Jasho huwa linanitoka. Haya kama kipindi hicho kunakuwa na mchumba wa dady, ndiye anasaidia siku hizo za jumamosi baba akienda kazini. Haya, Dady akigombana na mchumba, narudi kwa yule mwalimu wao wa darasa naenda kumuacha kwake kwa masaa hayo machache, namlipa, au akipatikana mchumba mwingine tena, tunahamisha makao.” Bella alianza kucheka. “Lewis ujue wewe huna akili?” “Alaa! Si ndio maisha ya mjini yalivyo? Nichune nikuchune, au? Wao wanapata pesa zangu na mimi wananilelea mwanangu.” Bella alitingisha kichwa.

 “Sasa kwa nini huowi?” “Si ndio hao wachumba unawapata, wengine wakija hapa wakiona huu mjengo wanachanganyikiwa wanataka ndoa, wakija kukaa na wewe siku mbili wakagundua kumbe jengo la urithi, huna hela, mshahara wenyewe mdogo, halafu wote unaishia kwenye kulipa ada ya shule ya mtoto, yeye anapata kidogo, kesho harudi.” Bella alikuwa akicheka sana. “Kwa hiyo ndio maana ukaniwahi kuniambia nyumba sio yako?” “Mapemaaaa. Usije ukaniona wa maana kumbe mwenyewe sina pesa.” Bella aliendelea kucheka. “Na sipendi sana mtu akamuona mwanangu mzigo. Nikishakusoma tu unamwangalia mwanangu visivyo, halafu nikahakikisha humpendi mwanangu, hata kama mzuri kuliko malaika, kesho hurudi humu ndani. Tena namwambia mlinzi asithubutu kukufungulia geti tena.” Bella alikuwa akicheka sana.

“Mama yake Toby yuko wapi?” Lewis alicheka sana. “Ushawahi kuona wanaume wenye viherehere?” Bella alizidi kucheka. “Basi kama hujawahi ona, huyu uliyekaa naye ni mmoja wapo.” Bella alikuwa akifuta machozi kwa kucheka. “Ndege mjanja?” “Mimi mwenyewe nilidhani hivyohivyo kuwa mimi ndege mjanja, sasa nilipoenda kunaswa! Wewe mwenyewe ungesema sikukosea kunaswa.” Bella alizidi kucheka. Lewis alikuwa na maneno ya mafumbo na yakuchekesha sana. “Nilimpenda mtoto wa mjini. Mzuri huyo, usiombe. Kila idara amekamilika. Hakuna alichopungukiwa kwenye mwili wake. Nilichanganyikiwa vibaya, ungeniona enzi hizo ungesema mimi bubu.” Bella alizidi kucheka. “Nilikuwa siongei kabisa kwa yule mtoto. Hapo ndio nimeanza maisha, nimepanga nyumba, nikanunuliwa na mzee gari. Mshahara wote ulikuwa ukiishia kwa mama yake Toby. Kila Mzee akiniambia jenga, kwani nilikuwa na pesa? Mimi kazi yangu ilikuwa kuzunguka mjini na mupenzi.” Bella alikuwa akicheka sana. “Na hela yako ya mshahara?” “Kumbe? Halafu siunajua mshahara unavyoishaga mapema. Halafu msichana mwenyewe alikuwa gharama kwelikweli, kabla hatujazunguka mwezi, mshahara umeisha. Alipoona habari za subiri mwisho wa mwezi ufike ndio nitakupa pesa, zinakuwa nyingi wakati anao mabwana wakumpa pesa kila anapotaka, hakutaka shida na mimi, akaja pale kwangu, akaniachia mwanangu, akasema yeye hakuwa tayari kuzaa wala kulea, na amepata bwana mwingine anataka kuendelea na maisha yake. Kama utani bwana, si akamuacha Toby akapotea! Nikaanza kuhangaika na mtoto na kazi. Pesa sina, nilishakopa mara kibao, tena kila mahali ili kumridhisha mama yake Toby. Sasa makato kazini yako juu, kodi pia ilinishinda kulipa. Kwanza sio kodi tu, hata bia ilinishinda kununua. Nilikaribia kuchanganyikiwa. Washikaji zangu wakawa wananicheka. Baa siwezi kwenda tena, sina hela na nina mtoto mchanga. Kijiweni mimi ndio gumzo. Kazini nilikuwa ndio shuguli. Mara niende leo, kesho napitiwa na usingizi sababu ya kubembeleza mtoto usiku kucha analia. Nusu nifukuzwe kazi. Ndio nikaamua kurudi hapa nyumbani nijisalimishe kwa wazazi. Walikuwa hata hawajui kama nina mtoto. Cha kwanza mama akaenda kumpima kama ni wangu. Bwana majibu kutoka, mtoto ni wangu kwa asilimia 100. Mama akaanza kumlea, huku natukanwa na Mzee kama mtoto mdogo. Akanipa muda wakufanya kazi na kulipa madeni ya watu wote, tena yote. Ikawa ni kazi ya kwenda kazini, mshahara nalipa madeni, risiti namletea Mzee, mpaka nikamaliza. Nilikuwa na shahada moja tu wakati ule, sikutaka kusoma sababu ya pombe na wanawake, utafikiri nilikuwa nimelogwa!” Bella alikuwa akicheka sana.

“Unafikiri nakutania Enabella? Nilikuwa nikiona wasichana nakuwa kama nimechanganyikiwa. Basi bwana, Mzee akaamua nirudi shuleni, hapo mama ananisaidia kulea mtoto.” “Umezaliwa peke yako?” “Nina dada zangu. Wanapenda shule hao, kama sijui nini. Baba alikuwa akiniambia ‘utakuja kutawaliwa na dada zako. Wewe endekeza starehe tu.’ Kwani nilikuwa nasikia? Mimi na starehe, starehe na mimi. Nilikuwa nalala klabu. Nilipoona hapa wananifuatilia, nikahama hapa nyumbani, nikaenda kupanga na ndipo kipindi hicho nikaangukia kwa mama yake Toby. Sasa nilipoishiwa ikabidi nirudi tena.” “Sasa hao dada zako wako wapi?” “Wapo hapa hapa mjini.” “Kwa nini hawakusaidii mtoto?” “Kwanza ukiwaona tu, utafikiri walimu wa shule zile wanazochapa watoto.” Bella alizidi kucheka. “Wakorofi hao! Halafu kila mmoja anamaisha yake, hawataki kubebeana mizigo. Hata kuonana ni shida, wakati wote tupo hapahapa mjini. Kuna mmoja nilishafanya kazi chini yake kwenye kampuni moja, wakanifukuza kazi.” Bella alianza kucheka tena.

 “Kwa nini?” “Si nilitaka kumpiga.” “Umpige dada yako!?” “Tumepishana sijui mwezi sijui mwaka, hata sielewi. Sema chenyewe kiliunganisha shule nyingi nyingii, kikamaliza mapema. Anajidai msomi huyo! Sasa wakati huo ndio mama na baba wamefariki, nahangaika na mtoto tena, kazini nikawa nachelewa, eti yeye badala anielewe ndio amekazana kunifuatilia. Mara aniite mbele za wakubwa wenzake, mara aniandikie barua za kunionya kuchelewa kazini. Nikimwambia ni sababu ya mtoto, ananiambia kwa nini sikufikiria hayo yote wakati namzaa. Sasa siku hiyo tulilala na mtoto alikuwa akichemka homa kweli, na mimi nilikuwa nahitajika kwenye kikao, wamiliki wa hiyo kampuni walikuwa wamefika, kutoka South Africa, ni makaburu. Nikaamka na mtoto akiwa bado anahoma kali, nikamkimbiza hospitalini. Nikiwa hospitalini simu zikaanza, ananipigia. Nikaona isiwe shida na kwakuwa nilishaandikiwa barua nyingi za maonyo, nikaona nitafute mtu pale pale hospitalini, anishikie Toby kwa muda wakati tunasubiri majibu, hapo tumeshapima kila kitu, nikamuachia huyo mtu hata simfahamu, mimi nikakimbilia ofisini, ili tu kuepusha shari na yeye. Nikafika kikao kinakaribia kuisha, halafu yeye ndio afisa mwajiri wa kampuni. Si akaanza kunigombesha bwana! Hapo nina usingizi, halafu mwanangu nimemuacha na mtu hata simfahamu vizuri, ili niwahi, eti yeye akaanza kunigombesha. Sijui nilipandwa na nini bwana, nilinyanyuka pale nilipokuwa nimekaa, nikaenda kumnyanyua alipokuwa amekaa kwenye kiti, mpaka juu kabisa. Nikataka kumuwasha vibao, nikakumbuka ni mtoto wa kike. Nikamuweka chini kwa nguvu, nikaondoka kurudi hospitalini. Tulikaa hospitalini siku mbili, mtoto anatibiwa, siku inayofuata baada ya kuruhusiwa nikarudi kazini, nikaambiwa sina kazi.” Bella alibaki ametoa macho. “Mjini shule, Enabella. Wewe acha tu.” “Pole.” Bella alitoa pole huku ametoa macho.

“Lakini imenisaidia sana kuishi kiakili. Kifo cha wazazi wetu, na kukimbiwa na mama yake Toby, kumenibadilisha sana. Isingekuwa hivyo hata hii nyumba ningeshaiuza.” “Wazazi walifariki na nini?” “Ajali bwana. Walikuwa wakienda kwenye msiba wa babu kijijini, gari likapata ajali njiani, walikufa wote mpaka dereva. Tena hapo hapo. Halafu mimi ndio nilikuwa nikiwaendesha dada zangu wote watatu. Yaani ilitokea mbele ya macho yetu, tukiwatazama wazazi wetu wakifa. Ilikuwa mbaya sana. Watu hawakuweza hata kuangalia maiti siku ya mazishi. Ilikuwa mbaya sana.” “Pole sana Lewis.” “Ndio hivyo bwana. Kwa hiyo kwa kuwa mimi ndio nilikuwa nikiishi nao hapa, wakasema nibaki hapa kuangalia nyumba. Wao wakagawana nyumba nyingine na mali nyingine walizoacha. Hata hivyo wamejijenga sana hao dada zangu na waume zao, hakuna hata aliyenisumbua. Ndio nikajishindia hili jumba, naishi na Toby, kimya wenyewe.” Bella alibaki akimwangalia Lewis huku akicheka.

“Lakini lazima uoe Lewis.” “Kwani sijajaribu? Kwanza nataka mwanamke mzuri. Sitaki nije kuwa na mke wangu ndani huku natamani wanawake wengine nje. Katika hilo sitakuwa mnafiki na wala sidanganyi. Nataka kuoa mwanamke mzuri kweli kweli. Sasa tatizo la hao wanawake wazuri wa hapa mjini, wanataka mamilionea, na mimi pesa sina.” Bella alikuwa anacheka sana. “Na mimi siwezi kukaa na mwanamke unayeweka pesa kwake utafikiri benki! Huo ujinga sifanyi. Nataka mwanamke mzuri  lakini pia awe anajua kutafuta pesa pia. Wote tuwe watafutaji, sio kugeuzwa mimi kitega uchumi. Nilifanya kosa sirudii kosa. Na usije ukasema Lewis mchoyo. Hapana, hata mimi najua kuhonga bwana, lakini vinamwisho. Khaa. Utaendelea kuhonga mpaka kwenye ndoa! Mtajenga saa ngapi? Mtakuwa hamna maendeleo.” “Ni kweli.” Waliongea siku nzima. Bella alijisahau kabisa kama amemuacha Elvin nyumbani. Walikaa mpaka ilipofika usiku.

“Sasa mimi mara nyingi siku za Jumamosi huwa siendi kazini, uwe unamleta Toby wakati unaenda kazini.” Bella alikuwa akiongea mara baada ya kupanda kwenye gari wakati wanaondoka. “Mmmmh!” Lewis aling’ata meno kwa nguvu. “Nini sasa?” “Mimi sitaki uje utuchoke bwana, uanze kuacha kupokea simu zangu.” “Acha utoto Lewis. Siwezi kufanya hivyo. Si nikichoka nitakuwa nakwambia tu.” “Kweli unaniahidi ukichoka utakuwa ukiniambia?” “Kweli Lewis. Kwanza mwanao wala haitaji msaada wa hivyo. Umemfundisha vizuri sana. Anajitegemea kwa kila kitu. Anahitaji mtu tu wakumuwekea chakula na akimaliza kula namuona anakuwa anatoa chombo chake mwenyewe. Kwa hiyo usiwe na wasiwasi, nikichoka mimi, mama atakuwepo. Na mama anapenda sana watoto.” “Mbona utakuwa umenisaidia sana. Si tunaanza haraka iwezekanavyo?” Bella alicheka. “Wewe ukibanwa na majukumu, mlete nyumbani au hata ukishindwa kumchukua shuleni, wataarifu kuwa mimi au mama au baba tunaruhusiwa kumchukua Toby. Usiwe na wasiwasi.” “Asante sana, jumatatu nitaenda kujaza hiyo fomu pale shuleni kwao, niwaongeze majina yenu ili muwe mnaruhusiwa kumchukua Toby. Mbona maisha yatakuwa marahisi hapa mjini!” Bella alicheka, akaondoka kurudi nyumbani kwao.

***************************************************

Bella alirudi nyumbani ilishakuwa usiku wa saa tatu kwenda saa nne. Eli alianza kucheka mara Bella alipoingia ndani kwa kupitia mlango wa nyuma. “Sasa unacheka nini badala uje unipokee mtoto!?” “Hivi yule jamaa, anaitwa nani tena?” Eli aliuliza. “Yupi?” “Yule uliyekwenda kwake.” “Si anaitwa Lewis. Kwani vipi?” “Anaonekana jamaa king’ang’anizi kweli! Siku nzima amekung’ang’ania.” “Eli bwana usiseme hivyo!” Bella alinong’ona. “Kama unamuhofia baba na mama, basi ujue na Elvin yupo pia hajaondoka, yuko hapo sebleni anakusubiri.” “Acha kunitisha bwana!” Eli aliendelea kucheka. “Saa tatu inakwenda saa nne, mtoto wa kike ndio unarudi nyumbani!  Watoto wa kiume wote tumerudi ndani. Wewe unahangaika mtaani! Sasa kama ulikuwa unazurula ukijua ukirudi hapa Elvin hayupo atakuwa amerudi kwake, sasa ujue umechemka leo. Yupo hapo sebleni, amekaa na Mzee.” Bella alitulia. “Muone alivyopooza sura.” Eli aliendelea kucheka.

*********************************************************

Ilikuwa ni siku iliyopita tu Bella alipomfanyia Eli sherehe nzuri sana ya ‘birthday’. Aliandaa usiku huo maalumu kwa ajili ya kusherehekea siku ya kuzaliwa ya Eli. Hakuwa amemwambia. Alimpigia simu baada ya kutoka kumchukua Toby shuleni, wakarudi nyumbani, baada ya wote kujiandaa, ndipo akampigia simu Eli, akamwambia anaomba wakutane kwenye ile hoteli, anashida sana, anataka ushauri wake. Eli alikuwa yupo baa na rafiki zake, akatoka baa akaelekea huko alipoandaliwa sherehe hiyo bila kujua. Alipofika hotelini alishangaa kukuta wazazi wake, JJ na watoto wake, wote wapo mezani wakimsubiri, alipokaa tu, kabla hata hajasalimia, akashangaa wahudumu wa pale kwenye ile hoteli, wote wakiwa kwenye sare zao za kazi, wamewasogelea kwenye meza yao wakimuimbia yeye wimbo wa birthday. Eli alibaki akimtizama Bella. Ndipo alipotoa zawadi nzuri, yeye na wazazi wa Eli na kumkabidhi Eli. JJ naye akampa zawadi yake na wanae wakatoa zawadi na Ric naye alimpa mjomba wake zawadi pia. Eli alibaki ameduwaa. Walikaa huko kwa muda mrefu wakiongea na kucheka, ndipo wakarudi nyumbani.

*******************************************************

“Umekamatwa utamu leo. Jamaa kajaa tele leo. Utakoma.” “Lakini mbona sijachelewa?” “Weee! Acha kabisa Bella. Tokea asubuhi umeondoka hapa nyumbani, tena watu tulikuwa tumelala, unarudi saa hizi! Michezo hiyo michezo gani? Kwanza mtoto mwenyewe amelala. Sasa leo utajieleza aliyekuwa anacheza ni mtoto au wewe.” “Bwana Eli hebu nyamaza. Utamuingizia wasiwasi Elvin.” “Mara ya pili? Hajala tokea alipoamka.” “Sasa kwa nini hamjampa chakula jamani Eli!?” “Apewe na nani?” “Si wewe?” “Ushamuona akila chakula nilichotayarisha mimi?” “Basi hebu pokea mtoto nimwandalie chakula haraka.” Eli alimpokea mtoto akaanza kucheka tena.

“Yaani wewe mpaka mtoto ukamuogeshea hukohuko kwa watu na kumbadili kabisa nguo za kulalia! Kweli ulijiandaa. Tena unaonekana ulikusudia kuchelewa kabisa.” “Tafadhali Eli naomba upunguze sauti. Begi hilo la mtoto ninalotembea nalo lina kila kitu chake kwa ajili akienda kwa baba yake. Kwa hiyo wakati Lewis anamuogesha mwanae akamuogesha na Ric.” Eli alicheka kwa sauti sana. “Ndio maana umechelewa! Kumbe jamaa amehakikisha anakufanyia maonyesho yote. Mpaka ukavutiwa. Ulikuwa hutaki kurudi nyumbani wewe.” “Nenda kamlaze mtoto Eli, na unyamaze. Tafadhali sana.” Eli aliondoka huku akicheka.

“Jamani eeh! Bella karudi. Msije kusema amechelewa kurudi. Karudi mapema ya saa nne kasoro na uzuri amerudi na mtoto ameshaogeshwa kabisa na Lewis.”  Eli alitangaza kwa nguvu huku akicheka. “Eli kamlaze mtoto na acha kelele ataamka.” “Sawa mama. Lakini umesikia kuwa mtoto ameshaogeshwa? Kwa hiyo huna haja bibi mtu ya kumuogesha mtoto tena, Lewis ashamuogesha.” “Nenda bwana wee. Muache mwanangu.” Kidogo Bella alitulia. Akaamua asogee sebleni huku akinyata. Kweli alimkuta Elvin, na wazazi wake pale sebleni wakiangalia tv. “Shikamooni.” Wote walimgeukia. “Samahani nimechelewa.” “Wewe usimsikilize Eli. Anakuchokoza tu.” “Eti mama eeh? Sijachelewa sana?” “Kidogo tu, lakini siku nyingine ujitahidi kuwahi kidogo.” Bella alibaki akimwangalia Elvin ambaye alishageukia Tv.

Alienda kukaa pembeni yake kwa utaratibu sana. “Vipi Vin?” Elvin alimgeukia akamwangalia kwa muda kisha akageukia tv. “Nilikusubiri uamke ili nikwambie naenda kumpeleka Ric, nyumbani kwa rafiki yake Toby kucheza, lakini hukuamka. Ndio nikaona niende tu.” Bella alikuwa akiongea kwa sauti ya chini sana lakini watu wote walikuwa wakiwasikiliza. Elvin alibaki kimya. “Umekula Vin?” Bella aliuliza tena kwa upendo.  “Wewe si nimekwambia hajala? Umezurula wee, sasa hivi ndio unamkumbuka. Eti, ‘Umekula Vin?’ Utakoma leo na kisauti chako hicho!” Eli aliitikia yeye na kuigiza sauti ya Bella. Mzee Mwasha na mkewe wakacheka. “Naomba uondoke Eli, uniache mimi na Elvin.” “Umekula huko, umeshiba ndio unakuja kumdanganya mwenzio. Na hakujibu leo. Rudi hukohuko ulikotoka kwa nani tena?” “Sitaki.” Bella alijibu huku amekasirika, lakini Eli aliendelea kuchochea. “Saa nne kasoro? Lewis huyo, Lewis gani!?” “Eli hebu nyamaza.” “Sawa mama. Lakini wewe kwa nini humuulizi Bella kama hapakuwepo na saa huko alipokuwepo? Anarudi nyumbani mida hii! Kujisahahu gani huko!?” Mzee Mwasha alikuwa akitingisha kichwa huku akicheka kimya kimya.

“Kweli Bella amebadilika! Wewe ndio wakumuacha Elvin ndani na kwenda kukaa kwa Lewis siku nzima!” “Eli ondoka bwana.” Bella alienda akamsukuma Eli mpaka nje, kisha akamfungia mlango. “Uchonganishi tu. Kwa nini hufikirii swala la foleni njiani?” “Jumamosi hii! Usitudanganye bwana. Foleni za usiku zinatokea wapi? Au mlitoka nje ya mji kidogo? Maana foleni za usiku zinakuaga za Ubungo kuingia jijini kutoka mikoani.” “Mungu wangu Eli wewe!” Bella akamfungulia mlango. “Utapata dhambi Eli wewe!” “Na wewe kwa nini umemfungulia mlango? Ungemuacha hukohuko nje.” Mama Mwasha aliingilia. Eli na baba yake walikuwa wakicheka sana. “Mlienda wapi Bella, best wangu?” “Mungu wangu ni shahidi, nilikuwa nyumbani kwake Lewis. Naomba Elvin usimsikilize Eli. Kweli nilikuwa nyumbani kwa Lewis.” “Ona jinsi anavyolitamka hilo jina la Lewis. Ndio maana jamaa alikuwa hakuachii huko.”  Mwasha na mkewe walizidi kucheka. “Wala sikusikilizi tena.”

Bella alirudi kukaa pembeni ya Elvin. “Nakuomba usimsikilize Eli kabisa, Vin. Ngoja nikakuletee chakula.” “Kwa hiyo huu muda uliorudi nyumbani unaona ni sawa Bella?” Elvin aliuliza. “Ehee! Jibu sasa.” Eli alidakia. “Naomba tukaongelee chumbani Vin, tafadhali.” “Anataka akakudanganye huko! Usikubali Elvin. Akujibu hapahapa wote tumsikie.” “Hayakuhusu Eli.” Bella alishabadilika. “Utamliza Bella bwana. Eli nyamaza.” Bella alishaanza kulia. “Usilie bwana Bella, wewe wangu. Nakutania tu.” “Umeona umemuudhi Elvin sasa?” “Elvin kachukia kwa kuwa umeondoka tokea asubuhi amelala, tena hukumuaga, umemuacha hapa bila chakula halafu umechelewa kurudi. Sio maswala ya mtoto kuogeshwa na kuvalishwa nguo za kulalia kabisa, hapana.” Mzee Mwasha na mkewe walishindwa kujizuia wakacheka kwa sauti. “Ona unarudia yaleyale! Unazidi kuharibu Eli jamani! Naomba unyamaze wala hunisaidii hapo. Unazidi kuharibu.” “Kuharibu swala la kuchelewa kurudi nyumbani, tena ukiwa na mtoto aliyepelekwa kucheza akiwa amerudi amelala au ni juu ya swala la mtoto kurudi akiwa ameogeshwa huko huko wakati baba yake amechimba kisima cha maji hapa, maji yanatoka mpaka vyumbani? Tena na sinki la kuogea mzee wa watu kajenga jipyaa, la kisasa.” “Eli wewe  jamani!” Bella aliendelea kulia. “Eli naomba uondoke sasa hivi. Ushamliza Bella, umefurahi. Sasa nenda.” “Sawa baba. Usiku mwema. Kesho nitamnunulia Bella wangu saa ya mkononi, nzuriii, ili awe anatunza muda.” Eli aliondoka huku akicheka. “Usiku mwema Bella wangu eeh.” “Sitaki.” Eli alicheka akatoka na kufunga mlango.

“Naomba tukaongee Vin, tafadhali.” Elvin alinyanyuka nakuelekea chumbani kwake. Bella alimfuata nyuma. Akaenda kukaa karibu yake pale pale kitandani. “Samahani nimechelewa kurudi nyumbani.” Bella alikausha machozi na kumtizama Elvin. “Siku nyingine sitachelewa tena.” “Kumbe kuna siku nyingine tena!?” “Toby ni rafiki wa Ric, Vin. Nampeleka huko ili wacheze. Naona anakuwa anakaa hapa na watu wazima tu. Na Toby ni mtoto mzuri, anamsaidia sana Ric kuongea na kuzoea maisha haya ya kawaida.” “Huyo Lewis ameoa?” Bella alianza kupatwa na wasiwasi. “Hajaoa.” Simu ya Bella ikaanza kuita. Alikuwa Lewis. Elvin alibaki akimwangalia. “Naomba niipokee. Nimsikilize.” Elvin hakujibu akabaki akimwangalia. “Haloo Lewis!” “Vipi?” “Safi tu.” “Nilikuwa nataka kujua kama mlifika salama.” “Ndiyo, tulifika salama kabisa. Asante.” “Haya. Usiku mwema.” “Asante na nyinyi.”  Bella alibaki akiiangalia simu yake.

“Ulisema rafiki ni Ric na Toby au ni wewe na Lewis?” “Elvin! Wewe unanijua Vin, siwezi kukudanganya.” “Watu wanabadilika sana Bella. Na hivi mimi nimeoa, na umesema kila mtu aendelee na maisha yake! Sasa sijui mwenzangu ndio umeendelea au la?” “Siwezi kubadilika Vin.” “Naona umeanza kubadilika Bella. Umeweza kuniacha hapa kitandani, nakuondoka, unarudi nyumbani mida hii! Hata kupiga simu kunijulia hali?” “Sikujua kama utakuwa umeamka Vin. Sikutaka kukuamsha.” “Ulimpigia hata mama simu kuniulizia?” “Hapo nilipitiwa Vin. Sikupata hilo wazo. Naomba unisamehe. Kweli sikufanya vizuri.” “Lakini unajua mimi nisingekuacha Bella. Hata iweje, nisingekuacha. Nakuthamini sana kuliko mimi mwenyewe. Huwa ikifika swala lako, kila kitu kinasimama, unakuwa wewe kwanza.” Bella alianza kulia. “Nimekosa Vin, naomba unisamehe. Siku nyingine sitarudia tena. Nilijisahau.” Elvin alivuta mto, akajilaza chali pale kitandani.

Bella alijivuta pembeni yake akajilaza ubavuni kwa Elvin. “Samahani Elvin. Nimekosa. Sitarudia tena.” “Yameisha Bella.” Elvin alimvuta karibu yake akaanza kumfuta machozi. “Usinitupe Bella bwana. Hasa kipindi hiki. Napitia kipindi kigumu sana cha maisha. Nakuhitaji sana.” “Siwezi Vin. Nakuhakikishia hakuna chochote kilichotokea kati yangu na Lewis. Na nina kuhakikishia hakuna kitakachotokea. Tulikuwa tukiongea tu, wakati watoto wanacheza. Sema tulikuwa ndani, mpaka tunatoka nje, ndio nikagundua giza limeingia.” Elvin alibaki akimwangalia. “Naomba ule Vin, usilale bila kula.” Bella alikuwa akiongea naye taratibu sana. Hasira zote zilimuisha Elvin. “Nikulete humu ndani au nikuwekee chakula mezani?” “Nitakuja kula mezani.” Bella alifurahi sana. Alimbusu shavuni. “Nakupenda Elvin.” Akasimama, akatoka kuelekea jikoni.

Mama Mwasha alishapika, kwa hiyo alipasha moto kile chakula harakaharaka, wakati anakiandaa mezani, Elvin alitoka. “Uliamka saa ngapi?” Bella alimuwahi kwa swali. “Kama kwenye saa sita hivi. Nikabaki nimekaa kitandani nikitegemea utakuja kuniangalia, kumbe mwenzangu uliondoka.” “Basi Elvin. Siku nyingine sitaondoka bila kukuaga. Hata kama umelala, nitakuamsha nikuage kwanza ndio niondoke.” Elvin alitabasamu. “Njoo ule. Chakula kipo tayari.” Walikaa wote mezani Bella akiongea huku Elvin akila. “Unajua nini Elvin?” “Nini?” “Siku nyingine itabidi twende wote. Lewis anakufahamu, nilimsimulia kila kitu juu yako. Kwa hiyo anakufahamu.” Mzee Mwasha na mkewe walikuwa wakiwasikiliza huku wakicheka kimya kimya, mwishowe walienda kulala na kuwaacha wakiongea hapo mezani.

***************************************************

Bella alizidi kuwa karibu na Lewis akimsaidia mambo ya mtoto. Kila Lewis alipozidiwa na kazi ofisini, Bella alikuwa akienda kuwachukua watoto wote shuleni. Anarudi nao nyumbani, anawalisha na kuwaogesha. Mara nyingi Lewis alipita kumchukua Toby akiwa amelala. Alianza na kuzoena na familia ya Mzee Mwasha. Alikuwa akikaribishwa hata siku za Jumapili ambazo wanakutana kama familia na yeye alikaribishwa. Akawa akija yeye na mtoto wake pale nyumbani baada ya ibada na wakati mwingine alienda kanisani kwa kina Bella. Walizoeana sana na Bella. Simu za hapa na pale hazikuisha. Kutakiana usiku mwema, kuulizana kama uliamka salama, lilikuwa jambo la kawaida kabisa.

“Mbona huyu Lewis ni kama amezidi?” “Naomba usianze Masha. Wewe mwenyewe ulinituma nikawatafute wazazi wa Toby, nimewapata unaanza kulalamika.” “Mbona sijawahi kumsikia mama mtu. Nakuona na baba yake tu?” “Wala hamna shida, huwa wanacheza siku za jumamosi, wanakuja hapa au nampeleka kwao. Wewe uwe unampeleka basi, na siku wanazotaka kuja kwetu uwe hapa unashinda nao. Tena itakuwa vizuri utapata muda mwingi na Ric.” Mzee Masha alitingisha kichwa. “Nini sasa? Maana najua shida yako ni kuniona mimi na Lewis. Sasa nishakusaidia kutafuta ufumbuzi, ushindwe wewe mwenyewe.” Mzee Masha alikuwa ameenda nyumbani kwa Mwasha kusalimia baada ya kutoka safari, akakuta kina Toby na baba yake nao wanatoka. Mzee Mwasha na mkewe walikuwa sebleni wakiwasikiliza wao wakiwa wamekaa kwenye meza ya chakula.

“Nimekuletea zawadi Bella.” “Akuu! Sina shida hata kidogo. Zawadi mpe mwanao. Wala usijisumbue na mimi. Sitaki hata shilingi yako.” “Kwa hiyo hizi zawadi nilizokuletea nifanyaje?” “Sijui wala sitaki kujua Masha. Hainihusu. Wewe nipe habari za waliohusika kuniteka nyara, basi.” “Ndio nimetoka safari Bella. Hata sijapumzika.” “Mbona kama nakuhisi unanificha? Au mkeo ndio anahusika nini?” “Umeanza Bella.” “Mbona hunitajii wakati uliniambia umewafahamu kwa asilimia fulani?” “Tatizo lako unaharaka sana wewe.” “Mimi nakujua jinsi unavyokuwa, pale unapokuwa hujapata majibu ya mambo yako. Hasa yanayonihusu mimi. Huwi hivyo Masha. Umetulia kabisa. Ule moto wakutafuta walioniteka umeisha. Kwangu inaniashiria umeshawapata, ila hujui kitu chakuwafanya. Wewe sio mtu wakutulia hivyo Masha.”  Masha alitulia kimya hakujibu.

“Sasa nakwambia ukweli Masha, nitawatafuta na nitawapata. Na nikiwapata, utaniona mbaya. Hata kama ni Zera au Junior ndio wamehusika, watawajibika.” “Utawapataje?” “Wewe umesahau niliishi Kigogo? Sasa ni heri uwaambie hao wanao au mkeo, waje wajisalimishe wenyewe, wakikamatwa huko barabarani, watalipa kuanzia ubaya ulionifanyia wewe, na wao kwa kumuua mdogo wangu. Nakuapia Masha. Sitatulia mpaka niwalipize kisasi wewe na familia yako. Kwa hiyo ukajipange sawasawa. Waambie nakuja. Na nikija, nitakuwa kama kifo, sitawahurumia kama wao walivyonitenda au kama wewe ulivyonitenda unyama, na mimi nitawalipiza. Na nilikwambia Masha, kabla hujafa, utaona kwa macho yako, ubaya ulionitendea mimi, Zera naye akitendewa. Mbele ya macho yako.” “Hivi unakumbuka kuwa wewe unajukumu la mtoto lakini? Au unafikiri jukumu lako liliishia kwa Eric peke yake? Kwa nini unataka kujiingiza kwenye vita ya hatari namna hiyo? Unataka ujitoe kafara kwa maisha yaliyopita! Kwa nini usishukuru Mungu amekupa nafasi nyingine yakulea mtoto wako, ukatulia na kuniachia mimi nihangaike na mambo mengine? Hivi unaona thamani yeyote ya huyu mtoto au huoni? Eti Bella? Unamthamini huyu mtoto kweli wewe?” Bella alipooza gafla nakuanza kulia. “Au unafikiria mimi ndio najivunia kwa mabaya niliyokutendea?” Bella alisimama na kuingia chumbani kwake akaendelea kulia. Mzee Masha naye akatoka bila kuaga.

“Gafla Happiness abadilika”

Jioni ya siku inayofuata Elvin alirudi nyumbani akiwa amepumzisha akili na tayari kwa ugomvi wa usiku huo ili alale. Alihakikisha amekula kabisa kabla yakuondoka nyumbani kwao, kwani alijua mazingira ya nyumbani kwake, anaweza asikute chakula kabisa au akakuta amewekewa mezani na nzi wakiendelea kukila. Alipofika tu alimkuta Happiness sebleni, alisalimia bila hata kumwangalia vizuri, akataka kupitiliza chumbani. “Vipi huko, wazazi hawajambo?” Happiness aliongeza baada ya salamu, kwa sauti yake nzuri na ya upole. Elvin alishtuka kidogo, akahisi hajasikia vizuri. Alisimama kwa muda kisha akamgeukia bila hata kuuliza. “Nauliza hali ya baba na mama huko nyumbani.” “Hawajambo!” Akiwa kwenye mshtuko, aligeuka na kuingia chumbani huku akiwaza kumetokea nini. Chumba kilikuwa kimesafishwa, mashuka masafi. Alibaki amesimama akijiuliza kulikoni.

Mara mlango ulifunguliwa, Happiness akaingia. Elvin alitegemea aanze maneno kama kawaida, akaona kimya. Akamgeukia, akagundua amesukwa nywele vizuri. “Umependeza.” Elvin alirushia neno kwa tahadhari sana. “Asante. Nikuletee chakula?” “Nimeshakula nilipokuwa nyumbani.” Happy alitulia. “Na wewe umekula?” “Nilikuwa nakusubiri tule wote.” Happiness alijibu kwa unyenyekevu sana. Elvin alitabasamu. “Twende basi nikakusubiri wakati unakula.” “Kwanza naomba nikuombe msamaha kwa maneno niliyokutukana juzi, Elvin. Naona nimekosea kukushtumu na Bella, wakati umeniapia hujalala naye tokea arudi.” “Sio tokea arudi, Happy. Sijawahi kufanya mapenzi na Bella. Naomba uniamini.” “Nakuamini mume wangu. Naomba unisamehe na yaishe. Nahisi ni wivu tu. Niliona ni kama hutaki kunitambulisha kwa Bella. Niliona ni kama unanificha kwake.” “Sio kweli. Tokea siku ya kwanza Bella anarudi nyumbani, alijua nilishaoa. Pale ni nyumbani kwa kina Bella pia. Wazazi wangu wanaishi nae kama mtoto wao, na yeye anakutambua kama mke wangu. Kwa hiyo usiwe na wasiwasi.” “Kwa hiyo utaenda kunitambulisha?” “Ni kwa kuwa tu hutaki kwenda nyumbani, ndio maana hujakutana naye mpaka leo. Lakini yeye yupo ofisini hata jumatatu tutaenda wote kukutambulisha kwake. Hilo halina shaka.” Happiness alijisogeza kwa Elvin akambusu kwa furaha.

Wanandoa hao ilishapita muda mrefu sana bila hata kushiriki tendo la ndoa sababu ya ugomvi usio isha. “Naona hata hamu na mimi imekuisha Elvin. Hutaki hata kunikumbatia.” Happiness aliongea kwa kulalamika kidogo, baada ya kumbusu Elvin na kubaki ametulia kama aliyekuwa amepata busu kutoka kwa mke wa kaka yake. “Nina hamu na wewe mume wangu.” Happiness aliendelea kumbembeleza Elvin kumtaka kimapenzi huku akijaribu kurudia kumbusu na kumpapasa. “Mbona hata hustuki Elvin jamani!?” Happy alilalamika, Elvin hakutaka kujibu kitu ili kuepusha maneno. Alimuweka mkewe kitandani, na kuendelea kufanya naye mapenzi huku akiwa kwenye mshtuko mkubwa. Happiness alikuwa ameoga vizuri, ananukia kawaida kama mtu msafi tu. Walimaliza, wakaoga nakurudi wamekaa kitandani, Elvin akiwa hajui aongee nini.

“Nimefurahia kweli leo Elvin. Umeniridhisha mume wangu. Nilikuwa na hamu na wewe.” Happiness alitupia neno, Elvin aligeuka akambusu shavuni bila ya kuweka neno. “Asante. Lakini naona nivizuri nirudi kwa Mama Mwasha nikaombe radhi, turudishe mahusiano.” Elvin alikaa akamtizama Happiness. “Ni nini kinaendelea Happiness.” “Nimeamua kutafuta amani Elvin.” “Mbona imekuwa gafla sana?” Elvin alihoji. “Wewe unafurahia haya maisha?” Happiness alitaka kuanza, lakini ni kama aliyekumbuka kitu, akajirudi. “Nataka turudishe amani kwenye nyumba yetu mume wangu, kwa ajili yetu sisi wenyewe na watoto wetu.” Elvin alibaki akimtizama. “Au hutaki nirudi tena kwenu?” Elvin alitulia kwa muda akimtizama. “Una uhakika Happiness? Kwa kuwa sitaki urudi kule tuaze matatizo. Ni heri tubaki na matatizo yetu sisi wenyewe. Ile nyumba ya wazazi wangu hawajui wala hawawezi ugomvi.” “Ndio maana nimesema naomba nikaombe msamaha. Wakishindwa kunisamehe basi.” Elvin alijirudisha kulala kwenye mto wake huku akiwaza. “Mbona kama hutaki Elvin, mume wangu? Wewe umesema unataka amani, nimejifikiria nikaona ni kweli, kwanza mimi mwenyewe sina raha. Yaani hata kesho naomba unipeleke kwenu nikaombe radhi. Au hutaki?” Baada ya muda Elvin alijibu, “Sawa.” Lakini jibu yake alionyesha wazi alikubali tu, lakini hakuwa ameridhika kabisa. Alimjua mkewe.

Mabadiliko ya gafla ndio yalizidi kumchanganya hasa baada ya ugomvi uliopita. Alirudi nyumbani mapema siku hiyo ya ijumaa, akaingia kuoga haraka haraka, bila hata kujibizana na Happiness aliyekuwa akiangalia runinga chumbani hapo wakati amejilaza kitandani. Elvin alisalimia lakini hakujibu ile salamu. Wakati anavaa, Happiness alianza kumuuliza mbona ni kama anaharaka yakutoka na wakati ndio ameingia tu hapo nyumbani? Ndipo akamweleza mpango mzima wa sherehe Bella aliyomwandalia Eli, kwa ajili ya siku yake ya kuzaliwa, na akamwambia familia yote ya Mwasha, wapo hotelini, anasubiriwa yeye tu kwa kuwa alichelewa kazini. Happiness alianzisha ugomvi ambao Elvin hakutegemea, akidai kwa nini hataki kwenda naye, ni muongo, anataka akakutane na Bella tu, na shutuma nyingi sana, ikiwepo na pafyumu aliyojipulizia usiku huo ilikuwa ni kusudi anukie vizuri kwa Bella huko wanapoenda kukutana wakati wanafanya mapenzi. Hakuna jinsi Elvin alivyojieleza Happiness akakubali hata kumsikiliza. Alimwambia hata kama yeye angependa kwenda, anakaribishwa, lakini alimfungia mlango akaondoka na funguo. Elvin alikaa hapo chumbani akiwa amefungiwa  mpaka saa sita usiku ndipo Happiness alipofungua mlango akimtaka atoke, kwa kuwa yeye na mtoto wanataka kulala. Kwa sababu ya kelele nyingi Elvin alitoka na kwenda kulala kwenye gari mpaka asubuhi ndipo alipokwenda kwao.

Happiness ajirudi. Ataka ndoa yake na amani na wakweze, lakini mabadiliko hayo yanamtia wasiwasi mumewe. Nini kitatokea?

Usikose Sehemu ya 19.

*My Past* Sehemu ya 17.

*My Past*
Sehemu ya 17.

Ulikuwa ni muda mzuri sana kwa Bella na mwanae. Alijifunza mapishi mengi sana kutoka kwa Mama Mwasha, akawa akimpikia mtoto wake vyakula mbali mbali. Mama Mwasha alikuwa mtaalamu zaidi kwenye maswala ya kulea, kwani alilea watoto wake wote bila usaidizi kutoka kwa mtu yeyote. Kwa hiyo alimfundisha Bella, jinsi ya kulea mtoto wake. Kwa muda mfupi Bella akajikuta mtalamu wa maswala ya watoto, na akaweza kumlea mwanae bila shida. Yeye mwenyewe ndiye alimuogesha na kumvalisha mtoto wake, hakutaka msaada wa mtu yeyote.

Masha naye akaanza mabadiliko aliyoyasema. Kila alipotaka kubadili kitu pale kwenye ile nyumba ya Mwasha, alimpigia Mzee Mwasha simu siku moja kabla na kumtaarifu sio kuomba ruhusa, kuwa mafundi watafika hapo siku inayofuata kubadili hiki au kile. Kwa haraka sana alijenga uzio kwenye ile nyumba. Ndani ya siku tatu kulijengwa uzio mkubwa na wakisasa hapo nyumbani kwa Mwasha. Walifika mafundi wengi sana huku wakisimamiwa na askari. “Sasa wanaojenga hapa ni askari au mafundi?” Bella alitoka kuongea na Masha mara aliposikia minong’ono kutoka kwa watu waliokuwa wakifanya kazi hapo nje kuwa Masha amefika. “Sitaki kuja kujuta baadaye, adui zangu wanaweza kujipenyeza hapa hapa wakajidai na wao kama ndio mafundi.” Bella alimtizama, kisha akaondoka. Hakutaka kuongeza jambo. Akang’oa geti lililokuwepo na kuweka geti alilochagua yeye mwenyewe Masha. Akahakikisha anajenga kwa haraka sana sehemu ya kuchezea mtoto wake pembeni ya nyumba ya Mwasha ndani ya huo ukuta, tena bila kuwaomba familia hiyo na akaongeza ulinzi kama alivyoahidi.

Walishangaa siku moja asubuhi geti linafunguliwa na gari kubwa la kuchimba kisima linaingia na gari mbili za polisi. Walianza kuchimba siku hiyo hiyo, wakasema walishafika hapo na kuangalia ni wapi maji yapo. Walishinda siku nzima hapo wakichimba kisima cha kisasa cha maji, wakisimamiwa na askari mpaka ilipofika jioni wakawa wamepata maji, siku inayofuata wakaja watu wakujengea, baada ya siku tatu Masha alihakikisha maji yanatoka mpaka ndani. Hakuna aliyekuwa akimsemesha. Walimwacha afanye kile anachotaka ili asipate sababu. Bella naye alikuwa akimwangalia tu kwa dirishani, kwani Masha hakuwa akiingia ndani kama Bella alivyomuomba ampe muda wa majuma mawili na mtoto wake.

Alijenga michezo mizuri sana, tena ya kisasa kwa ajili ya mtoto wake. Bella alikuwa akitoka hapo nje kucheza na mwanae mara kwa mara. Ric alikuwa mtoto mzuri sana, mtulivu na mwenye upendo. Bella ndiye aliyehitaji kujenga mahusiano na yeye, lakini yule mtoto alionekana kumfahamu mama yake vizuri sana, na kila alipomuona Bella amepooza akiwaza, alimsogelea na kumkumbatia. Lugha ndio walikuwa hawaelewani mwanzoni. Lakini Bella alijitahidi kumongelesha kwa vitendo, na yule mtoto hakuacha kuongea kilugha. Taratibu Ric alianza kuzoea watu wa mle ndani, ile hofu ya mlango ukifunguliwa kwa nguvu na kutetemeka kila wakati ilianza kuisha. Bella alimuhamishia chumbani kwakwe, usiku wakawa wakilala pamoja. Upendo wa kimama haukuchukua muda mrefu kwa Bella. Kila alipomtizama yule mtoto alimfananisha sana na Eric.

Bella kipenzi cha Mzee Mwasha, aliongeza upendo kwa baba huyo kama baba yake wakumzaa. Masha alipomaliza hekaheka zake kwenye hiyo nyumba, pakawa pametulia. Ucheshi wa Bella ukarudi, furaha kwake ikaongezeka kuona amepokelewa kwa garama kubwa vile, tena walikubali Masha awabadilishie nyumba yao atakavyo, ilimradi tu wawe naye mle ndani. Ilimgusa sana Bella. Alijisikia kupendwa kwa hali ya juu. Ujasiri uliongezeka, hakuna jinsi ungemwambia Bella pale sio kwao, akakubali.

 Hakuacha kuwa jikoni na Mama Mwasha kila wakati kujifunza kupika kile anachojua Mzee Mwasha anakipenda. “Hivi unajua hicho chakula unachokula baba, nimepika mimi mwenyewe? Mama alikuwa akiniangalia tu, hajasaidia chochote. Tena hata nyanya alinikatalia kunisaidia kumenya.” Mama Mwasha alicheka. “Sasa pishi moja unataka wapishi wawe wangapi, Bella mwanangu? Lazima ujue kufanya mambo yote wewe mwenyewe.” “Na umejitahidi sana mwanangu. Usingeniambia, nisingejua kama wewe ndio mpishi. Ladha ni kama ya chakula cha mama yako.” “Nimeshamzidi JJ?” Bella aliuliza na kufanya wote wacheke. “Kazana. JJ hodari sana.” Mzee Mwasha alijibu. “Sasa unajua nini baba? Nitakuwa namuomba aje apike hapa hapa, halafu nikae naye jikoni.” “Hayo ndio maneno. Zaidi jifunze kutengeneza juisi yake. Ukimudu hiyo, utakuwa umefuzu shule ya mapishi. Nabakiza kazi ya kunywa juisi kila siku asubuhi na jioni.” “Usijali baba yangu. Hiyo haitachukua muda, nitakuwa nimeshaimudu.” Amani na furaha vilitawala ndani ya nyumba hiyo. Mwasha alikuwa na furaha kila wakati. Kila alipokuwepo Bella pale nyumbani, awe nje au ndani, Mzee Mwasha alitaka awe karibu naye. Kwanza alimfanya acheke, pili hakutaka Bella awe mpweke. Bella alimpenda Mzee Mwasha na mkewe kama wazazi wake. Hakuna mtu angefika pale akajua Bella hakuzaliwa na wale wazee.

*********************************************************

Wakiwa wanacheza na mtoto wake jioni hiyo, Mzee Masha alirudi pale. Bella alimuona wakati anafunguliwa geti, akaenda kuegesha gari yake upande ambapo Bella alikuwa akicheza na mtoto, alipomuona anashuka na kuwafuata, akageuka kama hakumuona. Masha akaanza kucheka. “Hujambo Bella?” “Sitaki.” “Lazima ujifunze kuongea na mimi Bella. Hasa tukiwa mbele ya mtoto.” “Unaniudhi Masha.” “Sasa kama hapa nimekufanyaje Bella?” “Naomba niache, nicheze na mwanangu.” “Sema mtoto wetu.” Bella alinyamaza. “Majuma mawili yamepita.” “Siku zote umezitumia kufanya fujo zako kwenye nyumba ya watu. Asubuhi mpaka jioni ilikuwa kelele za mafundi wako na mapolisi. Umebadilisha nyumba ya watu bila hata woga. Fujo tu, wala sijapata muda mtulivu na mwanangu.” Masha alitingisha kichwa. “Mtoto anatakiwa aanze shule ili aanze kuchanganyikana na wenzake.” “Umepata shule sasa?” “Ndiyo. Anatakiwa aanze Jumatatu. Kila kitu nimeshalipia na nimesha mwandikisha. Hili ni jina la mwalimu wake na darasa lake. Nimewaambia haruhusiwi mtu yeyote kumchukua pale shuleni isipokuwa wewe, Mzee Mwasha na watoto wake tu.” “Asante Masha.” Masha alicheka. “Unacheka nini sasa?” “Ukitulia unakuwa mtoto mzuri kweli.” “Wewe ndio unanifanya nikuchukie Masha. Unaniudhi. Una roho ya ajabu sana, kama sio binadamu! Unajidai unanipenda huku ulikuwa unanitesa.” “Nakupenda sana Bella.” “Sasa kwa nini ulikuwa unanipiga vile?” “Nilikwambia nilikuwa nachanganywa na mambo mengi, nikakuahidi sitarudia tena kukupiga. Naomba unisamehe?” Bella alitoa macho. Wakati wote Masha amekua akiahidi kutorudia tena lakini si kuomba msamaha. “Wewe huyo, ndio unaomba msamaha leo!!?” “Mambo yamebadilika Bella. Namthamini sana huyo mtoto. Sitaki akue kwa makuzi ya ajabu, ambayo mimi na wewe hatuelewani.” “Kwa hiyo huo msamaha wako unamaanisha?” “Unafikiri nakutania? Sijawahi kuomba msamaha kwa mwanadamu yeyote yule hapa duniani, isipokuwa kwa mama yangu mzazi tu na leo kwako. Uliza watu watakwambia.” Bella alicheka sana.  “Unafikiri nakutania?” “Sasa kama kweli unamaanisha, nataka uniombe msamaha mbele ya mkeo na familia ya Mwasha ndio nitakusamehe.” Masha alitingisha kichwa.

“Hivi wewe Bella unajua wewe ni mkorofi sana?” “Kama hutaki basi. Lakini kama unataka amani na mimi mpaka uniombe msamaha vizuri tena mbele ya watu. Kila mtu anajua mimi nilikupendea pesa zako, nikaharibu ndoa yako kumbe ulikuwa unanibaka kila siku.” “Mtoto anakusikia Bella.” “Basi ondoka.” “Kesho kutwa namtaka mtoto.” “Hapana. Jumapili ni siku ya kanisani. Nyumba nzima tunaenda kanisani na tunakuwa pamoja kama familia. Kama unamtaka mtoto mchukue kesho.” “Kesho nina mambo mengi, Bella.” “Basi kama una mambo mengi ya muhimu kushinda mwanao, ndio usubiri mpaka siku utakayokuwa huna majukumu mengine. Lakini sio siku za Jumapili.” Masha alifikiria kidogo. “Utamleta?” “Wapi? Tena iwe sehemu ya wazi Masha. Sitaki tuwe sehemu peke yetu.” Masha licheka sana.

“Tena nina hamu na wewe kweli Bella.” “Najua sana. Huwezi kupata mtu aliyekuwa akikuhudumia kama mimi, halafu ndio ulininyanyasa kweli.” Bella alianza kumcheka. “Muone alivyopooza sura.” “Ukirudi sasa hivi Bella, sitakupiga hata iweje, nakuahidi Bella wangu.” “Aku!!” Bella alipandisha mabega yake kukataa. “Niache nipumzike.” “Halafu umeanza kurudia enzi zako, nywele kama mtoto wa kichotara!” Bella alicheka. “Lazima nipendeze. Hapa kwa Mzee Mwasha, napendwa na kuheshimiwa. Wananitunza kama mtoto wao. Sina hofu yakupigwa wala kusingiziwa. Kwa nini nisianze kupendeza? Nikiwa na mawazo wananifariji na kuniombea. Wakati wewe ulikuwa hujali furaha yangu hata kidogo Masha. Hata nilipojitahidi kukupenda, na kukunyenyekea,  hukunithamini. Ulinipiga utakavyo na kuniacha navuja damu. Tena naomba usinikumbushe. Umeshaleta fomu za mtoto za shule, naomba uondoke.” “Nimeahidi kubadilika Bella. Nitakujali na kukutunza vizuri.” “Akuu! Sitaki Masha, niache nipumzike. Nilikuwa nakubali unitese vile sababu ya Eric. Ndio maana nilikuwa navumilia vipigo vyote vile, ili mdogo wangu aishi kwa furaha. Nilikubali uusulubishe mwili wangu utakavyo, kwa ajili ya marehemu mdogo wangu. Sasa hivi sina hata sababu tena. Acha nipumzishe mwili wangu Masha. Baada ya kujua amefariki Eric, yale maumivu yote uliyokuwa ukinisabishia, mchana na usiku, ya vipigo vyako, matusi na masimango, huwezi amini Masha, vilirudi upyaa. Sikuwa najua kama nilikuwa nikiumia kwa kiasi kile mpaka nilipoonyeshwa kaburi la mdogo wangu. Sikutanii Masha, muulize Mama Mwasha. Mwili wote ulianza kuuma kama ndio umetoka kunipiga. Nilikuwa nasikia maumivu makali sana kwenye ule mshono wa upasuaji, kama ndio nimetoka chumba cha upasuaji. Tumbo lilikuwa likiniiuma, kama ndio umetoka kunipiga yale mateke uliyokuwa ukinipiga tumboni. Mdomo ulikuwa unajaa mate yenye ladha ya damu, kana kwamba ndio umetoka kunipiga vibao vya usoni na kuchana midomo yangu, kila nikitema mate nikijua natoa damu kinywani mwangu, damu ilikuwa haitoki, kumbe mawazo. Nilimshangaa Mungu vile alivyoweza kuyaficha maumivu yangu wakati ule na kunirudishia kipindi hiki kunionyesha uthamani wa uhuru alionipa. Bado naugulia maumivu ya mateso yako Masha, acha nipumzike. Ulinitesa sana Masha, tena bila sababu. Niliamua kutulia na wewe tu, lakini pia hukuthamini mapenzi yangu kwako. Nilikuwa nikikuridhisha kwa kila hali, bila kujijali mimi mwenyewe. Acha safari hii iwe zamu ya Enabella. Nikipata mwanaume ninayempenda, nakuletea mwanao ukae naye na mimi nifurahie maisha kama wanandoa wengine.” Masha alikuwa amenyamaza kimya akimsikiliza, huku akiumia moyoni. Alizidi kuumia na kuamini mateso anayosimulia Bella. Hakutegemea kumuona Bella yupo tayari kumuachia mtoto hasa baada ya vile vitisho vyakumnyang’anya mtoto. Alijua vingemuogopesha hata asifikirie swala la mwanaume mwingine lakini alishangaa utayari wake wakupoteza hata mtoto ilimradi awe mbali na yeye.

Yaani upo tayari kumuacha mtoto kwa ajili ya mwanaume mwingine!?” “Hee! Kwani si atakuwa kwa baba yake? Kuna ubaya gani mtoto akiishi kwa baba yake? Tena ndio vizuri atakuwa amepata mapenzi yetu wote wawili. Sio hivyo unavyotaka uwe unamchukua masaa mawili halafu umrudishe. Hujui akichukia yukoje au akiwa na tatizo fulani anafananaje. Sasa nitakuachia moja kwa moja na wewe umlee mtoto, na mimi niwe huru.” “Dereva atakuja kukuchukua kesho ukanunue nguo zako na mtoto.” “Simtaki yule dereva wako.” “Basi utaletewa gari.” “Sitaki.” “Unataka nini Bella? Gari yako utaletewa Jumapili.” “Tulishapanga na mama kwenda kesho madukani kutafuta nguo za mtoto.” Masha aliweka yale makaratasi kwenye bembea, na bahasha yenye pesa, akaondoka na kumuacha Bella akiendelea kucheza na mwanae.


“Bella aanza maisha mapya akiwa na mwanae.”
Aliamka Jumatatu asubuhi na mapema, akamwandaa mtoto wake, na kuandaa kifungua kinywa cha nyumba nzima, alipohakikisha mwanae ameshiba, alienda kugonga chumbani kwa Mama Mwasha. “Mbona mapema? Halafu umependeza sana Bella. Wewe na mwanao wote mmependeza.” “Asante mama. Nataka niwahi nikafahamiane na mwalimu wake Ric, ndipo niende kazini. Nimeshaandaa kifungua kinywa kipo mezani. Au niwaletee huku?” “Hapana Bella mwanangu. Asante.” “Naomba nimsalimie baba ndio niondoke.” “Ingia tu, yupo macho.” Bella aliingia akamchekesha kidogo Mzee Mwasha akambusu. “Nitakuletea zawadi baba yangu.” “Nitakuwa naisubiria kwa hamu.” “Utakuja kazini?” “Mkinihitaji nitakuja.” “Basi wewe pumzika, ngoja mimi nikamsaidie Elvin.” Waliagana, Bella akatoka. Alikuwa amenunuliwa gari nzuri sana, tena ya kifahari. Ilikuwa kubwa ya rangi ya maruni. Bella alikuwa amependeza kweli kweli. Wakati wote alijijulia mwili wake. Alijua kujitengeneza na ukichanganya na uzuri Mungu aliomjalia, alizi kupendeza. Aliondoka mapema, lakini aliacha ameshasafisha nyumba yote.

 Alifika shuleni kwa mtoto wake, akaongea kwa kirefu na mwalimu wa darasa la mtoto wake, wakamuahidi kuwa karibu naye sana. “Tafadhali, ukiona tu hana furaha, naomba unipigie simu nitakuja kukaa naye kidogo ili azoee. Ni mpole sana na ni muoga. Naomba msitumie sauti ya juu sana kuongea naye.” “Hata baba yake alituambia walimu wote ile siku alipokuja.” Bella alishtuka. “Kwani aliitisha kikao?” “Aliomba kuzungumza na walimu watakao mfundisha Ric.” “Yaani Masha!” “Lakini ni sawa tu. Na sisi tunafurahia wazazi wanao shirikiana na sisi kwenye malezi.” “Sasa huyo, mtamchoka!” Yule mwalimu alicheka. “Naamini Ric atakuwa na wakati mzuri.” Bella alimbusu mwanae akaondoka.

“Siku ya kwanza ya Bella kazini.”
Alikuta sura nyingi ni ngeni. Hata sekretari wa Elvin alibadilishwa. “Ngoja nimwambie bosi kama upo hapa.” “Sawa.” Yule dada alipiga simu kwa Elvin, baada ya muda mfupi Elvin akatoka. Alisimama akiwa amemkodolea macho Bella. “Siamini kama ni wewe!” “Lazima uwe umenisahau. Siku zote hizo! Ulijificha wapi?” “Mambo mengi. Karibu ndani. Nimeshakuandalia na ofisi yako.” Bella alicheka akaingia ofisini kwa Elvin. “Mbona hata nywele hujachana vizuri? Umechoka kama hujalala! Unaumwa?” “Mimi mzima kabisa. Vipi Ric?” “Ameanza shule leo. Ameanza kuelewa Kiswahili kidogo, nimefurahi tumeanza kuzoeana. Mbona ulikuwa huji nyumbani?” Bella alihoji. “Si ulisema unataka muda na mtoto wako?” “Nilikuwa nikimwambia Masha tu, sio na wewe Elvin jamani!” “Sasa kwa nini ulipoona kimya usinitafute?” “Elvin jamani! Mkeo hanifahamu, wala simfahamu ni mtu wa namna gani. Nilihofia nisije nikakupigia halafu nikazua matatizo bure.” Wala Elvin hakukanusha. Alibaki kimya. “Unaonekana umechoka sana Vin, halafu kama hujala. Nipe kazi zinazokukabili sasa hivi, mimi nizifanye halafu urudi nyumbani ukalale kidogo. Tena ukienda nyumbani, utakuta kifungua kinywa kizuri. Niliandaa kabla sijaondoka.” “Utakuwa umenisaidia sana. Nina usingizi karibu nachanganyikiwa.” Elvin alimuachia Bella majukumu yake, akarudi nyumbani kwao.

Alimkuta mama yake na baba yake mezani wakila. Alisalimia akavuta kiti akakaa. Mama yake aliona jinsi hali yake ilivyo, kwa kuwa alijua maswala yake ya ndoa, hakutaka kumuuliza. Alikaa pale akionyesha mwingi wa mawazo. Akala kimya kimya, akanyanyuka. “Naenda kulala kidogo. Nikiamka nitarudi kazini, nimemuachia ofisi Bella, naamini kila kitu kitaenda sawa.” “Wewe pumzika tu, kama kuna tatizo, atanipigia mimi.” “Asante.” Elvin alivuta kiti chake nyuma, akasimama kuelekea chumbani kwake. Alijitupa kitandani na viatu vyake, akapitiwa na usingizi.

Alilala kuanzia asubuhi ile mpaka saa nane na nusu mchana. Alikurupuka na kutoka pale. “Naomba uchane nywele kabla hujarudi kazini, Elvin.” Mama yake alimuwahi kabla hajatoka mlangoni. “Au uoge kabisa.” Baba yake aliongeza. Elvin alirudi ndani, akaoga na kubadili nguo akatoka. “Angalau sasa hivi unapendeza.” Elvin alimsogelea mama yake akambusu kichwani. “Baadaye.” Aliaga. “Chakula?” “Nimechelewa mama. Nitakuwa sawa.” Elvin akaondoka.

Alimkuta Bella amepunguza sehemu kubwa sana ya kazi. Alimzungusha kila ofisi kumtambulisha kwa wafanyakazi wageni, walio mfahamu walifurahi kumuona tena Bella, wakampa pole ya matatizo na kumkaribisha tena pale ofisini.

*********************************************************

Bella aliendelea na kuchapa kazi na majukumu ya mwanae ya kila siku. Aligundua Elvin ana matatizo sana nyumbani kwake. Kwa kuwa hakutaka kumwambia, na yeye Bella hakutaka kuuliza, kitu alichokifanya Bella ni kuhakikisha anatengeneza kitafunio cha kutosha kila siku usiku kabla ya kulala, au asubuhi kabla hajamuamsha mtoto wake, na kumbembea Elvin. Alihakikisha Elvin anapata mlo wa asubuhi na mchana kila siku. Na jioni kabla hawajaachana, alikuwa akimtengenezea matunda mengi, anamwachia mezani kwake, ndipo Bella alikuwa akiondoka kwenda kumchukua mtoto wake shuleni. Alipozidiwa na kazi, Mama Mwasha ndio alienda kumfuta Ric shuleni.
Furaha ya Elvin ilianza kurejea. Na afya yake ikaanza kurudi. Kama kawaida yao, walijikuta wanaanza kufuatana tena pale kazini. Kula pamoja kuanzia chakula cha asubuhi mpaka jioni wakiachana. Kama wakitamani chakula cha hoteli fulani, walikiagiza kiletwe pale pale ofisini kuepusha kuonekana tena pamoja. Maneno ya Mzee Masha yaliwaingia vizuri sana. Wakaongeza umakini katika kila jambo wanalofanya pamoja. Hawakutaka kuonekana tena wanazurula pamoja wakiwa peke yao. Katika yote hayo, Bella alionyesha anamuheshimu na kumkubali sana Elvin vile alivyo akiwa ameoa. Hakumuhukumu tena kwa kuoa kwake, akabaki akimfariji vile alivyoweza, kitu kilichoongeza faraja kubwa sana kwa Elvin. Kila alipomuona amekuja kazini bila furaha, alianza kumchokoza mpaka acheke, na kubadilisha ile hali yake. Aliahakikisha kila wanapoachana, Elvin anakuwa yupo na furaha. Kazi za pale ofisini zikaanza kwenda kwa haraka, ripoti aliyokuwa akimwandalia baba yake kila mwezi, ilianza kukamilika kwa wakati, kwani Bella alikuwepo pale kusaidia kila idara.
Taratibu Ric naye lugha ikaanza kuchanganya, akapata rafiki pale shuleni aliyekuwa akimuongelesha sana na kumfanya Ric kuanza kuongea. Kama kawaida yake, Mzee Masha hakuacha kupita pale shuleni kumwangalia mwanae. Siku za Jumamosi, Bella alikuwa kimpeleka kwa baba yake mida ya jioni, halafu usiku Mzee Masha alikuwa akimrudisha. Ric alibadilika akawa mtoto mwenye furaha, uzuri na ukarimu kama mama yake. Masha alimtambulisha yule mtoto kwa kila mtu, mpaka kwa mkewe na watoto wake. Mapenzi yote ya Masha yalihamia kwa Ric. Na kwa kuwa bado hakuwa na maelewano mazuri na familia yake, wakati wote Masha alisema Ric ndiye atakayemzika. Ric alizaliwa wakati Mzee Masha alikuwa na umri wa miaka 50 tayari.

*********************************************************

Kila mtu aliona mabadiliko ya Elvin. Gafla alinawili vizuri na furaha ilirudi usoni. Alijitahidi kuendelea kumpeleka mtoto wake nyumbani kwao kila siku za Jumamosi pale alipoweza au kuruhusiwa na mkewe. Walishinda na Bella, siku hiyo kuanzia asubuhi mpaka usiku, huku watoto wao wakicheza pamoja, mpaka muda wa Ric kwenda kwa baba yake ulipokuwa ukifika, ilimbidi Bella ampeleke, kisha anarudi tena kukaa na Elvin wakati akisubiri Ric arudishwe usiku. Taratibu Bella akaanza kumzoea na mtoto wa Elvin, Oli kama walivyozoea kumwita kwa kifupi cha Olivia. Muda ambao Ric anakuwa kwa baba yake, Bella aliutumia vizuri kuwa na Oli. Hakuwa mtoto mwenye tabia mbaya. Mtaratibu sana, kwani alizaliwa na wazazi wote wenye asili ya ukimya. Alifuata rangi ya wazazi wake, lakini kwa kuwa alikuwa mtoto, alikuwa na weusi mzuri sana. Yule mtoto alionekana kumpenda sana Bella. Kama kawaida ya Bella, hakuacha kumtekenya na kumfanya acheke, kitu ambacho hata baba yake hakuwa akijua kama yule mtoto ni mchekaji vile. Kila alipokuwa akimuona Bella, alijisogeza kimya kimya ili Bella amtekenye, na wote walikuwa wakijua hilo. Ilikuwa mtoto wa Elvin akianza kucheka hata kama una hasira, lazima na wewe utacheka tu. Alikuwa akicheka mpaka anatokwa na machozi. Ulikuwa ni wakati mzuri sana ambao Elvin alikuwa akiusuburi kwa juma nzima, kumleta mwanae kwenye mazingira hayo matulivu na yenye amani.

Jumapili Elvin hakuwa akionana na wazazi wake, kwani kutokana na maneno mengi yaliyokuwa yakiendelea kanisani kwao, Mwasha na mkewe walihama kanisa na kumuacha Elvin na mkewe kwenye lile kanisa. Kwa hiyo siku za jumapili Mzee Mwasha, mkewe, Bella, Ric, Eli na familia ya JJ, bila Diva, walienda kanisa jingine pamoja, na kila walipomaliza ibada, walikuwa wakikutana kwa chakula cha mchana pamoja. Mwanzoni Elvin alikuwa akija na yeye, lakini gafla waliona haonekaniki tena siku za jumapili nyumbani kwao. Hakuna aliyetaka kumuuliza kwani walijua kutokuelewana kwao na mkewe ndiko kunako changia. Mama Mwasha alijitahidi kwa kadiri ya uwezo wake, kutafuta amani na Happiness mke wa Elvin lakini ilishindikana.
“Naomba umwambie Happiness kesho nawakaribisha nyumbani kwa chakula cha mchana.” Mama Mwasha alimsogelea Elvin wakati akimvalisha mwanae viatu ili waondoke siku hiyo ya jumamosi. Elvin hakujibu, akanyamaza kimya. Bella aliona kila kitu, lakini hakutaka kuchangia neno kwa wakati ule.

Elvin alipoondoka, Bella akamfuata Mama Mwasha chumbani. “Vipi Bella?” “Kuna kitu kinanisumbua mama. Sijui ni sawa nikikuuliza?” “Wewe niulize chochote.” “Mbona tokea nirudi hapa, sijawahi kumuona mke wa Vin akija hapa nyumbani? Kuna tatizo lolote? Nahofia nisije kuwa mimi nasababisha tena kama alivyokuwa akisema Irene.” Bella alikuwa amekaa kwenye kitanda, pembeni ya Mama Mwasha. “Hapana Bella mwanangu. Mimi ndiye mbaya wa huyo mkewe.” Bella alikunja uso. “Wewe!?” “Ndiyo.” Bella alimjua Mama Mwasha jinsi alivyo, hakuwahi kumsikia wala kuona anaadui kwa muda wote aliomfahamu yule mama. Na alipenda sana amani. “Kwani kulitokea nini mama?” “Mmmh! Ni mengi.” Mama Mwasha alimueleza kuanzia mwanzo wa mahusino ya Elvin na Happiness mpaka ndoa yao, na Happiness alipoishi pale na wao, akaondoka na mpaka siku ya mwisho Mama Mwasha anaondoka nyumbani kwao wakati alipozaliwa Oli. Bella alianza kulia. “Pole mama yangu. Ndio maana Vin wangu anakuwa hana furaha! Vin hawezi maneno mengi, atakuwa halali vizuri.” “Kinachoniuma, ni vile asivyomjali mwanangu. Sijawahi kumwambia kabisa Elvin, lakini Happiness hamjali kabisa. Hajali kula yake wala furaha yake.” “Anataka nini sasa? Mbona Mungu amemjalia mwanaume mzuri hivyo?” “Sijui Bella. Mi mpaka wakati mwingine naona naingia dhambini nasema labda alimpendea pesa zake tu. Sasa, sasa hivi ananufaika nazo haoni tena umuhimu wake.” “Jamani Vin wangu! Mungu amtete. Ni mpole sana Elvin, na hajui kulalamika kabisa. Atakuwa anateseka tu ndani kwa ndani.” “Ndio hivyo. Lakini Bella, kama Mungu yupo, na kama huyo Elvin ni mwanangu basi Mungu atamtetea. Maana ni kweli sijawahi kumfanyia Happiness ubaya wowote ule isipokuwa nilimpenda bila unafiki. Unajua hata kanisani tulihama kwa ajili ya maneno yake?” “Mama!” “Kweli tena. Amewageuza watu akili, kila mtu akawa ananiona mimi mbaya. Ndio Mwasha akasema ni heri tuhame, nisije kutibua magonjwa ya moyo bure. Mjukuu mwenyewe ndio namuona akitaka yeye. Wakati mwingine Elvin anaweza kukwambia tunakuja, mara unashangaa mpaka siku inaisha hawajaja. Najua tu ni yeye, kwa kuwa Elvin wakati wote hawezi kuvunja ahadi yake. Najua labda ni yeye ndiye anayemzuia. Lakini Mungu yupo Bella, wala usilie. Yote haya yana mwisho.” “Kweli mama. Nasema labda nisingepotea mambo yasingekuwa hivi. Elvin alisema angenioa mimi.” Bella alizidi kulia. “Pole Bella.” “Ungekuta sasa hivi mimi ndio ningekuwa mke wa Vin. Roho inaniuma kweli.” “Na alikulilia Elvin jamani! Mpaka tulihisi angerukwa na akili. Ndio maana nilimshawishi sana aoe. Japokuwa Eli ananilaumu sana, lakini nia yangu ilikuwa nzuri Bella. Elvin alikuwa na wakati mgumu sana wa maisha. Na yule binti alikuwa akija mpaka hapa nyumbani akiniapia anampenda Elvin, tena mpaka kwa machozi. Nikaona upendo mkubwa vile, ndio ungemstahili Elvin kwa wakati ule. Nilimshawishi Elvin kwa muda mrefu sana, tena mpaka wakati mwingine nilimtishia ili tu amuoe yule binti. Nikajua wakiingia kwenye ndoa, atapata faraja. Kumbe ndio nilikuwa namwingiza motoni. Najuta Bella. Huwa nakaa humu ndani nalia, nakutubu nikimsihi Mungu amsaidie.” “Pole mama. Nia yako ilikuwa nzuri, wala usijilaumu. Sasa hivi Elvin anatuhitaji sana. Mimi najitahidi kumtia moyo sana kwenye ndoa yake, sitaki aishi kule bila furaha.” “Humjui Happiness, Bella mwanangu. Habebeki.” Mama Mwasha alimueleza Bella visa vya Happiness kwa kurudia rudia huku akijilaumu sana.


Mabadiliko ya Elvin yazua ugomvi.
Elvin alirudi nyumbani, lakini alipofika mtoto alikuwa amelala kwenye gari. Alimshusha taratibu ili asiamke, akambeba mpaka ndani. Alikuta watu wote wamelala kasoro Happiness alikuwa akimsubiri sebleni. “Habari za kushinda?” Elvin alisalimia mara tu alipoingia. “Namuomba mtoto wangu.” Elvin akiwa na mshangao alimsogelea Happiness na kutaka kumpa mtoto. “Lakini amelala, kwa nini nisiende kumbadilisha nguo, nikamlaza moja kwa moja?” “Hilo umeligundua saa ngapi?” “Ni nini tena Happness?” “Wewe umekaa na mtoto kwa huyo mwanamke wako mpaka saa hizi usiku, ulitegemea nini?” “Nilikuwa nyumbani Happy, tafadhali naomba tusianze malumbano saa hizi usiku.” “Unanifanya mimi mtoto mdogo sana, eeh? Unafikiri sikuoni jinsi ulivyobadilika. Siku hizi nikiongea, unajifanya kama husikii. Kutwa upo kazini, unatoka hapa asubuhi na mapema unajifanya unaenda kazini kumbe unamfuata Bella huko kazini. Unafikiri utanificha kuwa Bella amerudi mpaka lini? Taarifa zenu zote ninazo. Mnakula pamoja na kila kitu mnafanya pamoja. Nasikia haondoki jioni mpaka uwe umekula. Ameambiwa na mama yako kuwa sijui kupika?” “Naomba usimwingize mama yangu katika hili Happy. Tafadhali sana.” “Ataacha kuingizwa vipi wakati yeye ndio anakutafutia wanawake wengine wakati anajua una ndoa takatifu?” Elvin alipandwa na hasira sana, akaamua aondoke tu akamlaze mtoto. Happy alimfuata nyuma na maneno.

Tena nasikia amemuhamishia huyo Bella hapo hapo nyumbani kwenu. Ili mpate kuonana vizuri. Yaani siku zote unaondoka hapa na mwanangu, ukisema unaenda kusalimia wazazi wako, kumbe unaenda kukutana na mwanamke wako nyumbani kwenu! Unampeleka mwanangu kwa hawara yako! Tena wazazi wako wanajifanya wacha Mungu, huku wanakuruhusu uwe na wanawake wawili huku na huku. Wamejawa unafiki na kila mtu amewashtukia pale kanisani ndio maana kanisa limewashinda wamehamia kwengine. Na huko pia watawajua tu hila  zao.” “Happiness, tafadhali acha kuwasema vibaya wazazi wangu. Tafadhali sana. Sijawahi kuwavunjia wazazi wako heshima hata mara moja. Naomba kama umeshindwa kuwa karibu nao, tafadhali usiwaseme vibaya. Inaniuma sana.” “Kumbe wanavyonifanyia mimi ndio unaona ni sawa?” Elvin alimaliza kumbadilisha mtoto wake akamuweka kwenye kitanda chake huku Happiness akiendelea kuongea tena kwa sauti.

Na kuanzia leo, marufuku kukuona unaondoka hapa na mwanangu. Huyo Bella na yeye si mwanamke? Basi zaa naye  na yeye mtoto wa kike. Mtoto wangu sio wa maonyesho. Usithubutu kumrudisha mwanangu huko kwenu. Unanisikia wewe Elvin?” Elvin hakutaka kujibu, alianza kuvua nguo zake ili apande kitandani alale. “Na huwezi kulala hapo hivyo ulivyo mpaka ukaoge. Unataka kuniletea jasho lako ulilotoka kulala na mwanamke wako!? Hata siku moja.” Elvin alicheka akatingisha kichwa akapanda kitandani na kujifunika shuka.  

Happy alilivuta shuka na kung’oa chandarua. “Happiness unatafuta matatizo wewe! Kwa nini unanifanyia hivyo?” “Sitaki uchafu?” “Umeanza lini huo usafi? Ona hii nyumba ilivyo chafu. Meza ya chakula tu kufuta ni shida, inavyakula vya kuanzia asubuhi, nzi wamejaa humu ndani, maji kila mahali. Ona shuka lenyewe lilivyo chafu! Sasa usafi upi unaozungumzia Happiness?” Happiness alianza kulia kwa sauti mpaka mtoto akaamka na kuanza kulia. Elvin alitaka kwenda kumchukua mtoto, lakini Happiness alimsukuma. “Usimshike mtoto wangu.” “Sasa hapo unavyolia kwa sauti, kinachokuliza ni nini?” “Umenitukana mimi na ndugu zangu. Unasema sisi ni wachafu.” Watu wote waliamka. Happy alikuwa akilia kwa sauti sana huku akiongea. Elvin alikaa pembeni ya kitanda akimwangalia.

Majirani walishazoea ugomvi kwenye nyumba yao, kwa hiyo hakuna aliyekuwa akienda kuwagongea tena kama zamani. Hata mlinzi wao alishawajua. Kwa kuwa Happiness alikuwa akiongea sana, basi kila mtu alikuwa akiwasikiliza kila wakianza kugombana.

“Tangia Bella amerudi umebadilika sana. Nampigia simu Mchungaji nimwambie umeanza kutoka nje ya ndoa na huna heshima na mimi kabisa.” Happiness alimpigia simu Mchungaji wao, yeye akiwa analia na mtoto wake akiwa analia. Aliongea kwa muda mrefu sana. “Yaani sasa hivi ndio anarudi nyumbani, na chakusikitisha wazazi wake wanajua hilo lakini hawamkatazi. Wanaishi na huyo mwanamke hapo hapo nyumbani kwao. Wanaishi kama mke na mume huko kazini. Muulize hata Paulina anafanya nao kazi huko ofisini, atakusimulia. Ananidhalilisha sana Elvin. Nimejitahidi kumpenda kwa kadiri ya uwezo wangu lakini anatukana mpaka wazazi wangu. Anasema kwetu ni wachafu, tena mama akiwepo humu humu ndani.” Happiness aliendelea kulia na mtoto wake akilia. Elvin alibaki anamwangalia mkewe. Alisimama, akavaa nguo zake, akatoka pale ndani.

Alikwenda akachukua chumba hotelini, akaingia kwenye hicho chumba. Alikuwa kwenye mshtuko mkubwa sana. Alibaki akiwaza mpaka palipo pambazuka ndipo alipopitiwa na usingizi. Alilala mpaka ilipofika jioni ilikuwa siku ya Jumapili. Alikuwa amezima simu yake. Alienda kuoga, akaenda sehemu ya kula. Aliposhiba ndipo aliporudi nyumbani kwake. Alikuta wazee wakanisa na wachungaji wakimsubiri, pamoja na mkewe na wazazi wa Happiness. Walimuomba akae. Kesi ikaanza. Alishukuru Mungu kwani hata wao walijionea jinsi Happiness alivyokuwa akiongea na kubadili maneno hapo hapo kwenye kikao na kushindwa kumpa nafasi hata mmoja wao. Aliongea yeye peke yake, kuanzia mwanzo wa kikao mpaka mwisho. Alikuwa akilalamika huku akilia.

Elvin kwa kuwa alimjua, alijiegemeza kwenye kochi akabaki ameangalia dari huku amefunga macho. “Mmemuona anavyonidharau? Kwa kuwa ananiona sijasoma kama Bella. Anaondoka hapa asubuhi anajidai anaenda kazini kumbe ni sehemu yao yakukutania.” Hapakupikwa siku hiyo, walibaki wakimsikiliza Happiness. Nyumba ilikuwa chafu, nzi walikuwa wengi utafikiri wao inzi, ndio walikuwa wenyeji pale ndani. Wageni hawakuwa wamepewa kitu chochote tangia wafike pale. Mwishowe hata wao walishindwa kukaa pale ndani. Ilibidi waage. Hapakuwa pakitamanisha kukaa hata kidogo. Nyumba ilikuwa nzuri, lakini chafu kupita kiasi. Mama Mchungaji aliomba wafunge kwa maombi wandoke, hata hivyo mtoto alianza kulia. Alikuwa mchafu na yeye, hatizamiki. Hakuna aliweza kumuhoji Elvin hata swali. Hata wao waliwashangaa wanawezaje kuishi kwenye nyumba kama ile, tena na mama yake Happiness akiwepo humo humo akiishi nao.

********************************************************

Ndoa ya Elvin haikuwahi kuwa na amani hata kidogo. Na kwa kuwa mkewe hakuwa akiambilika, hata Mama Mchungaji alishindwa kumshauri yeye na mama yake kabisa. Elvin aliendelea kwenda kwao bila mtoto na kila alipofika kwao alianza kwa kulala kwanza ndipo alipoweza kutoka na kuongea na watu. Bella ndio alikuwa kama kimbilio lake. Alipenda kila alipofika nyumbani kwao, Bella awe karibu yake, na yeye ndio amuhudumie hata kama ni maji ya kunywa apewe na Bella. Ikitokea akifika kwao asipomkuta Bella, hata kula wala kunywa mpaka Bella arudi nyumbani. Na alichukia sana kila alipomkosa Bella nyumbani. Wakati mwingine alifika bila taarifa, lakini alitaka amkute Bella pale nyumbani. Wazazi wao walikuwa wakiwaangalia bila kuwaingilia kwa lolote.

******************************************************

Ric atengeneza rafiki shuleni.
Baada ya muda, Ric alipata rafiki aliyekuwa akimtaja sana nyumbani kwao. Kila mtu alipomuuliza Ric maswali, alimtaja huyo rafiki yake. Mwishowe Mzee Masha alimuomba Bella afuatilie wazazi wa huyo mtoto, ili wafahamiane zaidi. Siku hiyo ya jumatatu Bella wakati anamshusha Ric shuleni alimuomba mwalimu wake kumuona Toby ambaye ndiye rafiki wa Ric. Aliongea naye kidogo, akaomba namba ya simu ya wazazi wake. Alipofika ofisini na kuweka mambo sawa akaamua kupiga ile simu. Alitegemea Mama yake Toby ndio apokee, lakini ilikuwa sauti ya kiume upande wa pili. “Samahani kwa usumbufu. Nilitaka kuongea na wazazi wa Toby.” “Kuna nini? Toby yuko salama?” “Usiwe na wasiwasi, mimi ni mama yake Ric, nilitaka tufahamiane zaidi ili kuendeleza urafiki kati ya Ric na Toby. Ric hana marafiki kabisa, lakini anaonekana amempenda sana Toby ndiye anayemtaja kila wakati.” “Oooh! Hamna shida. Naweza kukupigia baadaye, naingia kwenye kikao kidogo?” “Sawa, asante.” Bella alijibu na kukata simu. Alikaa mpaka jioni alipokwenda kumchukua mtoto wake bila kumsikia tena huyo mzazi wa Toby. Alijisikia vibaya sana. Aliona amedharaulika, alijuta hata kwa nini alipiga ile simu.

Alifika mpaka darasani kwa Ric, Ric alifurahi sana kumuona mama yake. Alimkimbilia, Bella akabemba. Walibaki pale wakizungumza kidogo, mwishowe akamuaga mwalimu akatoka pale darasani kurudi kwenye gari lake, ili warudi nyumbani. Wakati wakitembea kuelekea kwenye gari, Bella alisikia mtu akisema “Samahani! Samahani!” Bella aligeuka. “Toby!” Ric alifurahi sana kumuona tena Toby, kana kwamba hawajaonana muda mrefu wakati walikuwa pamoja darasani muda mfupi uliopita. “Naitwa Lewis, ni baba yake Toby.” Bella alivua miwani yake ya jua akabaki akimwangalia. “Samahani sana, nilitingwa na kazi nyingi ofisini ndio maana nilishindwa kukupigia.” “Sawa.” Bella alijibu na kutaka kuondoka. “Hata Toby anampenda sana Ric. Haishi kumtaja. Ni hivi tu nimekuwa na mambo mengi, lakini na mimi ningewatafuta tu.” Bella alikuwa amekasirika kidogo, alibaki kimya akimsikiliza. “Unafikiri kesho ni siku nzuri, wanaweza kucheza pamoja? Ninakuwa nakwenda kazini nusu siku, tunaweza kuwatafuta baada ya hapo.” Lewis aliendelea kuongea. “Au unaweza kumleta asubuhi wakati wewe unaenda kazini, wao wakacheza, ukitoka kazini unaweza kuja kumchukua Toby.” “Itakuwa ni asubuhi sana, haitakuwa usumbufu kwenu? Maana wakati mwingine namuacha hata hajaoga au hajala bado.” Lewis aliongeza. “Kwetu kuna maji pia na huwa tunakula.” Lewis alicheka. “Kwa hiyo nimlete akiwa bado amevaa nguo za kulalia?” “Na za kubadili.” Bella alijibu na kumfanya Lewis acheke tena lakini yeye hakuonyesha kutabasamu hata kidogo. “Asante. Ulisema unaitwa nani tena?” Bella alifikiria kidogo. “Tutaonana kesho.” Bella alivaa miwani yake na kuelekea kwenye gari yake.

Lewis alimkimbilia tena. “Samahani. Sio kwamba nilidharau simu yako asubuhi. Pale ulipopiga, nilikuwa nimesimamiwa na mabosi zangu na walikuwa wakinisubiria tuanze kikao.” Bella alimfunga mtoto wake kwenye kiti chake vizuri, akamgeukia Lewis. “Naitwa Enabella. Lakini wengi wamezoea kuniita Bella.” “Asante Bella.” “Tutaonana kesho.” Bella alijua wazi Lewis ni msomi na ana pesa. Kwani ile shule ilikuwa ni ya gharama sana. Watoto wa vigogo tu ndio walisoma pale, watu wenye kipato cha kawaida wasingethubutu hata kusogeza watoto wao karibu ya ile shule. Kila kitu pale ilikuwa pesa. Alikuwa kijana mrefu aliyenyooka na  alikolea rangi ya weusi. Nadhifu na hata harufu ya manukato yake, Bella mpenda pafyumu alijua ni ya gharama. Waliagana na kurudi nyumbani.

Siku nyingi za jumamosi Bella alikuwa akiwa mama wa nyumbani kwelikweli. Alikuwa akiamka asubuhi namapema na kusaidia kazi za mle ndani kabla ya mtoto wake hajaamka. Mama Mwasha alikuwa msafi sana. Kwa hiyo Bella alihakikisha siku hizo za jumamosi kila Mama Mwasha alipoamka alikuta nyumba yake safi na kifungua kinywa kipo mezani. Aliamshwa na simu ya Lewis. “Pole najua nimekuamsha. Lakini ninataka kukutaarifu kuwa nipo njiani nakuja  na mtoto. Tena amelala. Nimechelewa kidogo, kama unaweza kusogea mpaka hapa barabarani ili kumchukua, ningeshukuru zaidi.” “Hamna shida. Baada ya muda mfupi nitakuwa nimefika.” Bella alivaa harakaharaka na kuingia ndani ya gari yake na kwenda barabarani. Alipofika tu, na Lewis naye alifika.  “Asante sana. Nitawaona baadaye. Kama kwenye saa saba nitakuwa nimeshatoka kazini. Uniombee radhi kwa baba yake Ric, najua nimewaamsha.” “Usijali.” Bella alimpokea Toby, akamuweka kwenye kiti cha Ric ndani ya gari yake, akamfunga mkanda vizuri, akiwa bado amelala wakaondoka. Walirudi nyumbani kwao, akamlaza. Wote wawili, Ric na Toby, walilala mpaka saa nne.

Bella alifurahi kwani waliamka akiwa amemaliza kazi zake zote. Ric na Toby walifurahi sana kuamka na kujikuta pamoja. Wote walipoamka walikataa kuoga kwanza, kwa kuzidiwa na michezo. Bella alifanikiwa kuwawekea chakula mezani wakala na kuwalazimisha kuoga. Walipooga tu aliwatoa nje kucheza. Walicheza mpaka Lewis alipokuja pale. “Pole sana. Hawajakusumbua?” “Hata kidogo. Naona kweli hawa ni marafiki.” Lewis alicheka. “Sasa kabla sijakaa na kukupokea ulezi, naomba niingie ndani nikasalimie.” Lewis aliwabeba watoto wote akaingia nao ndani.
Alimkuta Mzee Mwasha na mkewe, pamoja na Eli. “Huyu ni baba yake Toby.” “Karibu baba.” Mzee Mwasha alimkaribisha. “Hawa ndio wazazi wangu Lewis. Na huyu anaitwa Eli, anko wa Ric.” Eli alimpa mkono. “Karibu sana Mkubwa.” Eli alimkaribisha. Lewis alionekana kaka muungwana na alikuwa na heshima zake zote. Alikaa pale ndani akaongea kidogo, mwishowe aliomba atoke akacheze na watoto. “Nakuwa na kazi nyingi sana, nakosa kabisa muda na Toby. Ndio maana najitahidi siku za jumamosi na jumapili niwe naye karibu.” “Hamna shida baba. Nyinyi kachezeni tu. Chakula kitakapokuwa tayari tutawaita.” Bella, Lewis na watoto walitoka nje.

Lewis alikuwa akimwangalia Bella kwa kujiiba sana na Bella alijua. Bella naye alikuwa akimshangaa jinsi anavyokimbizana na watoto. Alikuwa akicheka sana. “Unakuwa kama mtoto, Lewis!” “Huoni wanavyocheka? Wananiona mtoto mwenzao.” Watoto walikuwa wakimkimbiza Lewis na walipokuwa wakimkamata aliwabeba na kugaragara nao chini huku akiwatekenya. Vilijaa vicheko kwa watoto hao, Bella hakuchoka kuwa nao. “Sasa itabidi jumamosi inayofuata nije niwachukue mje kwetu.” “Unataka tulipize?” “Hamna bwana. Sasa mlitaka mje kwetu lini? Kwanza sijamuona baba yake Ric. Amesafiri nini?” Bella alitulia kidogo. “Haishi hapa. Hapa naishi na wazazi wangu tu.” “Ooh! Sawa kabisa. Naamini siku moja nitamfahamu.” Bella hakujibu kitu. Walipata muda mzuri wa pamoja mpaka giza lilianza kuingia. Lewis aliaga akaondoka na mwanae. Ric alikuwa amechoka sana. Bella alimuogesha, lakini alishindwa kula kabisa. “Mpe tu maziwa akalale huyo. Amechoka sana leo, hawezi kula tena.” Mama Mwasha alimkuta Bella na mwanae wakilishana pale mezani. “Sidhani hata kama anaweza kuyanywa hayo maziwa. Kione kinavyosinzia.” Wote walimcheka Ric.

Bella alienda kumlaza mtoto akarudi sebleni. “Vipi mbona huna raha.” Mama Mwasha alimuona Bella amerudi na uso usio na furaha. “Naomba mpigie simu Vin, muangalie hali yake.” “Kwa nini upepatwa na wasiwasi naye.” “Sijamsikia leo, halafu jana alikuja kazini hakuwa na raha kabisa mama. Naomba mpigie tu kujua ameshindaje.” Mama Mwasha alimpigia Elvin. Iliita mara ya kwanza ikakatwa, ikaita tena mara ya pili ikakatwa. Mzee Mwasha aliingiwa na wasiwasi. “Ngoja na mimi nimpigie.”  Mzee Mwasha alipiga simu ikaita muda mrefu ndipo Elvin akapokea. “Ninataka kukusalimia tu.” “Asante sana baba. Mimi nipo…” alianza kusikia kelele ya Happiness akigomba. “Usiku mwema baba.” Elvin aliaga na kukata simu. Walimuona Mzee Mwasha anasimama pale kitini kimya kimya na kwenda chumbani kulala. Mama Mwasha na Bella walikaa pale kimya kila mtu akiwaza lake.

************************************************************

Bella alijitahidi kuwa karibu na Elvin na kumfariji kwa kadiri ya uwezo wake, lakini alimuona kabisa ni kama amefikia mwisho. Kila siku alikuja kazini akionekana amechoka na mwingi wa mawazo. Kile kicheko kikapungua sana, hata kula yake ikaanza kuwa ya shida. Aliwahi kuja kazini mapema sana zaidi ya muda wake wakawaida na pia alimuacha pale pale ofisini. Wakati mwingine Bella alihisi anakuwa analala palepale ofisini, kwani alimkuta na nguo zile zile alizokuwa amevaa siku iliyopita, lakini aliogopa kumuuliza.

Jumamosi waliyotakiwa kwenda kwa Lewis na Toby, hawakwenda, Lewis alimpigia simu Bella na kumwambia amebanwa sana kazini, hawataweza kuonana siku hiyo, kwani atachelewa kutoka kazini. “Hamna shida Lewis. Kazi njema.” “Naomba tufanye jumamosi ijayo.” “Naomba usijisike kama upo na deni Lewis. Siku yeyote utakapopata nafasi tutaonana, au hata kama umezidiwa na kazi, sio lazima wewe uwepo. Unaweza kumleta Toby, mimi nikamrudisha jioni.” “Najisikia vibaya. Naona kama nakuachia mzigo mkubwa.” “Huna sababu yakujisikia hivyo. Toby ni mtoto mkubwa na anajitegemea. Hakuna kitu cha ziada kinachonilazimu kumfanyia. Kwa hiyo usiwe na wasiwasi.” “Sawa. Lakini Jumamosi ijayo nitakuwa nyumbani, sitaenda kazini. Nafikiri itakuwa siku nzuri ya nyinyi mfike nyumbani kwetu.” “Sawa.” Bella alikata simu na kurudi kucheza na mwanae.

*********************************************************

Ijumaa jioni wakati anaenda kumchukua mtoto wake, alikutana na Lewis. Hawakuwa wamewasiliana kwa muda wa juma zima. “Pole na kazi.” Bella alimuanza. “Asante na wewe. Mnaendeleaje?” “Sisi tupo salama kabisa.” “Na wazazi je?” Lewis aliuliza. “Hawajambo.” “Bado kesho mnaweza kuja nyumbani kwetu?” “Nakuona kama una majukumu mengi sana Lewis. Sitaki na sisi tuingie kwenye orodha ya majukumu ambayo unaona nilazima uyakamilishe. Nia yangu ni watoto wacheze pamoja tu. Lakini sio kuku…” Lewis alitabasamu. “Siwaoni nyinyi kama mzigo Enabella. Nitafurahi kuwaona kesho.” Bella alibaki akijifikiria. “Naomba iwe wakati mwingine Lewis. Nitakutaarifu siku tutakayokuwa na nafasi.” “Nimechukua mapumziko kesho siku nzima kwa ajili yenu.” Hamu ya urafiki ilishamuisha Bella, aliona anajiingiza kwenye ratiba nyingine ambazo asingeziweza, hata hivyo siku hiyo ya ijumaa aliiandaa rasmi kwa ajili ya ‘birthday’ ya Eli. Alitaka amfanyie ‘surprise’. Hakuwa amemwambia kabisa Eli mwenyewe ila ndugu zake wote walijua usiku huo Bella aliutangaza ni usiku wa Eli. Kwa hiyo alijua wangechelewa kurudi nyumbani, kwani alikuwa amemwandalia kwenye hoteli nzuri sana ya kifahari tena kwa pesa yake, na alijua wazi wangechelewa pia kulala siku hiyo ya ijumaa ya shuguli nzima, na hakutaka kumuamsha tena Ric asubuhi asubuhi.

 “Naomba mkaribie kwetu. Kutakuwa na mambo mengi yakufanya, nakuahidi hutajuta.” Bella alitoa tabasamu, lakini wazi alionekana alishabadili mawazo. “Tuje muda gani?” “Wowote tu kuanzia asubuhi. Hata mkitaka kifungua kinywa mje kupata kwetu.” “Sawa. Basi tutawasiliana wakati natoka nyumbani.” Waliagana kila mtu alirudi kwake.

Bella aliamka asubuhi kama kawaida yake, lakini akiwa na uchovu wa jana yake usiku. Kwani walichelewa sana kurudi nyumbani kutoka kusherehekea siku ya kuzaliwa ya Eli. Akafanya usafi, alipomaliza kupanga kifungua kinywa mezani, alishangaa kuona Elvin naye anaingia asubuhi hiyo. Alibaki akimwangalia kwani Elvin alitakiwa afike kwenye sherehe hiyo jana yake pamoja na familia yake, lakini hakutokezea na wala hakupiga simu yakutoa udhuru. “Kuna kitu chochote cha kula? Nataka nile nikalale.” Elvin alikuwa akiongea lakini ni kweli alionekana na usingizi. “Kila kitu kipo mezani na jana tuliwabakizia keki ipo kwenye friji. Nilete?” “Asante, lakini nitaila baadaye.” Elvin alikula haraka haraka akaingia chumbani kwake. Bella akamfuata. Alimkuta ameshajitupa kitandani amefunika uso wake kwa mto. “Unaumwa Vin?” “Hapana.” Alijibu kwa kifupi huku bado amejifunika mto usoni na amelala na viatu vyake. Bella alipiga magoti, akaanza kumvua viatu na soksi taratibu. Alichukua shuka lililokuwa pembeni ya kile kitanda akamfunika. Hicho chumba Mama Mwasha alikuwa akikisafisha na kubadili mashuka kila wakati, kwa kuwa alijua mwanae wakati wote huwa akilemewa nyumbani kwake, anarudi kupumzika hapo. Elvin alijigeuza vizuri, akapotelea usingizini.

Bella alitoka na kwenda kulia chooni. Alilia sana akimuhurumia Elvin, huku akijuta kwa nini alimuacha kwa muda wote ule mpaka akaoa mwanamke anayemtesa. Alitamani asiende kwa Lewis tena, ili abaki na Elvin, lakini alikumbuka Lewis hakwenda kazini siku hiyo kwa ajili yake. Alimsikia mtoto wake ameamka anamwita. Alimtayarisha mtoto wake, akamlisha huku akisubiria Elvin aamke ili amuage lakini Elvin hakutoka chumbani mpaka saa tano alipoona ujumbe unaingia kwenye simu yake. “Mnakuja au ndio nimeachwa kwenye mataa?” Uliingia huo ujumbe kutoka kwa Lewis. “Tunakuja sasa hivi.” Bella alijibu. “Basi tunawasubiri.” Bella alijishauri kidogo, akamfuata Mama Mwasha. “Nampeleka Ric kucheza kwa kina Toby. Sitachelewa. Elvin…., sitachelewa.” “Usiwe na wasiwasi Bella. Akiamka nitamwambia.” “Sawa mama. Lakini hana raha. Natamani nibaki ili akiamka angalau niwepo. Lakini kule kwa kina Toby nilitoa ahadi, wanatusubiria. Nikiona michezo imekolea, nitamuacha Ric, halafu nitarudi kuja kumuangalia Vin.” “Huna sababu ya kufanya hivyo Bella. Wewe nenda ukapate muda na mwanao, ukirudi utamkuta Elvin.” “Basi usimsahau chakula. Hakikisha anakula na kushiba. Baadaye umpe matunda na juisi ipo nyingi tu, nilitengeneza jana, naomba usiache kumpa. Tafadhali sana mama.” Bella alijisahau kama anaongea na mama yake Elvin mwenyewe. Tena anayempenda huyo mtoto kuliko kitu chochote. Mama Mwasha alicheka. “Sawa Bella, nitafanya hivyo.” “Naomba uwe makini na Eli, mama. Anaweza akamaliza juisi yote halafu Vin asipate kitu. Wewe si unamjua Eli?” Mama Mwasha alicheka. “Usicheke mama. Eli sijui yukoje! Umwambie akinywa yote halafu Vin akakosa, nikirudi nitamtapisha.”  Mpaka Mzee Mwasha aliyekuwa amelala kimya, akacheka. “Nitahakikisha hamalizi.” “Halafu kama ukimuona analala sana, labda umpelekee chakula huko huko chumbani. Umuamshe ale kwanza ndio aendelee kulala. Usimuache akalala muda mrefu sana bila kula.” “Sawa Bella.” Bella alisimama pale kwa muda kama asiyeridhika na maamuzi yake ya kwenda kwa Lewis. Alihisi hajaacha maagizo yakutosha. “Sijui umenielewa mama?” “Nimeelewa Bella mwanangu.Eli asimalize juisi, abakishe ya Elvin, nikiona amelala muda mrefu, nimuamshe kwanza, ale chakula ndipo aendelee kulala. Si ndio maagizo yenyewe?” Bella alicheka. “Ndio maana nakupenda mama yangu.”  Akatoka lakini akionekana hana furaha na anachokifanya.

Alivaa kiheshima tayari kwenda kukutana na wazazi wa Toby, lakini alipendeza sana kama kawaida yake. Bella, mtoto aliyezaliwa mjini, alijua kujipangilia. Kila alipotoka, alihakikisha amependeza, hajawahi kutoka kawaida. Kawaida ya Bella tu, hakuchosha kumuangalia. Alijaliwa kuwa na vitu vya thamani sana. Alimvalisha na mtoto wake vizuri, akapendeza ndipo wakatoka.

Mzee Mwasha ni wazee waliokuwa wamejenga nyumba zao zamani na wakabahatisha viwanja vikubwa. Walikuwa wakiishi Mbezi beach. Na walikuwa na eneo kubwa sana. Nyumbani kwa Lewis huko Bunju, hapakuwa karibu ya barabarani. Kwa hiyo iliwalazimu kuwa kwenye simu kwa muda mrefu wakielekezana. Kutokana na mawazo na kuzunguka sana, Bella alishafikiria kurudi njiani, bila kufika nyumbani kwa kina Toby. Hata hivyo alimuacha Elvin nyumbani, hakutaka aamke halafu asimkute. Wakati wote wa matatizo yake, Elvin ndio alikuwa faraja yake kuhakikisha anarudisha furaha usoni mwake. ‘Sitaki Elvin aone sasa hivi namkimbia.’ Bella aliendelea kuwaza huku akielekezwa na Lewis jinsi yakufika nyumbani kwake.

Kutokana na mawazo mengi, Bella hakuwa akitilia maanani maelekezo ya Lewis, kwa hiyo safari ilizidi kuwa ndefu. “Haupo mbali na nyumbani Enabella. Naomba usikate tamaa. Au egesha gari hapo hapo ulipo, sisi tutawafuata.” “Naona hilo ni wazo zuri.” Bella aliegesha gari akapotelea mawazozi. Alishtukia Lewis amesimama mlangoni kwake akimtizama. Alishusha kioo. “Samahani, umesimama hapa muda mrefu?” Bella aliuliza huku akitabasamu. “Sio sana. Niliogopa kugonga nisije kukushtua. Mliamka salama lakini?” “Ndiyo.” “Basi unifuate, ili tuongozane mpaka nyumbani kwetu. Lakini tunamuomba Ric ahamie kwenye gari yetu.” Bella alicheka. “Umepoteza imani na mimi nini?” “Hukawii kurudia njiani, usifike kwetu.” Wote walicheka. Bella alitoa loki ya milango ili Lewis aweze kumtoa Ric aliyekuwa amekaa kiti cha nyuma ya mama yake, akambeba na kiti chake cha gari, akamfunga kwenye gari yake.

Macho yalimtoka Bella alipoegesha gari yake pembeni ya gari ya Lewis nyumbani kwake. “Ushawahi kusikia nyumba za urithi?” Bella alicheka kwani alijua Lewis amemuona jinsi alivyoshangaa. “Umenishtukia nini?” “Nakuona unavyotoa macho. Najua huko kichwani unajiambia ‘Jamaa mambo yake safi kweli’. Nyumba ya wazazi wangu hii. Nilipewa mimi urithi baada ya kifo chao. Sijanunua hata tofali moja hapa.” Bella alicheka. “Utafikiri hoteli!” Bella alianza. Lewis alicheka. “Karibuni ndani.” Kwa kweli lilikuwa jumba la kisasa. Bella aliendelea kutoa macho. Picha zilizokuwa zimening’inizwa humo ndani, zote zilionekana kuchorwa vizuri sana. “Mama yangu alikuwa mchoraji sana. Kwa hiyo hizo ni moja ya kazi zake.” Bella aliendelea kuzunguka mle ndani. “Utafikiri jumba la maonyesho!” Bella aliendelea kushangaa kwa sauti ya juu huku akiangaza macho yake mle ndani. Alishika hiki na kurudisha kile.


*Lewis ameongezeka kwenye picha na Elvin naye yupo kwenye kipindi kigumu sana cha ndoa, anamuhitaji Bella. Nini kitaendelea

Usikose Sehemu ya 18.