Story

"My Past" Sehemu 3.

Thursday, April 20, 2017 Naomi Mwakanyamale 0 Comments

"My Past"

Sehemu 3.
Bella hakuwa na usingizi hata kidogo. Alijisogeza pembeni zaidi ili asigusane na Mzee Masha, akaendelea kulia taratibu. Ilikuwa ngumu kwa Bella kujua kama ametatua matatizo yake yeye na mdogo wake au ndio ameongeza matatizo zaidi. Alikaa akiwaza, mpaka ilipofika mchana Mzee Masha alipoamka. “Tuwahi kuzunguka madukani, Bella. Nataka ukanunue nguo za kutosha.” Katika maongezi yao, Mzee Masha ndiye aliyekuwa akitoa maagizo tu na Bella alikuwa lazima kuitikia jibu moja tu, la ndiyo. Alimzungusha kwa taksii kwenye maduka ya thamani. Alimnunulia nguo, viatu, pochi na pafyumu za gharama sana. Bella alibaki kimya kabisa akiangalia jinsi Mzee Masha anavyomwaga mapesa mengi sana juu yake. Walirudi hotelini Mzee Masha akionekana anafuraha sana, lakini sio Bella.

“Mbona upo kimya? Unafikiria nini?” Masha aliuliza lakini Bella hakujibu. “Ninapouliza swali, au ninapoongea na wewe nataka uwe unanijibu, Bella. Umenisikia?” “Ndiyo.” “Sasa nakuuliza, kwa nini upo kimya?” “Nasikia maumivu mkali sana, na…” Bella alinza kulia kwa kwikwi. “Ngoja nikupe dawa za kutuliza maumivu, nitaagizia chakula tule humuhumu ndani. Pole sana.” Kidogo Mzee Masha alionyesha ubinadamu. Alimpa dawa, na kurudi kukaa naye pale pale kitandani mpaka alipolala. Walikaa pale hotelini kwa siku kama nne zaidi. Asubuhi Mzee Masha alikuwa akitoka na kumuacha Bella hotelini mpaka mida ya mchana ndipo anaporudi na kuwa naye siku nzima, huku akimuhudumia kwa karibu, bila kumtaka tena kimapenzi. Alipunguza ukali kidogo, akawa na ubinadamu kiasi.

**************************************************

Bella hakujua ni nini Mzee Masha anafanya, na wala watoto wake hawakuwahi kuzungumzia biashara ya baba yao, lakini alijulikana kuwa ni milionea. Hata uzee ambao watu walikuwa wakimwita ni sababu ya pesa nyingi, lakini hakuwa mzee kihivyo. Wakiwa wanarudi Tanzania, wakati wapo kwenye ndege, alianza kumuuliza Bella. “Ungependa kuishi maeneo yapi?” “Popote tu.” “Nataka ufikirie, kisha uniambie ili nijue nakununulia nyumba maeneo yapi. Hatuwezi kuendelea kuishi hotelini tena.” Bella alitamani kuruka nje ya ile ndege. Kila alipofikiria kuwa ndio ameshaolewa, na nilazima aishi na yule baba, alihisi kuchanganyikiwa. ‘Lakini kwa sababu ya Ric, acha nikubali kujitoa kafara.’ Bella aliwaza. 

“Hili ndilo gari nimekununulia jana wakati umelala. Unalionaje?” Mzee Masha alitoa ‘Ipad’ yake na kuanza kumuonyesha Bella picha ya gari la thamani sana alilomnunulia. “Wamelisafirisha leo, kuelekea Dar.” “Asante sana.” “Umelipenda lakini?” “Ndiyo, nimelipenda.” Masha alifurahi sana. “Sasa bado sehemu ya kuishi. Nataka tukaishi kwenye nyumba yetu, Bella. Mimi na wewe. Umesikia?” “Ndiyo.” Mzee Masha alikuwa na sura iliyojaa furaha sana. Tabasamu halikumwisha usoni.

 “Maisha ya Bella na Masha yaanza rasmi.”
Bella alinunuliwa jumba la kifahari, Mbezi Beach. Ninaposema beach, namaanisha ufukweni. Hakujua yule mzee alifanyaje, kama alihamisha mtu au la, lakini Bella alitolewa hotelini na kuhamishiwa kwenye nyumba hiyo. Mzee Masha alikuwa ni kama amechanganyikiwa na Bella. Alijawa na furaha aliyoshindwa kuificha. Japokuwa alijulikana kama katili sana, lakini kwa kitendo cha kufanikiwa kummiliki Bella, furaha ilijidhihirisha usoni mwake. Huku hofu ya kuporwa Bella mjini hapo ikimsumbua, kwa tofauti ya umri wao, aliamua kutumia mabavu yote kumuogopesha Bella, ilimradi tu yeye ndiye awe mwanaume pekee kwake. 

Baada ya kuona utoto na hofu kwa Bella, yule dereva wa Masha kwa kujipendekeza kwa Masha, alimpa wazo la kumtafutia Bella, mama mtumzima anayeweza kumfundisha Bella maisha ya kuishi na mume na ya unyumba kwa ujumla. Masha alilipokea hilo wazo kwa furaha sana, yule dereva akamleta huyo mama aliyekuwa akilipwa mapesa mengi sana, ili awe anakuja kumfundisha Bella. Alikuwa akifika nyumbani hapo kila siku, kwa masaa matatu, mara Masha anapoondoka kwenda kazini, kasoro siku za Jumamosi na Jumapili ambazo Masha anapokuwepo nyumbani. Mzee Masha hakutaka mtu yeyote pale nyumbani kwao siku hizo au muda huo yeye awapo nyumbani. Alitaka abaki yeye na Bella tu. Nyumba ilijaa wafanyakazi wa kila namna, na wote walikuwa wakimtumikia Bella. Walikuja asubuhi na kuondoka wote jioni kabla Mzee Masha hajarudi nyumbani hapo. Wapo waliokuwa wakisafisha ndani, wengine nje. Wapo wafanyakazi waliokuwa wakifua, na wanaohusika na mambo ya jikoni. Kazi yake Bella ilikuwa ni kumfurahisha Mzee Masha na usafi wa chumbani kwake tu.

***********************************************

Kwa kuwa Masha alikuwa msafi wa kupitiliza, ile nyumba ilikuwa ikiwaka wakati wote. Hata Bella mwenyewe ilimlazimu kuwa nadhifu wakati wote. Masha alikuwa na kinyaa ambacho Bella alihisi ni ugonjwa. Hakuwa akitaka harufu mbaya au tofauti na harufu anazozichagua yeye. Nyumba yao ilinukia manukato aliyoyachagua yeye mwenyewe Mzee Masha, na Bella alitumia losheni, sabuni zakuogea na pafyumu alizochagua Masha, sio vinginevyo. Nguo za ndani za mzee huyo, zote zilikuwa nyeupe sana. Alijaliwa weupe na kwa kuwa alijua usafi, kwa kumwangalia tu, utajua ni msafi. Ngozi yake yenyewe iliwaka kama taa. Alitumia vitu maalumu kwenye mwili wake. Hakuwa akiogea kila sabuni au kupaka kila mafuta. Alikula na kujali mwili wake, kitu kilichokuwa kikimshangaza sana Bella, aliyezoea kuyaona hayo mambo kwa baadhi ya wanawake. Kila kitu cha Masha kilikuwa na usafi wa aina yake. Ilimlazimu Bella kujipenda zaidi yake ili kumridhisha na kuweka amani pindi arudipo nyumbani. Chumbani kwake hakutaka mtu yeyote aingie wala aguse hata kitanda anacholalia isipokuwa Bella tu. Na wafanyakazi wake wote walikuwa wasafi, na walivaa sare maalumu kila wajapo kazini.

*************************************************

Yule mama aliyekabidhiwa kumfundisha Bella aliporidhika na kuona amefanikiwa kumtoa Bella kwenye kundi la watoto na kumfikisha kwa watu wazima, ndipo alipomkabidhisha rasmi kwa Mzee Masha. Mzee Masha alimlipa pesa nyingine nyingi kama shukurani yake kwake. Bella alibadilika sana, na kwa kuwa mafunzo yote alikuwa akipewa kutokana na matakwa ya Mzee Masha, alijitahidi kumridhisha huyo Mzee kwa kadiri ya uwezo wake. Alikuwa kama mtumwa kwa Masha. Kwa kuwa pia alikuwa mtoto sana, na alifanya kwa kuamrishwa, na yeye alikubali kwa kumlinda mdogo wake. Kwani Mzee Masha alirudia rudia sana, kumtishia Bella uhai wake na mdogo wake, pindi Bella atakavyo fanya vinginevyo. Kwa hiyo Bella hakuwahi kufaidi mapenzi hayo hata kidogo. Alihesabu ni moja ya wajibu wake anaotakiwa kutimiza kila Mzee Masha atakapo muhitaji. Wakati mwingine Mzee Masha alitoka asubuhi akisema anaenda kazini, lakini baada ya muda mfupi alirudi nyumbani akisema anamuhitaji Bella. Alimtumia huyo mtoto kwa muda na wakati anaotaka yeye. Asubuhi, mchana au usiku, kwa kadiri alivyojisikia yeye siyo Bella.  Sehemu pekee aliyopata ya kutoa dukuduku lake ni kipindi akiwa chooni au Mzee Masha anapokuwa amelala au yupo kazini. Bella alikuwa akilia sana. Jumba lile la kifahari na mavazi ya thamani aliyonayo, hayakumpa furaha hata kidogo. Alijiona mtumwa wa kila kitu. ‘Lakini kwa sababu ya Ric, nitavumilia. Atakuja kumuua Ric bure. Huyu baba ni mkatili sana.’  Bella aliendelea kujifariji.

**************************************************

Muda mwingine Bella aliokuwa akiupata wakupumzisha mwili na akili zake, na hata kupata nafasi ya kwenda kumtembelea mdogo wake shuleni, huko Arusha ni pale tu Mzee Masha anapokuwa amekwenda nchini Uholanzi kuona familia yake. Hapo ndipo Bella aliweza hata kufikiria kitu kingine sio Mzee Masha pekee. Alinunuliwa simu, lakini hiyo simu ilikuwa imewekwa ‘GPS’, ambayo ilikuwa ikimuonyesha Mzee Masha kila mahali Bella alipo, kana kwamba isitoshe, aliitegesha jinsi ya kujirikodi. Kwa hiyo endapo simu yeyote ingeingia au kutoka kwenye simu hiyo, ingejirikodi namba na mazungumzo yote. Alimchunga Bella kupita kiasi. Alikuwa kama aliyekuwa amechanganyikiwa na mtoto huyo.

**************************************************

Siku moja Mzee Masha akiwa safarini, Bella aliamua kumtafuta dereva wao, Mat. Kwani ilishapita muda mrefu sana tokea siku ile alipowapeleka kwa Mzee Masha kwenda kuomba msaada, hawakuonana tena wala kuwasiliana. Aliwashusha nje ya geti na kuwaahidi angewafuata jioni yake. Alijua wazi Mat angekuwa na wasiwasi, kwani hakujua alijibiwa nini siku aliporudi kuwafuata. Hakuweza kumtafuta kwa kipindi chote hicho kwani alikuwa akifungiwa ndani, hakuruhusiwa kutoka mle ndani isipokuwa yupo na Mzee Masha tu, hata simu yenyewe alinunuliwa si kwa ajili yake, ni kwa ajili ya Mzee Masha mwenyewe pindi awapo mbali naye. Uzuri wa Bella, tofauti ya umri na mambo aliyokuwa akimfanyia Mzee Masha, ilimbidi Mzee Masha azidi kuwa makini sana kuhakikisha vijana wa mjini hawamzidi mahesabu.

Kwa mara ya kwanza Bella alitumia simu hiyo kumpigia mtu mwingine mbali na Mzee Masha. Na wala hakujua kama simu hiyo inauwezo wa kurikodi na kuonyesha alipo. “Nimewatafuta mpaka nimekata tamaa. Upo wapi?” “Nipo kaka. Nilitaka kukusalimia na kukujulisha tupo salama.” “Asante sana Bella. Nataka nije niwaone.” Bella asingeruhusu hata iweje Mat kufika hapo nyumbani kwake yeye na Mzee Masha, kwani kulikuwa na camera kila kona, na zote alikuwa akimuona Mzee Masha akizipitia kuziangalia kila arudipo nyumbani. “Tunaweza kukutana mahali.” Bella alimuwahi. Mat alikaa kimya kwa muda. “Hata hivyo Ric hayupo. Nipo mimi peke yangu. Kwa hiyo ni bora nije tu mimi.” “Kwani unaishi wapi?” “Naomba tuongee kila kitu tutakapo kutana.” “Lini?” Mat alihoji. “Hata leo. Au una kazi nyingi?” Bella aliuliza. “Kukuona wewe ni muhimu Bella. Sijui uko wapi, sijui mnaishije huko, lazima tuonane. Wakati wowote ule utakapokuwa tayari ukiniita, nitakuja.” “Basi naomba tukutane mida ya mchana. Tunaweza tukapata chakula cha mchana pamoja.” Bella alimpa maelekezo yote, muda na hoteli watakayo kutania na Mat.

Alivaa kawaida sana, ili asimstue Mat, lakini kutoka na uzuri wake, alipendeza kama kawaida yake. Tena hakutaka hata kuvaa vitu vya thamani. Alivua dhahabu alizokuwa amenunuliwa na Mzee Masha, na kurudisha cheni aliyokuwa amepewa zawadi na mama yake, tena ilikuwa  na kidani chake, ambacho kilibeba kumbukumbu zilizokuwa zikimpa nguvu za kuendelea kupambana na maisha anayoishi sasa. Swala la usafiri ndio lilianza kumsumbua, kwani gari alilokuwa amenunuliwa lilikuwa la kifahari sana, alijua lingeibua maswali mengi sana kwa Mat ambaye hakuwa tayari kumwambia maisha anayoishi kwa wakati ule, kwa kulinda usalama wake. Lakini sehemu waliyokuwa wakiishi hapakuwa na taksii, wala daladala, na simu aliyokuwa nayo kichwani ilikuwa ni ya Mat tu mbali na ya Mzee Masha. Kwa hiyo ilimlazimu aondoke na gari yake.

Alimkuta Mat anamsubiri sehemu ya kuegesha magari. Alibaki akimwangalia Bella alipokuwa akishuka kwenye gari hiyo. “Shikamoo kaka Mat.” “Ulisema unaishi wapi?” Hilo ndilo swali la kwanza Mat, alilomuuliza Bella mara baada ya kushuka kwenye lile gari, tena yeye akiwa dereva. “Bella?” Bella alishindwa kujibu kabisa. “Mtoto yuko wapi?” “Nimempeleka shule ya bweni, Arusha.” Bella alijibu kwa hofu kidogo. “Ndivyo alivyokuwa amekwambia mama yako hivyo?” Bella alinyamaza kimya. “Hiyo gari ni ya nani?” Bella alinyamaza. “Unaishi wapi na unaishi na nani?” Kimya. “Bella?” Kimya. Mat alibaki akimtizama Bella. “Ulisema kwa nini umenipigia simu?” Mat aliuliza kwa ukali kidogo. “Nilitaka kukusalimia tu, Kaka Mat.” “Naona kweli kilichokuleta hapa ni salamu. Si tumeshamaliza kusalimiana? Basi kwaheri.” Mat alitaka kupanda kwenye gari yake ili aondoke. “Naomba usiondoke kaka Mat.” Bella alianza kulia. Mat alikuwa ni kijana mwenye maadili na alijiheshimu sana.

“Naomba usiondoke kaka Mat. Nipo kwenye mazingira magumu sana, ambayo siwezi kukwambia. Lakini huku kukuona tu, kunanifariji kaka yangu. Naomba usiondoke. Angalau tukae kidogo. Wewe unanijua tokea mtoto, sijabadilika kaka.” “Hukua hivyo Bella.” “Naelewa kaka. Nakuahidi nitakujibu maswali yako yote siku nyingine, lakini sio leo. Naomba leo angalau nipate muda na wewe tu. Hata kama hatutaongea kitu, lakini hujui ni kiasi gani nafarijika hivi ninavyokuona tu. Tafadhali kaka Mat.” Mat alirudi. “Umekula?” Mat aliuliza. “Sijala kaka.” Waliingia ndani, wakaagiza chakula, wakaanza kula, kila mtu akiwa kimya.

“Naomba nikwambie kitu kaka, lakini usiniulize swali lolote, nitakujibu maswali yako yote wakati mwingine, lakini sio leo.” Bella alirudia tena, Mat alimtizama Bella kwa makini. Hali aliyokuwa nayo Bella na gari aliyokuwa akiendesha, viliibua maswali mengi kwa Mat, lakini kwa kuwa alimfahamu sana Bella tokea mtoto, kwa kumwangalia tu aliweza kujua kuna jambo kubwa sana linaendelea ndani ya ule unadhifu na utajiri aliobeba kwa nje.

“Kwanza nataka kujua kama huwa unakwenda kumuona mtoto?” “Ndiyo, huwa naenda. Na kesho pia nitakwenda kumtembelea. Lakini nataka ujue nafanya haya yote kwa ajili yake.” Bella alianza kulia. “Nataka asome sana, na awe na maisha mazuri.” “Na wewe? Unajifikiria na wewe mwenyewe lakini? Usiwe kama mama yako Bella. Mama yako amekufa akiwa anawahangaikia nyinyi. Umeshafikiria maisha ya Eric bila wewe wala mama yenu?” “Niko makini kaka.” “Sawa Bella. Naamini umejifunza kutokana na mama yako. Na aliongea na wewe bila kukuficha. Naomba usije ukasahu, ukarudia makossa. Shida tulizokuwa nazo wakati mnaishi na mimi pale Kigogo niza muda tu. Rudini nyumbani, tutahangaika, maisha yataendelea kwa kadiri Mungu atakavyojalia, lakini sitaki ujitoe kafara.” “Ulipata ile tenda uliyokuwa ukifuatilia siku ile ulipotuacha kwa kina Zera?” “Sikupata. Waliniambia gari ni ya zamani sana. Kama ingekuwa angalau ya 2014, ndio wangenikodisha. Kwa hiyo bado nahangaika. Lakini hatutashindwa kuishi Bella, rudi nyumbani.” “Sitaki Ric aendelee kucheza mpira tu mtaani, kaka. Lazima asome.” “Kwa nini tusimpeleke shule za kawaida? Rudi nyumbani Bella. Unaonekana wazi huna furaha.” “Unakumbuka shule tulizokuwa tukisoma wakati wa uhai wa mama? Elimu yake ni ya tofauti kabisa na elimu ya hapa Tanzania, kaka. Itamuia ngumu kuelewa darasani. Mpaka aje awe sawa na wenzake atakuwa ameshakuwa mtu mzima. Sipendi vile alivyokuwa anashinda pale mtaani, atajiingiza kwenye makundi mabaya, itakuwa ngumu kumrudisha tena kwenye mstari. Eric ana moyo mzuri sana, na sasa hivi ni msikivu. Akipoteza hiyo, ataharibikiwa kabisa.” Mat alinyamaza. “Natamani mambo yangekuwa kama zamani, Kaka Mat.” Bella alianza kulia tena. Mat alimuonea sana huruma. Alimfananisha Bella na mama yake. Tunu alikuwa hawezi kumuona mtu yeyote akiteseka akaacha kusaidia. Alikubali yeye akose, ili mwingine apate, hata kama itamgarimu vipi. Ikitokea upo kwenye shida, alisaidia bila kujali uadui wenu na ndio maana alidumu sana na Mat. Alimpenda Mat, kama mdogo wake wakuzaliwa tumbo moja. Hakumchukulia kama mfanyakazi wake.

“Ulitaka kuniambia nini?” “Sasa hivi nina pesa nyingi sana. Sina jinsi ya kumfikishia babu kule kijijini. Naomba umpelekee kiasi, na wewe uchukue. Nimekuja na pesa nyingi sana, zipo kwenye gari. Naomba uende kijijini ukamuone babu, mnunulie vyakula vingi. Msaidie kuvipanga vizuri, visiharibike ili awe anapata chakula chakutosha kila wakati na wewe naomba ubadili maisha yako.” “Mimi sihitaji msaada wako Bella.” “Naelewa kaka. Lakini naomba ufanye hivyo kwa ajili yetu. Ili siku moja na sisi tupate pakukimbilia.” Mat alibaki kimya. Bella alingalia saa, kisha akasimama haraka kama mshale. “Lazima niondoke sasa hivi. Naomba twende kwenye gari.”  Mat alisimama akiwa anafikiria sana huku akimfuata Bella kwa nyuma. 

Walipofika kwenye gari, Bella alitoa mfuko uliokuwa umejaa pesa. Mat alishtuka sana. “Beba mkoba mzima, utaenda kuhesabu hukohuko.” “Pesa zote hizi? Umezitoa wapi Bella?” “Nilikuomba leo usiniulize maswali kaka yangu. Wewe chukua na uondoke. Halafu Kaka Mat, hii karatasi nimeandika shule na jina kamili la Eric. Uwe unaenda kumtembelea. Nakuomba usiwahi kunipigia simu, hata iweje, mimi ndio nitakuwa nakupigia.” Mat alibaki akimtizama Bella huku haamini. Kwa kipindi hicho ambacho kila Mtanzania analia hali ngumu ya uchumi, lakini Bella alikuwa na pesa ambazo alimpa bila kujali atazitumia vipi. Bella aliingia ndani ya gari na kuondoka kwa haraka.

**********************************************

Alikuwa akiwahi nyumbani kwake, kwenda kuongea na Mzee Masha, kwa kutumia kompyuta ya mezani kwake. Mzee Masha alikuwa akitumia njia hiyo makusudi, ili kuhakikisha Bella yupo nyumbani. Na alipiga kila siku muda ambao Bella alijua anakwenda kulala huko nchini Uholanzi alipo kwa familia yake. Pesa alizompa Mat, alijua Mzee Masha hawezi kugundua, au kujali kwani alikuwa akimuona akiingiza mle ndani mamilioni ya pesa mara kwa mara. Wakati mwingine alikuwa akiingia nazo usiku kwenye mabegi, na wakati mwingine alitoka na baadhi ya hizo pesa bila kumuona akihesabu. Ni yeye na Bella tu ndio walijua zilipo hizo pesa alizokuwa akizifungia kwenye SAFE kubwa ya chumbani kwake, nyuma ya chumba cha nguo. Ilikuwa ngumu kwa mtu yeyote kuiona hiyo SAFE kwa haraka kama ukiingia chumbani humo, kwani ilifichwa nyuma ya suti zilizokuwa zimening’inizwa za Masha. Ni yeye na Bella tu ndio walijua kama kuna Safe humo ndani na jinsi ya kuifungua. Alimruhusu Bella kutumia atakavyo.

**************************************************
Wakati anaingia ndani, alisikia simu ya Mzee Masha ilikuwa ikiita kwenye kompyuta. Bella alitamani kulia kwani alikuwa amechelewa kama kwa dakika mbili tu. Alikimbia, lakini alipoikaribia kompyuta ili apokee  ile simu kwa njia ya skype ilikata. Bella alikaa chini nakuanza kulia. Alijua wazi adhabu inayofuata kwa kutopokea simu yake. Baada ya muda mfupi kupita, zilianza kuingia kwenye simu yake picha zake akiwa na Mat na zote zilitoka kwa Mzee Masha. Bella aliitupa ile simu kwa hofu kubwa sana na kuanza kufikiria.

Japokuwa alishapigwa marufuku kumpigia simu Mzee Masha akiwa na mkewe, Bella aliisogelea ile kompyuta na kumpigia simu Mzee Masha. Iliita bila kupokelewa. Alipiga tena na tena mpaka alipopokea. “Muonyeshe Zera hizo picha, anamfahamu huyo kaka, anaitwa Mat alikuwa dereva wetu. Ndiye aliyekuwa akitutunza mimi na Ric, wakati tukiishi Kigogo. Unanisikia Mzee Masha? Usije kumdhuru hata kidogo. Amekuwa kama ndugu sasa hivi, na ndiye mtu pekee tuliyebaki naye maishani. Umenisikia? Kwa mara ya kwanza Bella aliweza kuongea na Mzee Masha kwa hasira na kumfanya ashtuke kidogo na kubaki bubu kwa muda. “Ukimdhuru tu au ukimfanyia kitu chochote, utakuta maiti humu ndani. Nakuapia kwa Mungu, Masha. Hutanikuta, nitajiua.” Bella alishajua udhaifu wa Mzee Masha, kuwa ni yeye. Alijua wazi hawezi kuishi tena bila yeye. Kuna vitu alivyokuwa akimfanyia, ambavyo Mzee Masha alikiri ni Bella pekee ndiye anayeweza kumfurahisha kwa kiasi hicho. Upendo wake kwa Bella ulizidi, japo wivu ndio ulizidi kipimo, nakumfanya awe mbabe kwake. 

Bella alikuwa anatetemeka sana. “Umenisikia? Usikate simu bila kunijibu na nataka uniahidi hutamfutailia Kaka Mat. Na nimempa pesa za kumpelekea babu kijijini, kwa kuwa nilijua hutaniruhusu niende mimi mwenyewe.” Bella aliendelea kuongea bila kujibiwa. “Sema kitu chochote T. Please. Usipojibu kitu, ninakata hii simu, na hutakaa ukasikia sauti yangu tena.”  Mzee Masha alishamkataza Bella kumwita Mzee Masha, alitamani sana awe anamwita jina lake Tito. Sasa kusikia anaitwa T, ilimtuliza zaidi. “Narudi kesho, tutaongea vizuri.” “Hapana, huwezi kurudi kesho. Kesho naenda Arusha kwa Ric.” “Nisubiri twende wote.” “Haitakaa ikatokea Ric akatuona mimi na wewe tuko pamoja, hata iweje. Umenielewa?” Mzee Masha alizidi kushangaa ujasiri wa Bella, wa siku hiyo. “Kwa nini?” Mzee Masha aliuliza. “Kwa nini unataka kumuona Ric?” Bella aliuliza kwa ukali kidogo, nakumfanya Masha anyamaze.  “Wewe shida yako ni mimi. Nimekubali kukufanyia kila kitu unachotaka, kaa mbali kabisa na Eric. Tena wala nisikusikie hata umemtembelea shuleni wala kumsogelea. Wewe sio baba yake na wala huna maadili mazuri yakumfundisha Eric kitu chochote kile. Eric ni jukumu langu mimi. Kesho nakwenda kumuona, na kesho kutwa nitakuwa hapa nyumbani. Mtume dereva aje anichukue anipeleke uwanja wa ndege, nataka tiketi ya asubuhi.” Bella alikata simu nakuanza kuhema kwa nguvu. Hata yeye hakuamini kama ameweza kuongea na Mzee Masha nakuweza kumudu kumbadili mawazo.

Haraka sana aliokota simu yake iliyokuwa vipande vipande pale sakafuni, akaiunganisha na kumpigia simu Mat. “Kaka Mat? Kaka Mat?” Bella aliita kwa wasiwasi kwani simu ilipokelewa lakini hakuna aliyeongea. Mwishowe alisikia sauti ya mtu mwingine lakini sio Mat. “Mpe simu Mat haraka sana.” Bella aliongea kwa ukali. “Kuna nini Bella? Nini kinaendelea na hawa vijana ni kina nani?” “Wamekuumiza?” “Hapana. Lakini wamenitoa kwenye gari na kunipokonya kila kitu. Ngoja kwanza.” Mat alinyamaza kwa muda. “Kaka Mat!” Bella aliendelea kuita kwa wasiwasi. “Nipo nipo. Subiri kidogo Bella.” Baada ya muda, Mat aliita. “Bella?” “Nipo kaka.” “Wamenirudishia kila kitu changu na kuniomba msamaha. Ni kina nani hawa?” “Samahani kaka, na pole. Hawatakusumbua tena. Rudi tu nyumbani. Usisahu maongezi yetu.” Bella alikata simu nakuanza kulia sana. Alilia siku nzima akiwaza juu ya maisha yake yalivyogeuka kuwa yakitumwa. Alijuta na kulaani siku aliyopata wazo la kwenda kuomba msaada nyumbani kwa kina Zera. Hakujua kama analindwa kwa kufuatiliwa kwa kiasi kile. Alijua ndio amepoteza uhuru wake kabisa. Hana tena maisha yake binafsi, na kila atakayemsogelea yeye atakuwa hatarini. Alilia asijue chakufanya.

**************************************************

Asubuhi alikuja kuchukuliwa kupelekwa uwanja wa ndege wa Mwalimu Nyerere tayari kwa safari yake ya Arusha. Alitua uwanja wa ndege wa KIA, bado ilikuwa mapema tu. Akatoka nje ya uwanja huo akiwa na lengo la kutafuta usafiri wa kumpeleka jijini Arusha, lakini akakuta mtu amebeba bango lenye jina lake hapo nje akimsubiria. Alimsogelea. “Mimi ndio Enabella.” Bella alijitambulisha, wakasalimiana kwa kifupi sana, yule mtu akionyesha heshima kubwa sana kwa Bella. “Nimeagizwa nikufuate. Una mizigo yeyote?” “Hapana.” Hakutaka kuuliza maswali mengi, alijua tu ni mmoja wa watu wa Mzee Masha. Akapanda kwenye gari mpaka jijini Arusha, shuleni kwa Ric. 

Eric alifurahi sana kumuona dada yake. Alimkumbatia kwa muda mrefu sana. Ilikuwa kama mtu anaosha moyo wa Bella, moyo wake ulifunguka, furaha ya ajabu sana ikaingia nafsini mwake. Kwa muda mrefu wa matatizo, Bella alijikuta akicheka baada yakumuona Ric.


“Unazidi kuwa mrefu na kunenepa. Unasoma kweli?” Bella alianza kumuuliza mdogo wake. “Shule ni nzuri sana Bella. Nimeipenda. Kwani utanihamisha tena?” Bella alifurahi sana kuona mdogo wake anafurahia hiyo shule, kwani yeye alijawa na hukumu moyoni. Aliona ni kama amemtelekeza mdogo wake, kitu alichokuwa ameonywa na mama yake. Lakini alishindwa kumuhamishia Dar, hakutaka mdogo wake ajue maisha anayoishi na Mzee Masha. “Unauhakika unataka kubaki hapa?” “Lakini kama ni gharama sana, nitaenda popote kule.” “Usiwe na wasiwasi na pesa, Ric. Ninachotaka ni wewe uwe na furaha.” Eric alianza kucheka. “Ninafuraha sana Bella. Ujue nini?” Bella alicheka na yeye, alimuona vile Ric alivyojawa na furaha, akajua mateso yake sio bure. “Nini?” “Nimechaguliwa kwenye timu ya mpira wa kikapu, {basketball} wamesema mimi ni mrefu sana, kocha wa mpira wa miguu pia amesema niingie kwenye timu yake.” “Sasa unaenda kwenye timu ipi?” “Ndio nataka nikwambie wewe kwanza, unisaidie kuchagua. Maana vyote natakiwa kulipia. Lakini kama huna hela naweza kusubiri tu, hamna haraka.” “Kwa nini usicheze michezo yote, halafu baadaye ndipo ukafanya maamuzi?” “Kweli Bella? Utanilipia!?” “Lakini uniahidi utasoma Ric. Kumbuka mama alivyosema tusome sana.” “Na wewe umeanza shule?” Bella alipooza kidogo. “Nitaanza Ric.” Bella alipotelea kwenye mawazo. “Umependeza sana Bella.” Ric alijaribu kumtoa dada yake kwenye mawazo. Bella akacheka kinyonge. “Asante Ric. Lakini nimefurahi sana kukuona.” Walikaa siku nzima wakicheka, angalau Bella alisahau maisha yanayomsubiri jijini Dar.


Usiku ulipoingia, aliamua kurudi hotelini kupumzika. Usiku kucha wakati yupo hotelini, Bella alikuwa akijiambia jinsi ya kuyabadili maisha yake na kujaribu kumpokea Mzee Masha moyoni mwake, ili aendelee kumnufaisha mdogo wake. Bella alikuwa mtoto mdogo sana, ndio alikuwa ameingiza miaka 18 tu. Alibaki akilia na kutamani kama mama yake angekuwa hai abaki kuwa mtoto sio kama sasa hivi anaishi kama mke wa Mzee Masha. Alijihesabia miaka yake, nakujilinganisha na Zera, ambaye ni mtoto wa Mzee Masha, ambaye kwa wakati huo alikuwa shuleni. Ric alimuuliza swali lililomfanya ajiulize na yeye zaidi. ‘Mzee Masha ataniruhusu kutoka pale ndani kila siku na kwenda shule? Nina zungukwa na walinzi wake kila mahali. Ukute hata hapa hotelini yuko mtu ananilinda. Sina raha hata kidogo. Alinisamehe kukutana na Kaka Mat, nafikiri sababu ya kumwita T. Labda nibadilike, nimuonyeshe nampenda, labda ataacha ukatili. Lakini anafanya kazi gani? Mbona anapesa nyingi sana?’ Bella aliendelea kupanga mikakati ya maisha yake, mpaka alipopitiwa na usingizi.

Asubuhi alipoamka na kujitayarisha, akatoka mle chumbani na kushuka chini mpaka mapokezi. Akakuta yule dereva akimsubiria. Alimuomba amrudishe tena shuleni kwa kina Ric, kama alivyomuahidi. Alilipia kila kitu kilichokuwa kikitakiwa, muda wa ndege yake kuondoka Arusha ulipofika, ilimbidi Bella amuage mdogo wake ili asichelewe ndege. Alitamani kulia, lakini aliapa kutomuonyesha mdogo wake hisia zake za ndani. Aliamua kufa ndani kwa ndani.


********************************************

Akiwa kwenye ndege Bella aliendelea kuwaza huku machozi yakimtoka. ‘Narudi tena jela.’ Mama aliyekuwa amekaa pembeni yake, alijaribu kumuuliza kama yupo sawa, lakini kama kawaida ya Bella ya kuongea pale anapoamua yeye, alinyamaza bila yakumjibu yule mama. Ni Mzee Masha tu ndiye ilimlazimu kumjibu. Bella aligeukia dirishani na kuendelea kuwaza. ‘Lazima nibadili maisha yangu. Lazima niyakubali hivi yalivyo sasa, ili niweze kuishi na Mzee Masha vizuri. Hakuna dalili ya kutoka kwenye maisha ya yule mzee, sio leo wala kesho. Ameniapia kifo pekee ndicho kitatutenganisha. Lazima nifanye maisha yangu yawe rahisi mle ndani.’ Bella aliendelea kupanga mipango yake huku akitokwa na machozi. Yule mama alishindwa kukwepesha macho yake, kwani uzuri wa Bella aliokuwa nao, na vitu vya thamani alivyokuwa amevaa, na harufu nzuri aliyokuwa akinukia, ilikuwa ngumu kujua kama ni mtoto wa milionea, au ana mwanaume mwenye pesa nyingi. Na kwa kuwa alikuwa akitokea Arusha, alijua lazima ni mmiliki wa mgodi ndiye anayemmiliki binti huyo. ‘Kitakuwa kinatembea na waume za watu hiki kitoto.’ Yule mama alijisemea  moyoni.*********************************************
Alifika uwanja wa ndege wa Dar, akakuta dereva akimsubiri. Aliendelea kushangaa jinsi Masha ambavyo anamuhangaikia bila hata kumuomba. Alimwandalia kila kitu. Kuanzia usafiri wa kumtoa sehemu moja kwenda kwingine mpaka hoteli aliyofikia jijini Arusha. Dereva huyo alimpeleka hotelini bila hata Bella kujua kama alishaandaliwa sehemu ya kulala jiji hapo. 

Waliondoka pale kwenye viwanja vya ndege vya Mwalimu Nyerere, giza ndio lilikuwa likiingia, na kwa sababu ya foleni njiani, alifika  nyumbani kwake usiku. Alimkuta Mzee Masha akimsubiri sebleni. Alishtuka kidogo. “Pole na safari.” Bella alisalimia kwa hofu asijue nini kitafuata. “Asante na wewe pole na safari. Eric anaendeleaje?” “Asante. Anaendelea vizuri tu." Bella alitulia kidogo kama anayesubiria aone kinachofuata. Masha alikuwa ametulia kwenye kochi, akazima tv, na kufunga gazeti alilokuwa anasoma, akaweka pembeni. "Asante kwa maandalizi ya safari. Sijasumbuka hata kidogo." Bella aliongeza. "Afadhali na karibu." Masha alijibu na kubaki akimtizama Bella. "Umeshaoga?” Bella alimchokoza kama kumpooza. Alishajua udhaifu wake, akaamua kuutumia ipasavyo. Mzee Masha alicheka kidogo. “Nakusubiri wewe.” “Twende basi.” Bella aliongea kwa upole, na kumfanya Mzee Masha aliwazike. Aliweka pochi yake juu ya meza, akaanza kufungua zipi yake pembeni ya ubavu wa gauni hilo alilokuwa amevaa huku  akimtizama Masha, akaelekea chumbani. Masha naye akasimama kumfuata na tabasamu usoni. Alishangazwa na ushirikiano wa mara ya kwanza alioupata kutoka kwa Bella.


“Umekuwa na wakati mzuri huko?” Bella alihoji taratibu. “Akili yote ilikuwa huku.” Bella alicheka kidogo. “Nimekuudhi?”  Bella aliuliza huku amemuegemea kwa karibu sana. “Sio sana. Lakini ningependa uwe unanitaarifu mambo mapema, Bella. Unanichanganya kweli. Nimeshindwa hata kuendelea kukaa huko.” “Pole. Nilijua nikikwambia mapema ungeweza kunikatalia. Wakati yule kaka alitusaidia sana. Usiwe na wasiwasi T, bwana. Siwezi kukuzunguka.” “Kweli Bella? Au unanidanganya tu?” “Nakwenda wapi? Wakati kila kitu unanipa?” Kichwa kilikuwa kinakaribia kupasuka, kwa sifa. Furaha iliyomuingia iliondoa hasira zote. “Haya bwana.” “Kwanza nimefurahi umerudi mapema, nilikuwa nimepooza.” Bella aliamua kuendelea kumdanganya. “Sijakuletea zawadi lakini. Nimeondoka nikiwa na haraka haraka sana.” Bella alicheka kidogo. “Unanicheka?” “Wivu utakuuwa Tito. Sasa ulifikiria nini?” “Hawakawii watoto wa mjini kunipora. Na uzuri wote huo!” Bella alimbusu mgongoni alipokuwa akimsugua wakiwa wamekaa kwenye jakuzi lenye maji vuguvugu. “Hamna wakukupora bwana. Twende ukanipe zawadi yangu.” “Nimekwambia sijakuletea kitu chochote, Bella.” “Wewe ndio zawadi yangu bwana.” Mzee Masha alihisi yupo ndotoni, kwani wakati wote ilimbidi kutumia nguvu kulala na Bella, lakini usiku huo, Bella ndiye aliyekuwa akimtaka kimapenzi! Hakuamini. Alimgeukia Bella, akambusu na kutoka naye bafuni, kurudi naye chumbani.

***************************************************

Ukweli Bella aliamua kubadilika, na akaziteka fikra za Mzee Masha kupita kiasi. Alimfanya ajione kama kijana kabisa. Alimwita majina ya mapenzi tena kwa utaratibu. Bella alikataa kabisa kutoka mle ndani bila Mzee Masha. Alimfanyia utundu mwingi sana wakitoto, uliozidi kumchanganya. Taratibu alianza kujisahau kama ameoa na alikuwa ni mtu wakuheshimiwa sana kwenye jamii. Alirudia tabia za ujanani, angalau kujifananisha na Bella. Bila hofu au haya alianza kutoka na Bella sehemu mbalimbali za starehe. “Huwezi kuendelea kujifungia humu ndani Bella. Unakuwa kama mama mzee!” Bella alicheka, lakini moyoni alijua wazi kabisa, salama yake ni kuwa mle ndani, kwani akijichanganya tu, akatoka, ataibua matatizo kati yao, kwani alimjua jinsi Mzee Masha alivyo na wivu na katili. “Wewe hufurahii hivi unavyonikuta nakusubiri nyumbani?” “Nafurahi, lakini sitaki ukaja kuyachoka haya maisha.” “Siwezi T. Labda unikimbie.” “Naenda wapi Bella?” “Ukipata dogodogo mwingine?” “Wewe umeshakutana na mwingine kama wewe?” Bella alicheka sana. “Haya bwana. Lakini kama nikutoka lazima tutoke wote, sitaki kutoka peke yangu.” Mzee Masha aliona kama amekabidhiwa dunia. Akaanza kuwahi sana kurudi nyumbani kukaa na Bella.

Safari za Uholanzi kwa familia yake zikaanza kupungua, huku akimkataza mkewe asirudi Tanzania kwa kisingizio kuwa yeye anakuwa safarini. Aliona shida sana kumtaja mkewe kwa Bella, na Bella naye kama alivyofundishwa na yule mama, mwalimu wake, hakutaka kwenda kinyume naye. Alimwambia iwe mwiko, kumtajia mkewe, na wala asionyeshe wivu. Tena anapomtajia mkewe, aonyeshe kumuheshimu sana, akamwambia ndio njia pekee ya Mzee Masha kuwa upande wake yeye. Alimfundisha mapishi mengi mazuri ya kiswahili, na huo ujuzi wa mke, uliokuwa ukimchanganya Mzee Masha.

Waliongozana kama kumbikumbi, vicheko na amani vilitawala kati yao. Mzee Masha akageuka kuwa mwema kupita kiasi. Akaanza kumshirikisha Bella baadhi ya mambo yake. Alipotoka kwenda kazini, Bella hakuacha kumwandikia kiujumbe kidogo, na kukiweka kwenye shati lake, huku akimwambie akasome akishafika kazini kwake. Alimwambia ni jinsi gani alivyo wa thamani na hakuacha kumshukuru kwa kumtunza yeye na mdogo wake. Alimwandikia jinsi anavyomsubiri arudi nyumbani, ili wafanye hili au lile, ilimradi tu, kumchanganya Mzee Masha. Akaanza kwenda naye Arusha kumtembelea mdogo wake, lakini  yeye alimuacha hotelini. Akawa ana kwenda kwa mdogo wake akiwa peke yake. Kwa kuwa alisafiri naye, safari za Arusha zilianza kuwa kila mwisho wa juma. Walisafiri wawili hao, walilala siku ya kwanza hotelini bila kutoka, kisha siku inayofuata Bella alikuwa akienda shuleni kwa mdogo wake, nakurudi hotelini alipokuwa akimuacha Masha. Mzee Masha alikuwa akiona anathaminiwa sana na Bella. Penzi lake kwa Bella lilizidi kukua.

***************************************************

Siku zilizidi kwenda, Masha akiendelea na kazi zake nyingi, huku Bella akibakia nyumbani akimsubiria. Alitamani sana kurudi shule japo aliogopa kumwambia Mzee Masha. Kwani alishamuonyesha Bella hakuna sababu yakurudi tena shule, yeye ameshampa kila kitu na alishamfungulia hata dola akaunti. Ni kweli Bella alikuwa na pesa nyingi sana, lakini bado alitamani sana kurudi shuleni. Kila alipotaja swala la yeye kusoma, alimuona jinsi Mzee Masha anavyobadilika gafla. “Walimu watakuchezea tu Bella. Kwanza unataka kusoma ili iweje? Una kila kitu. Unayo pesa yakukutosha benki, nyumba nzuri unayo, gari ya kifahari unayo, sema hutaki tu kuiendesha mwenyewe.” “Nataka tuwe tunakuwa wote T. Haya mambo ya kuendesha kila mtu gari yake, ndio chanzo cha kuanza kupishana mlangoni.” “Kweli Bella umetulia. Nakushukuru mpenzi wangu.” Bella alitabasamu.

Aliendelea kuwaza jinsi ya kumfanya Masha amkubalie arudi shule, bila mafanikio. Mwishowe akapata wazo. Lakini alimuona vile alivyo na kazi nyingi, akirudi amechoka, akaamua amtoe pale jijini ili akajaribu kutupia ndoano nyingine, sehemu tulivu. Alimsubiri siku hiyo baada ya kutoka kazini, akiwa amepumzika, akajisogeza mpaka alipokuwa amening’iniza miguu yake kwenye stuli, akainyanyua, akakaa na kuipakata miguu ya Masha, na kuanza kuiminyaminya taratibu. “T!” Bella alimwita taratibu. “Naona tumekaa sana nyumbani. Halafu umekuwa nashuguli nyingi kweli. Ukirudi unakuwa umechokaa tunakosa muda mpenzi wangu. Twende tukajifungie mahali. Mimi na wewe tu. Tena unazima na simu yako kabisaa.” Mzee Masha alifurahi sana. “Chagua basi wapi unataka twende Bella.” “Tutafute sehemu ambayo na wewe hujawahi kufika. Tukajifungie huko, hamna hata kutoka nje mpaka niridhike.” “Utaniua Bella wewe! Ujue mwenzako Mzee?” Wote walicheka. “Usijizeeshe bwana. Bado unadai kabisa.” Kwa kuchanganyikiwa na mapenzi, Mzee Masha alikuwa akiamini kila anachodanganya na Bella, na kusahau kabisa kuwa Bella ana umri sawa kabisa na binti yake wa mwisho.

Japokuwa ni kweli aliwahi kuzaa, lakini bado Mzee Masha kama wengi walivyozoea kumwita sababu ya pesa zake, alikuwa mkubwa kwa Bella. Masha alikuwa na miaka 48 na Bella 18. Mtoto wa kwanza wa Masha alikuwa na miaka 20, wakati Zera alikuwa na umri unaolingana na Bella, miaka 18.

“Bella akanyaga visiwa vya Caribbean, kwa mapumziko.”
Kwa kuwa ulikuwa msimu wa joto nchini Marekani, Mzee Masha alitafuta sehemu nzuri sana ya kwenda kupumzika, kama Bella alivyoomba. Walikwenda kwenye visiwa vya Caribbean. Wakati wengine wakilia njaa, Bella aliponda raha kana kwamba anaishi nchi nyingine siyo Tanzania. Walitua visiwani humo ikiwa ndio mara yao ya kwanza kufika visiwani hapo. Japokuwa Bella hakuwa akifurahia chochote kinachoendelea kati yao, hususani mapenzi, lakini alifurahia sana utulivu wa visiwani hapo. Walikuwa na wakati mzuri sana. Masha alianza mapenzi ya kumbembeleza Bella, na kweli walijifungia bila kutoka kwa siku mbili mfulilizo, Bella akimtumikia Masha ipasavyo bila kuchoka, huku Bella akionyesha yeye ndio anafaidi zaidi yake. Alimwaminisha Masha kuwa wakati wote alipokuwa akimgusa, aliridhika, kumbe ulikuwa ni uongo tu. Masha alijivunia sana kwa kila anachomfanyia Bella hapo kitandani, nakuona uthamani wake. Bella alimpa heshima zote na kumsifia sana.

“Sasa hapa si itakuwa imekugharimu sana?” Bella alijaribu kuhoji siku hiyo jioni walipokuwa ufukweni wakitembea kwa mara ya kwanza tokea wafike visiwani hapo, kwani kwa siku mbili walibaki chumbani tu. Masha akisema anahitaji sana ule muda wa mapumziko kwani alikuwa na shuguli nyingi sana huko nyumbani. Na ni kweli alipata muda wakulala vizuri, kwa kuwa hakuwa akiwaza kazi, na Bella mrembo wake akiwa pembeni yake.


Ilikuwa rahisi kwao kutembea pamoja, au hata Bella kumbusu Masha na kuonyesha mapenzi yao waziwazi, hadharani bila shida katika maeneo hayo, kwani hakuna aliyemjali mwenzake. Kila waliyekutana naye huko, alikuwa akiangalia mambo yake. Kwa hiyo hata Mzee Masha hakusita kutembea akiwa amemshika Bella kiuno, akijivunia mapenzi ya mtoto huyo. “Unastahili Bella. Hakuna gharama inayoweza kufikia mapenzi unayonipa. Unanipenda, unanitii, na kuniridhisha kwa kila hali. Unastahili Bella wangu.” Bella aliona jinsi Mzee Masha alivyokolea, akaamua kutoa ombi lake, kabla hajabadilika. “Asante T. Lakini unajua nini?” “Nini?” Mzee Masha alimgeukia Bella kutaka kujua anachotaka. Bella alisita kidogo. “Niambie tu Bella. Usiogope.” Bella alitabasamu na kumbusu kwa muda kisha akajisogeza karibu na mabega yake. “Natamani nikianza shule, wewe ndio uwe unanipeleka na kuja kunichukua.” Kidogo Mzee Masha alitulia, Bella akaogopa kwani alijua wazi ni kiasi gani asivyopenda aende shule kwa kuhofia atamsaliti pindi atakapokutana na vijana wengine. “Au hutaki watu watuone tupo pamoja?” Bella aliunganisha kuzidi kumpoteza. “Hapana Bella. Mimi nilidhani unahofia kuonekana na mimi?” “Jamani T! Kwa nini?” “Huwezi jua bwana, unaweza ukakutana na vijana wenzako ukaniona sifai tena.” “Umeanza wivu T. Nitakuwa natafuta nini tena?” “Sijui.” “Siwezi T. Nimeshakwambia zaidi ya mara kumi, nimeridhika na wewe. Usiwe na wasiwasi. Umesikia?” “Nakusikiliza.” “Wewe mwenyewe uliniambia kifo ndicho kitatutenganisha, au umesahau?” “Natamani na wewe ungesema hivyohivyo Bella. Angalau nikusikie hata mara moja tu ukiniambia unanipenda.” “Mimi ni mzuri wa vitendo T.  Unanijua sio muongeaji sana. Sasa heri ni lipi? Niongee sana halafu nihangaike na wanaume wengine huko nje au nikuonyeshe vitendo vyangu kuwa nimetulia na kuridhika na wewe?” “Heri kutulia. Siwezi kuvumilia na sitakaa nikusamehe hata siku moja nikisikia umenisaliti Bella. Nitamuua huyo mwanaume.” Bella alishtuka sana. “T!?” “Nakuapia kwa Mungu. Hiyo ndiyo itakuwa adhabu pekee itakayomstahili mwanaume atakaye kutoa kwangu. Sitasamehe Bella. Wewe ni wangu.” Bella alitamani kukaa chini. Alipooza gafla, uongo wote ulimwisha.


Ukweli hakuwa na hisia zozote zile za kimapenzi kwa Mzee Masha. Moyo wake ulijaa machungu yakupitiliza. Kila alipokuwa akimshika, alijikaza sana ili kuweza kuishi na kuendelea kumsomesha mdogo wake aliyekuwa akilipiwa ma milioni ya pesa. Hata milango ya kutoka kwa Mzee Masha ilishafungwa, alimwahidi kifo pekee ndicho kitakachomtoa kwake. Hakuwa na jinsi isipokuwa kukubaliana na hali halisi.

“Unataka kuanza shule lini?” Mzee Masha alimua kuvunja ukimya wakati wanalala, kwani ni kweli Bella alipooza sana. Tokea wapo baharini, alipomwambia vile, Bella hakuongea tena, wakarudi chumbani wote wakiwa kimya, na Mzee Masha alionyesha hakuwa akitania, alimaanisha kila kitu alichomwapia Bella. “Wakati wowote utakao ona unafaa.” “Mbona tena umebadilika?” “Unanitishia sana, T. Nimejaribu kukuonyesha kuwa nimetulia, lakini bado huniamini.” “Sikuogopeshi Bella. Nakwambia ukweli ili ujue na ujihadhari. Sitakubali kukuona na mwanaume mwingine hata iweje. Umenisikia Bella?” “Ndiyo.” “Kwa hiyo hata kama ulikuwa na wazo hilo, tafadhali Bella, nakuomba ulifute kabisa. Sitataka kukudhuru, kwa kuwa itabidi na mimi nijidhuru. Nitapoteza kila kitu hapa duniani, lakini sio wewe. Unaelewa?”  Mzee Masha hakuwa akitania kabisa. Kila alipokuwa akizungumzia hilo, alihakikisha Bella anaelewa. “Unamaanisha utaniua?” Bella aliuliza kwa taratibu huku akimuangalia Mzee Masha usoni kwa mshangao kidogo. “Tutakufa wote, Bella. Sitakaa nikakushiriki wewe na mwanaume mwingine yeyote, labda nisiwepo hapa duniani. Ni heri kufa.” Mzee Masha hakukwepesha macho hata kidogo. Alimaanisha alichokuwa akisema. Bella aligeuka upande mwingine, akalala.

***********************************************

Kwa kuwa alifaulu vizuri kidato cha nne, Bella alianza chuo katika ngazi ya ‘diploma’ ya mambo ya ‘Information technology’{IT}, chini ya ulinzi mkali sana. Kwa kuwa alijua anachunguzwa sana, alijitahidi kukwepa si marafiki wa kiume tu, bali hata wakike huko darasani kwao. Hakuwa na rafiki yeyote yule pale chuoni. Watu walikuwa wakimuonea wivu sana, kwa vitu vya thamani alivyokuwa akimiliki. Uzuri wake ulivutia kila mtu, na kutaka kuwa karibu naye, lakini alijitahidi kuwakwepa kwa kadiri ya uwezo wake. Hata salamu hakuwa akitoa kwa mtu yeyote yule. Alijitahidi kuwahi kuingia darasani na mara kipindi kilipoisha, alitoka bila kukaa humo darasani hata zaidi ya dakika moja. Kila alipofika darasani alikaa kwenye kiti chake na kufungua laptop yake na kuendelea na shuguli zake kimya kimya. Hata mtu alipomsalimia, hakujibu.

Hata hivyo alishaona marafiki hawana maana yeyote ile. Alikumbuka maneno machafu kutoka kwa rafiki ya mama yake, alivyokuwa akimsema marehemu mama yake, wakati hata hajazikwa, yaani maiti ikiwa bado ndani. Bella alichukia sana wanawake. Hakutaka ukaribu nao kabisa. Kwa upande wa wanaume asinge thubutu hata kuwatazama machoni, kwa kuhofia asije kumsababishia matatizo. Alijua endapo Mzee Masha, hata akihisi kuwa ana mwanamme tu, atamuua. Kwa hiyo hakutaka kuingiza mtu yeyote matatizoni. Alijetenga na kila mtu. Alisikia wanafunzi wenzake wakimsema kuwa anaringa sana, lakini Bella hakutaka kujihusisha nao hata kidogo. Alibaki kujichunga na mara nyingi sana Mzee Masha ndiye aliyekuwa dereva wake, ili tu kuepusha shari.

Waliendelea kuongozana kama kumbikumbi. Bella hakuonekana maktaba wala kwenye makundi yakujisomea. Alimpa Masha ratiba yake yote ya vipindi vya darasani. Kwa hiyo kila kipindi kilipoisha, alimkuta Masha anamsubiria nje. Kwa kuwa alikuwa na msingi mzuri sana wa elimu, na yeye na mdogo wake wote walikuwa watundu sana wa kompyuta, kwani mama yao aliwanunulia kila mtu kompyuta yake tokea zamani, walishinda nyumbani kwao wakishindana kutumia kompyuta, yeye na mdogo wake. Kwa hiyo hata alipokuwa shuleni alikuwa na uwezo mkubwa sana wakuelewa mambo. Alikuwa akijisomea yeye mwenyewe na alifaulu vizuri sana. Amani ilikuwepo na Mzee Masha hakuwahi kulalamika hata mara moja. Bella alifuata masharti yote bila shida.

************************************************

Maneno yakaanza kuenea mtaani. Minongono ikawa mikubwa mpaka ikafika kwa wazee wenzake Mzee Masha. Kwani Mzee Masha alibadilika sana. Hakuwa akionekana mahali popote hata kwenye vikao. Ilikuwa ni yeye, kazini kwake na Bella tu. Akili na mawazo ya Masha yalikuwa kwa Bella pekee, wakati wote. Kwani naye Bella alizidi kupamba akili za Masha. Maneno matamu na ujumbe wa hapa na pale havikuisha kwa Masha.

Kulikuwa na kundi moja la kabila la kina Mzee Masha, walikutana hapo jijini Dar, tokea miaka ya 70, wakitafuta maisha. Wanaume hao wakaamua kuunda kundi lao na kusaidiana katika hali na mali. Wote walianza wakiwa chini sana kimaisha, na wakamua kwa pamoja, kunyanyuana na kuapishana kuwa kamwe watoto wao hawatakuja kuwa masikini. Walikuwa na kanuni zao ambazo walizifuatilia sana. Walikuwa na umoja na mshikamano wa hali ya juu. Hata wake zao walio waoa pia iliwalazimu kushikamana sana na kujikuta kama ndugu. Mwishowe watoto wao wakajikuta wakioana wenyewe kwa wenyewe, kwani ndio walikuwa wakikutana mara kwa mara.

Walikuwa wakikutana kijijini kwao vipindi vya sikukuu za krismasi, lakini pasaka, walikuwa wakiwa pamoja mjini. Walitafuta nyumba moja, walipika pamoja na kula pamoja. Mpaka walipokuza familia zao, utaratibu uliendelea. Watoto wao walisoma shule nzuri sana kwa kupitia michango yao wao wenyewe. Waliofanikiwa kwenda vyuo vikuu, hawakusubiri mikopo ya serikali ili kupeleka watoto wao shule, wao wenyewe walichanga na kusomesha watoto wao.


Ilikuwa ni rahisi pia kwa watoto wao kuwa pamoja au kuona, kwani ni kama walilelewa na mama mmoja. Kina mama hao walikuwa wacha Mungu. Walikuwa wakikutana pamoja na kuombea familia zao kila siku za jumamosi asubuhi kwa wale walioweza. Waliwekeana njia mbalimbali za kuwakuza watoto wao kwenye maadili ya Mungu na hata walipopata mtoto mwenye tabia mbaya, walisaidiana kuomba. Hapakuwa na mtoto wa familia fulani, wote walikuwa watoto wa wote.

Huo umoja ulidumu kwa muda mrefu sana . Hapakuwa na mwenye shida kati yao, iwe pesa au ndoa zao. Hata kama kulikuwa na mambo mabaya yanayoendelea katikati yao, ilikuwa ni kwa siri, na yalimalizwa kimya kimya.

Sasa Mzee Masha ndiye alianza kuleta sifa mbaya kati yao. Walianza kumlaumu mkewe kuondoka na kumuacha mumewe nyuma, lakini hayo yalikuwa ni makubaliano ya familia nzima. Mzee Masha alimpa mkewe baraka zote, na kumwahidi kuwa akienda kumtembelea mara kwa mara. Mzee Masha alikuwa akiingiza pesa nyingi sana katika biashara aliyokuwa akifanya. Hata mkewe alikubaliana naye, isingekuwa jambo la busara kuacha biashara zao huku Tanzania na kwenda kuishi kwa mshahara wa mkewe aliokuwa akilipwa na serikali huko nchini Uholanzi.

Kwa mara ya kwanza Masha alimshirikisha Bella baadhi ya biashara anazofanya, kuwa alikuwa ameingia mkataba na serikali kuwauzia kampuni ya umeme, nguzo za umeme na kwenye makampuni ya simu, aliwauzia minara ya simu pia. Alimwambia pia kampuni anayomiliki huwa inachukua tenda za serikalini na makampuni mbalimbali, endapo itashinda kwa tenda anazochagua yeye Masha, na anazoona zitamlipa pesa nyingi, tena kwa haraka bila kuwekeza pesa nyingi kwenye tenda hizo. Alimwambia ndio maana haachi kusoma magazeti ili kujua tenda zinazotangazwa na yeye kujaribu kuzifuatilia mpaka anaposhinda tenda hizo. Alimwambia kinachohitajika ni umakini katika kuchagua aina ya tenda, kushindana na makampuni mengine ili kupata tenda hizo, na akishapata kuhakikisha anapeleka vitu vizuri ili kujenga jina zuri, ili kudumu kwenye soko. Kwa hiyo ni kweli yeye ndiye alikuwa akiingiza pesa nyingi sana kuliko mkewe. Na ndio maana walikubaliana yeye abaki na mkewe aende kushika nafasi hiyo aliyoipata kwa bahati sana, na mkewe alimwambia ni kitu alichokuwa akikitamani tokea zamani.

Haikutokea tokea tu mama huyo kuteuliwa kuwa balozi. Alianza kujijengea jina tokea zamani, na alikuwa ni mama aliyejulikana sana nchini Tanzania. Kuteuliwa huko, kwake ilikuwa ni moja ya ndoto zake alizotamani kuja kutimia, kwani alikuwa na ndoto za kwenda juu zaidi ya hapo.


Kwa kuwa Masha alikuwa na pesa nyingi sana kuliko wazee wote kwenye kundi lao, yeye ndiye alikuwa akitegemewa sana kwenye michango ya kundi lao. Hakusoma sana kama wenzake walikuwa wamefika mjini kwa lengo la kujiendeleza kielimu. Yeye alipotua tu jijini miaka hiyo ya 70, alijitupia kwenye biashara moja kwa moja. Kwa hiyo enzi hizo wakati wapo vijana, Mzee Masha aliyekuwa ameshajua njia nyingi za kupata pesa, aliwainua sana wenzake walipokuwa wakitoka chuoni. Aliwasaidia kuwaombea kazi kwenye kampuni mbalimbali na watoto wao pia aliwasaidia. Alikuwa mtoaji sana na hakuwa Mzee wa kukata tamaa. Alipokusudia jambo kubwa litokee katikati yao, hata kama wote watakata tamaa, lakini Mzee Masha huwa hakati tamaa, atasimamia hilo jambo mpaka litokee. Iwe upande wa watoto wa rafiki zake, au marafiki zake wenyewe. Alihakikisha wote wanahali nzuri za kimaisha kwa kuhimizana na kuwafundisha njia zakuwaingizia pesa zaidi. Kwa hiyo yeye ndiye alikuwa msemaji mkuu kati yao, na walimuheshimu sana katika hilo kundi. Hakuna jambo au kikao kilichopitisha jambo bila Mzee Masha kuidhinisha, japokuwa yeye ndiye alikuwa mdogo kidogo kuliko wote. Na hakuwahi hata mara moja kuwa na sifa mbaya katika jamii, ila Bella ndiye aliyemchanganya na kumwingizia dosari kwenye ndoa yake. Alijisahau kabisa kama anatizamwa kwenye jamii. Hakujali mtu yeyote isipokuwa Bella tu, ambaye  kwake alikuwa kila kitu.

 “Historia ya Bella na familia hiyo ya Masha.”
Haikuwa kwa bahati mbaya kutokea kumpenda Bella. Ni mtoto aliyekuwa akilala mara nyingi tu nyumbani kwake. Alishamuona akiwa uchi, yaani na vinguo vya kuogelea, alishamuona akiwa amevaa taulo tu wakiwa wanaenda kuoga, hapo nyumbani kwake na hata kwenye mahoteli waliyokuwa wakienda kama familia. Zera rafiki yake kipenzi, alikuwa akimwalika Bella kusafiri nao kila wanapokuwa wanasafiri kwenda mapumzikoni. Bella alikuwa na maumbile ya kutamanisha sana. Japokuwa alikuwa mtoto, lakini hakuna aliyeacha kutupia macho kwenye mwili wa binti huyo aliyekuwa na akili za kitoto.  Kama mama yake alivyokuwa anamshauri kusubiri na kumwambia hana haja ya kuwa na mpenzi kwa wakati ule, kweli Bella naye alijiona mtoto, hakuwahi kufikiria swala la mapenzi hata kidogo.

Hata kaka yake Zera, Junior Masha, alimsumbua sana Bella, akimtaka awe mpenzi wake, lakini Bella alishamkatalia katakata, akimwambia yeye ni mtoto na hataki mambo ya wakubwa. Zera alikuwa na mahusiano ya kimapenzi na wanaume tofauti tofauti, hata Junior alikuwa akimwambia Bella, kuwa haina shida kwani hata Zera rafiki yake anao wanaume na haimletei matatizo, lakini Bella alimkatalia, tena kwa kitoto sana.

Junior mtoto mkubwa wa Masha, alijua kutapanya pesa ya baba yake. Alivuma jijini, kila mtu alimjua Junior Masha. Alijua kuweka heshima kila alipokanyaga na wenzake kwa starehe. Alikunywa pombe kwenye baa za kisasa na wanawake walikuwa wakimkimbilia kwa kuwahonga pesa za maana. Marafiki zake ni watoto wavigogo watupu. Kila wanapofika baa, Junior na rafiki zake walianza kulipa kwanza, ndipo wakae na kunywa. Waliacha mapesa kaunta, ndipo wanatafuta meza yao maalumu nakuanza kunywa vinywaji vikali. Walitembea na warembo na wasichana maarufu sana hapo nchini. Katika kundi lao, mtu aliyewazungusha akili, na kubaki kitendawili kigumu kati yao alikuwa Bella pekee. Walimtamani binti huyo na kumtafutia njia nyingi za kumpata lakini walishindwa. 

Junior alijitahidi kuacha pombe kwa muda, akimuahidi Bella atatulia lakini Bella alimkatalia kabisa. Zera alisha mbembelezea kaka yake, na kumwambia Bella, endapo angemkubali Junior kaka yake, itamsaidia kutulia na labda angependa shule kama wenzake. Lakini Bella alikataa kata kata, hata kunakipindi urafiki wao uliisha sababu ya Bella kumkataa kaka yake. Mwishowe walikubali kuwa Bella haingiliki.


Bella hakuwa akitoka kwenye familia yenye pesa sana kama wao na wala mama yake hakuwa msomi kama mama yao, lakini mama yake Bella alijinyima sana kuhakikisha watoto wake wanasoma katika shule za matajiri na ni kweli walifiti kwenye jamii hiyo ya watoto wenye pesa. Kwa hiyo Enabella na Eric, walijikuta wakifikiri,  walitazama mambo yao, na kuongea kama watoto wa matajiri. Na ndio maana Bella aliweza kupenya kirahisi sana  na kuishi katikati la kundi hilo la kina Zera, la watoto wa matajiri wa jijini bila shida. Mara nyingi walikuwa wakila na kutembea kama kikundi wawapo shuleni, na baada ya kutoka shuleni pia hawakuacha kuwa pamoja. Sherehe zao zakuzaliwa walizifanya pamoja, tena kwenye mahoteli makubwa na ya kisasa pale jijini, huku wazazi wao wakiwa ndio wafadhili wao. 

Watoto hao wakiongozwa na watoto wa Masha, upande wa mabinti kiongozi wao alikuwa Zera Masha na upande wa vijana wakiume wale wenye tabia za ajabu, waliongozwa na Junior Masha, walikuwa wakitapanya pesa za wazazi wao, bila kujali kesho. Zera ndiye alikuwa kipenzi cha baba yake, kwa kiyo hata kama Mzee Masha alikuwa na kazi nyingi kiasi gani, anapohitajika kuhudhuria kitu chochote alichoandaa binti yake, alikwenda. Na ndipo huko alipokuwa akionana na Bella akiwa uchi au wamevaa yale mavazi yao wanayodai ya watoto wakizungu na kuacha sehemu zao kubwa za mwili nje. Na ndio kwa mara ya kwanza maishani jicho la Mzee Masha lilipoanza kupata matatizo juu ya mtoto huyo Bella.


Siku moja kwenye birthday ya Zera akiwa anatimiza miaka 15, walienda kufanyia sherehe hiyo kwenye hoteli moja ya kitalii iliyokuwa pembezoni mwa bahari. Zera alikodi vyumba kadhaa ambavyo angelala na marafiki zake mara baada ya kusherehekea na wazazi wao. Alialika marafiki zake, watoto wa matajiri wa hapo jijini, wazazi wao pia walihudhurua na Bella  naye alikuwepo. Kasoro mama yake Bella hakuwepo siku hiyo kwani alishaanza kuumwa, kwa hiyo kama kawaida, Mat, dereva wao ndiye aliyempeleka Bella kwenye tafrija hiyo.

Walipofika tu hotelini hapo, wakati wazazi wao wakila na kunywa, watoto hao waliingia chumba cha kubadili nguo, na wote wakatoka na nguo za kuogelea. Wazazi wengine, waliwatazama binti wale kama watoto, lakini Mzee Masha tamaa ilianza kumsumbua sana. Kila alipokuwa akimtizama Bella, alitamani awe mtu mzima kidogo, ili angalau arushe ndoano yake. Kadiri muda ulivyozidi kwenda, wakati watoto wao wakiogelea na kucheza bila hofu mbele ya wazazi wao, wakiwa na nguo za kuogelea, ndivyo Mzee Masha alivyokuwa akitokwa na mate kwa Bella. Alitaka kuongea naye usiku huo wakati mabinti hao wanapoingia kwenye vyumba vyao, hotelini hapo kulala, lakini Bella alikataa katakata kulala, akasema anataka kurudi kumuuguza mama yake na kweli aliondoka mapema sana, kitu kilichomuumiza sana Mzee Masha, na kuapa kumsaka Bella kwa wakati wake.

Mzee Masha alishatafuta njia nyingi za kumvutia Bella, akijidai kutoa misaada ya hapa na pale, ilimradi tu kumvutia Bella, lakini Bella alijawa na utoto mwingi sana akilini mwake, hakuwa hata akimuelewa, alimuhesabu kama baba tu. Alishasaidia kulipa baadhi ya garama pale shuleni, akijidai kumpongeza Bella kama rafiki wa karibu wa binti yake Zera, ambaye alimuhimiza masomo. Bella ndiye alikuwa akimsaidia sana Zera shuleni. Ndio maana hata mama yake Zera alimkubali Bella aendelee kuwa karibu na mwanae, na kusafiri naye sehemu mbalimbali za starehe ili kumsaidia mambo ya shuleni.

Kila walipotoka kama familia na kwenda mapumzikoni sehemu mbalimbali hapo nchini, Masha alimruhusu Zera kualika rafiki mmoja tu, akijua wazi Bella ndiye angealikwa ili ikiwezekana apate naye muda, lakini aliambulia patupu kwani Bella hakuwa akielewa kitu juu ya mapenzi. Kila jambo alilokuwa akiambiwa sirini na baba yake Zera, Mzee Masha, alilisimulia wakiwa wamekaa familia nzima mezani huku akicheka, bila hofu mbele ya mkewe na watoto wake Masha. Ndipo Masha alipoona ni heri amwache kwanza, kwani ni kweli alikubali Bella ana akili za kitoto. Baada ya kumaliza shule, kidato cha 4, Bella akiwa na umri wa miaka 16, mama yake alizidiwa sana, akapotea kabisa katikati ya kundi hilo la marafiki. Hata walipokuwa wakimpigia simu aungane nao kwenye starehe zao, Bella alikataa. Alibaki akimuuguza mama yake tu.

 “Bella kabla ya kifo cha mama yake.”
Ilifika kipindi Tunu, alikuwa hawezi kuamka kabisa kitandani, kwa hiyo yeye kama nguzo ya familia, mtu mmoja tu aliyekuwa akiingizia familia kipato aliposhindwa kuleta pesa nyumbani, mambo yalianza kuyumba. Msichana wa kazi za ndani na kijana wa maua waliwakimbia kwani waliacha kulipwa mshahara, akabaki Bella akimuuguza mama yake kwa karibu sana akisaidiana na Mat. Na hapo ndipo Bella alipojifunza maisha. Tunu aliugua kwa muda mrefu sana, lakini ilikuwa ni kipindi ambacho ni kama Mungu alikuwa akimuandaa Bella, mtoto aliyekuwa haelewi kama kuna watu wanaweza kukosa pesa, au hata kulala njaa hapa duniani. 

Ndicho kipindi hicho Bella ilimbidi ajifunze maisha au kazi za nyumbani. Alijifunza biashara, kwani ilimbidi kuanza kuuza baadhi ya vitu vya thamani walivyokuwa navyo ili kuweza kumudu matibabu ya mama yake, na ada ya mdogo wake ambaye bado alikuwa shuleni. Bella alikuwa msaada mkubwa sana kwa mama yake. Zile akili za kitoto na kupenda starehe, akizunguka kwenye magari ya kina Zera Masha, na kulala kwenye mahoteli ya gharama na familia hiyo ya Masha, zilibadilika, akarudi kwenye uhalisia wa mambo, akaanza kushika majukumu ya mama yake.


Tunu alikufa akiwa na furaha sana, akijua angalau amemuacha Eric kiziwanda wake, kwenye mikono ya dada yake aliyekwisha jua maisha ni nini, na alijua alikuwa amewaachia ngalau  mali ambazo zingewasogeza kimaisha.

Tunu alijua kujipamba kwa dhahabu, tena za hali ya juu. Viatu, nguo zake, vitu vya thamani alivyokuwa amejaza kwenye nyumba yake, alijua kila kimoja ambacho Bella angeuza, angepata pesa nzuri sana. Alimwambia Bella, auze kila kitu, akipata pesa, wahamie kwenye nyumba ya kawaida sana, aanzishe biashara itakayowasaidia kuishi. Na alishamwandaa kukatisha masomo. Alimshauri asiende kidato cha tano na sita, ili kupunguza gharama, bali akosome chuo cha miaka miwili tu cha mambo ya IT, kisha atafute kazi ili amsaidie mdogo wake.

Mipango hiyo alikuwa akipanga na mwanae, Tunu alijua kabisa asingepona. Alikuwa ameathirika na ugonjwa wa UKIMWI, na alichelewa kuanza matibabu. Kwa hatua aliyokuwa amefikia, alijua wazi ana siku chache sana zakuishi, angekufa tu. Alimwandaa Bella kiakili. Alimfundisha mambo yakufanya, changamoto atakazokutana nazo, na jinsi gani yakupambana nazo, kukabiliana na maisha. Kwa hiyo Bella alishakubali kuwa mama yao atawaacha, na alijua ataweza tu maisha bila mama yake.

Mat dereva wake, alikuwa mcha Mungu sana. Alikuwa msaada sana kwao. Aliomba na Tunu, bosi wake kila siku huku akisoma naye neno la Mungu kumjenga Kiroho na kumwandaa na kifo chake. Alimtoa wasiwasi juu ya watoto wake, akamwambia Mungu atawalinda na yeye atakuwa nao bega kwa bega. Kwa hiyo Tunu alikufa akiwa na amani kubwa sana moyoni akijua anawaacha watoto wake kwa Mat ambaye alimpenda sana Tunu. Ile gari ilikuwa kama ya Mat. Alimpa Tunu pesa atakavyo yeye. Tunu hakuwa akimdai ila Mat mwenyewe ndiye alikuwa akikusanya pesa na kumuwekea benki.

Kwa hatua aliyokuwa amefikia Tunu, walijua hatakaa muda mrefu, atakufa, kwa hiyo hata yeye mwenyewe hakutaka kulipa tena kodi ya nyumba waliyokuwa wakiishi. Tofauti na matarajio yake, Tunu hakufa kwa haraka. Baada ya hospitalini kumrudisha nyumbani wakisema hakuna chakufanya, Bella na Mat, wakisubiri siku yeyote afe, Tunu aliugua kwa muda mrefu sana. Wakati mwingine Bella alipata matumaini kuwa mama yake angepona lakini hali yake ilikuwa ikibadilika badilika sana, mpaka alipochanganyikiwa kabisa, kufikia hatua yakutotambua kabisa mtu yeyote yule hata Eric kipenzi chao na mwishowe kukata kauli  mpaka kifo.

Walimzika Tunu, wakiwa wameshafilisika vyakutosha. Bella alikuwa ameshamaliza pesa zote benki kwa kulipa ada kubwa ya mdogo wake, na alishauza vitu vingi vya thamani wakati akimuuguza mama yake. Hata vitu walivyokuwa wameviacha wakati walipoenda kijijini kuzika pia vilipotea. Ndipo Bella akajikuta amebakia yeye na Eric tu, nyumbani kwa Mat ambaye naye alikuwa akihangaika na maisha yake yeye mwenyewe. Kwa hiyo mipango aliyokuwa ameachiwa na mama yake yote haikufanya kazi hata mmoja. Akajikuta amebaki hana urithi wowote ule.

Siku aliyokwenda kuomba msaada nyumbani kwa Mzee Masha, na mkewe kumfukuza kikatili Bella aliyeonekana ni kama amegonga mwamba, ndipo Mzee Masha alipopata mwanya wa kumnasa binti huyo. Wakati Mama Zera anamfukuza Bella, huku wakisaidiana na Zera mwanae kumkejeli, Mzee Masha alimtumia ujumbe dereva wake aliyekuwa upande wa pili, mezani akisoma gazeti, amkimbilie Bella na mdogo wake, awachukue na kuwapeleka kwenye moja ya hoteli zake. Na kweli bila maswali mengi, Bella akiwa kwenye shida, akaingia kwenye lile gari alilokuwa amezoea kulipanda, kumbe safari hii alikuwa akijiingiza kwenye mtego aliokuwa ametegeshewa kwa muda mrefu sana.

 “Ndoa ya Masha, matatani.”
Ndoa ya Mzee Masha ilianza kuleta matatizo. Habari za kuwepo binti mdogo kwenye maisha ya mumewe, zilimfikia mpaka mkewe. Na kutokana na mabadiliko aliyoonyesha mumewe, Mama Masha aliamua kurudi nchini kufuatilia ukweli. Alichanganyikiwa sana aliposikia mumewe anaishi na mtoto mdogo. Kwani sifa za Bella, zilienea kila mahali. Uzuru wake ulikuwa haufananishwi na mtu yeyote. Ila Mama Masha aliambiwa ni mtoto mdogo, mzuri sana. Kazi ilianza kumshinda Mama Masha. Safari za Tanzania zikaanza ili kunusuru ndoa yake, bila mafanikio yeyote. Kwani Mzee Masha alishajiingiza kwenye penzi la Bella, hakujua jinsi ya kurudi kwa mkewe au jinsi ya kuwa nao wote wawili.

Mapenzi yalilemea kwa Bella, msichana asiye na jukumu lolote isipokuwa kumfurahisha yeye tu. Bella hakuwa akiwaza pesa wala kitu chochote kile. Kila kitu alichotaka alitamka tu, Mzee Masha alileta. Hata hivyo alifundwa. Bella hakuwa mtoto tena kama alivyoonekana. Alipata mwalimu aliyehakikisha anamfundisha na kuelewa. Tena alifundishwa vizuri sana jinsi yakuishi na mume, hasa Masha. Shule yake ilikuwa ya uhakika kwani alifundishwa akiwa tayari akiishi na Masha. Kwa hiyo yule mwalimu wake alihakikisha Bella anamwambia tabia zote za Masha, ugumu anao pambana nao kwenye maisha yake na Masha, na yeye akamuelekeza jinsi ya kuishi kutokana na vile Masha alivyo. Bella alimjulia Masha, kuanzia akili yake mpaka mwili wake. Tofauti na Mama Masha aliyekuwa na majukumu mengi tena yote yakimsubiri yeye. Watoto wawili wote waliolewa utajiri wa baba yao, waliokuwa wakimsumbua mama huyo mchana na usiku, huku akiwa na kazi ya kuwakilisha taifa la Tanzania nchini Uholanzi, hapakuwa na jinsi ya kumlinganisha na Bella hata kidogo.

Alikubali kuonekana na mkewe, sababu ya kuridhisha jamii tu kutokana na nyadhifa walizokuwa nazo wote wawili, lakini si mapenzi tena. Alijitahidi kuonyesha kwa nje kila kitu kipo sawa lakini ndani akiwa na mkewe alikuwa akimjibu vibaya sana. Kila Mama Masha alipotaka wazungumzie swala la mwanamke mwingine aliyenaye, Masha alikuwa mkali sana. Na alipiga marufuku asiwahi kumfuatilia maisha yake tena. Ilikuwa ngumu sana Mzee Masha kuwa naye nyumbani pindi anapokuwa amerudi kumtembelea hapa nchini. Kwani Masha alishahama nyumbani hapo muda mrefu sana, akawa akiishi na Bella. Kitendo cha mkewe kurudi, na kumlazimu arudi nyumbani aishi naye kama mume, kilikuwa kikimkasirisha na kumuharibia utaratibu wake mzima. Ilibidi Masha awe anaibua safari za dharula pindi mkewe awapo nyumbani, akimdanganya anasafiri nje ya nchi, ili tu  awe nyumbani kwa Bella.  

Inapomlazimu kulala nyumbani kwake mkewe akiwepo, usiku kucha anakuwa na wasiwasi labda Bella ataondoka nyumbani na kwenda kwa wanaume wengine. Alikuwa akiamka katikati ya usiku, au alfajiri sana kumpigia simu ya skype na ilikuwa lazima Bella apokelee simu hiyo kwa kompyuta ya mezani sio simu yake ya mkononi, ili kuhakikisha amelala nyumbani. Alikuwa kama amechanganyikiwa kati ya mahusiano hayo. Na ukali ulikuwa ukiongezeka mara mbili pindi wanawake hao wote wawili wawapo kwenye mji mmoja. Hofu yake kubwa ni kumuacha Bella peke yake. Kila alipokuwa mbali na Bella, alihisi anaibiwa tu. Hakuamini hata njia alizokuwa ameweka za kumlinda huyo Bella. Alihisi  Bella anaweza kumzidi ujanja sehemu akamtoroka wakati yeye akiwa na mkewe.


*******************************************

Masha aliendelea kumuadhibu mkewe kimya kimya kwa kosa kubwa sana alilomtendea, ambalo Masha hakuwa amemwambia mkewe kuwa anajua uovu wake. Mkewe naye alizicheza karata zake kwa makini sana. Alibadilika akawa mke mwema, huku  bado akiwa anaficha kwa makini sana siri aliyokuwa ameibeba moyoni mwake, kwa miaka mingi, asijue kuwa mumewe alishajua uovu wake. Hasira zilikuwa zikimsumbua Masha kadiri alipokuwa akimtizama mkewe jinsi anavyojionyesha mke mwema, huku akijua wazi amemkosea na anashindwa hata kutubu.

Ukweli Masha alishakuwa kwenye mapenzi ya dhati kwa mkewe. Hakuwahi kuwa na mwanamke wa nje, Bella pekee ndiye wa kwanza. Alipogundua uovu wa mkewe, alichanganyikiwa sana, na kujiambia labda atakuja kutubu leo, au kesho. Siku zilizidi kwenda Bella mkewe kutubu ila kulalamikia tabia za mumewe. Kila baya alilokuwa akifanyiwa na Masha alimkumbusha kuwa yeye ni mume wake, na aliapa katika shida na raha, kwa hiyo kifo pekee ndicho kitawatenganisha. Mzee Masha alikuwa akikasirika sana kila akisikia kauli hiyo, kwani alimjua vile mkewe alivyo. Ni mwanamke aliyekuwa akijua ni kitu gani anataka maishani, na hata kama ni kigumu namna gani, akisema atapata, lazima atakipata tu, kama mumewe alivyo. Hata hivyo alikuwa na sababu kubwa sana iliyomfanya abaki na Masha.


Mama Masha aliishi na mumewe kwa malengo makubwa sana, ambayo hakuna mtu aliyeyajua isipokuwa yeye mwenyewe. Wala si penzi la Masha alilokuwa akilihangaikia, bali ni mali na heshima ile ya ndoa ndivyo vilikuwa ngazi yakumfikisha aendapo au kutimiza malengo yake makubwa sana aliyokuwa ameyabeba tokea anaolewa na Masha. Asingekubali msichana aliyejitokeza karibuni, avunje ndoto zake. Aliamua kupambana kufa na kupona ili Masha asimuache, mpaka atimize lengo lake. Alifanya kila njia ili kumdhibiti mumewe, hasa kwenye upande wa talaka. Alikubali yote, lakini hakuweka mwanya wa kuachana na Masha.

Masha alipoona mkewe ameng’ang’ana akaanza kuanzisha ugomvi usio na maana, ilimradi apate sababu  yakutoka hapo nyumbani na kwenda kwa Bella. Wakati mwingine aliondoka usiku usiku katikati ya ugomvi wao, kurudi kwa Bella, aliyekuwa akimkuta mara zote amelala nyumbani kwao bila wasiwasi. Ulinzi kwa Bella uliongezeka, lakini hakuwahi kumkamata na mwanaume hata mmoja. Lazima tu atatafuta mwanaume huko chuoni. Kwani naingia naye darasani? Mzee Masha akaanza kujutia uamuzi wake wa kumruhusu Bella kwenda shule. Alitamani amkatize masomo, lakini hakuona kosa lolote lile kwa Bella. Alikuwa ametulia kama maji kwenye mtungi. Heshima yake kwa Mzee Masha ilikuwa palepale, na hakuacha kumliwaza kila aliporudi nyumbani kwake akiwa na hasira, bila kutaka kujua kulikoni.


“Penzi la Bella lavunja umoja wa kinamama hao.”
Mama Masha alivumilia kuficha tena aibu ya familia yake, lakini akashindwa. Mwishowe aliamua kuwashirikisha wanawake wenzake akitaka ushauri na waombe kama kawaida yao. Mara nyingi watoto wake ndio waliokuwa wakiombewa mara kwa mara na kina mama hao. Kwani wote wawili, Zera na Junior, ndio walionekana ni washawishi wabaya kati ya kundi la watoto hao. Kwa hiyo kila walipokuwa wakikutana waliwaombea watoto wa Masha. Aliamua kujikaza akaenda nyumbani kwa Mama Mwasha kukutana nao, siku hiyo ya jumamosi alipokuwa nchini.

Nyumbani kwa Mama Mwasha ndio kilikuwa kituo chao kikubwa, kwani mama huyo alikuwa mama mwenye hekima sana, na alijawa na upendo. Kwa hiyo ni kama alikuwa  ndiye kiongozi wao, hao kina mama. Walifanyia vikao vyao vyote nyumbani kwa Mwasha. Waliambizana kuwa Mama Masha yupo nchini na angeomba wote wakutane, ana jambo la kuwashirikisha.


Siku hiyo asubuhi Mama Masha akiwa amechelewa kidogo, wakati anaingia aliwasikia wenzake wakimsema vibaya sana. “Kwani ni jambo gani Mama Masha anataka kutushirikisha tena?” Mmoja wao aliuliza. “Itakuwa janga la mumewe tu.” Mwingine alijibu na kufanya wote wacheke kidogo. “Alipokuwa anaondoka alifikiri nini?"  "Eti sasa hivi ndio anakumbuka shuka wakati kumekucha!” Walimcheka tena. “Nilimshauri kweli Mama Masha aachane na mambo ya Ubalozi. Walikuwa wamefika mbali na muwewe, yeye akaondoka. Alikuwa anatafuta nini na utuuzima huu?” “Sasa ndio ajue, alichokitafuta kakipata. Kavunja nyumba yake kwa mikono yake yeye mwenyewe, sasa hivi mtoto mdogooo ndio anaijenga.” “Kitoto chenyewe mmekiona lakini?” “Namsikia tu!” “Si mchezo. Huwezi kumfananisha na Mama Masha hata kidogo.” “Lakini mwenzetu msomi jamani. Acheni akaishi majuu.” Aliongeza mama mwingine kwa kejeli.  “Basi ndio atulie sasa huko huko majuu na elimu yake. Aache watoto wamtunzie mume.” Wote waliendelea kucheka taratibu huku wakigonga. Mwishowe Mama Masha akaamua kuingia pale sebuleni, wote wakanyamaza, wakidhani hakusikia, kumbe alisikia kila kitu wakati yupo nje. Mama Mwenye nyumba hiyo, Mama Mwasha, alikuwa jikoni akiwaandalia kitu chakula wakati marafiki hao wakiendelea kusengenya.Ulizuka ugomvi mkubwa sana ndani ya hiyo nyumba ya Mwasha, wakisutana kwa hili na kutukanana mpaka Mama Mwasha alipoingilia kati na kuwatuliza. Hapakuwa na maombi siku hiyo zaidi ya ugomvi. Walivurugana kupita kiasi, kila mmoja aliondoka kwa njia yake. Kwani walisemeana siri zao zote. Kila mmoja alisema vile huyu alimsema huyu, na huyu alisema vile. Na huo ndio ukawa mwanzo wa kuvunjika umoja huo wa wakina mama hao. Hakuna aliyemtafuta mwenzake, kila mmoja alikuwa na hasira na mwenzie, huku wakisemeana kwa waume zao, wakati huo Bella ametulia tuli na Mzee Masha nyumbani kwao. Bella hakuruhusu ugomvi wowote ule katikati yao. Alimuunga mkono Mzee Masha kwa kila uamuzi anaotaka kufanya na alipoona ni mambo ya familia yake, alinyamza kimya, hakutaka kuingilia hata kidogo. Alitimiza wajibu wake, pesa yake ikawa inaendelea kuingia benki na ada ya mdogo wake ikawa inaendelea kulipwa.


******************************************
Njia hiyo ya kina mama iliposhindikana, Mama Masha akapata wazo la kutumia watoto wao, kuwa awe anarudi nao Tanzania kumsalimia baba yao hukuhuku nchini sio kumsubiria tena kule Uholanzi kwani Masha alishaanza kutoa udhuru wa kutokwenda kwa familia yake. Kuna kipindi alishindwa kurudi kwa Bella kwa siku mbili mfululizo, mchana na usiku,  kwa kuwa mkewe alirudi nyumbani na watoto wote, Masha akashindwa kuleta fujo au kuacha familia nzima nyumbani, kwani hakuwa amewaona wanae kwa muda mrefu, na wote walimganda baba yao wakionyesha kuwa na hamu naye sana.

Alikaribia kurukwa na akili. Mwili ulikuwa kwa familia yake, akili kwa Bella, aliyekuwa akienda na kurudi shuleni peke yake, tena akijua wazi Masha yupo mjini kwa mkewe, lakini hafiki nyumbani kumuona. Hiyo ndiyo ilizidi kumchanganya Masha. Alikosa ujasiri hata wakupiga simu kwa Bella aliyekuwa akimkataza kuwa na wanaume wengine, wakati yeye yupo na mkewe nyumbani kwake, na kushindwa hata kumuona.


Baada ya siku ya pili, Masha alikuwa na hali mbaya. Alishindwa kujizuia kila mahali walijua kuna tatizo. Si nyumbani kwake wala kazini, alikuwa akigomba sana. Walinzi aliokuwa amewaweka wamfuatilie Bella kila aendapo, walitoa ripoti nzuri tu juu ya Bella, lakini bado dhamira ya Masha ilikuwa ikimsumbua sana. Aliamua kwenda nyumbani kwa Bella bila kujali litakalo tokea tena kwa familia yake. Siku hiyo hata ufunguliwaji wa geti na walinzi waliokuwepo zamu nyumbani kwa Bella, ulikuwa sio sahihi. Alidai wanahatarisha maisha ya Bella. Alianza kugomba kuanzia getini. Alikuwa akiwaka kama moto. Alianza kufukuza kazi wafanyakazi wote pale kwa Bella. Kuanzia kampuni ya ulinzi getini kwa Bella, mpaka wafanyakazi wa nyumbani hapo. Aliitisha wafanyakazi wote kikao cha dharula nje kwenye ua, mara tu dereva alipoegesha gari.

Bella akiwa chumbani kwake akijisomea, alimsikia akigomba sana huko nje. Akaamua asimame, amchungulie ajue kulikoni. Akamuana jinsi anavyofoka, na kupiga teke vyungu vya maua. Alibadilika kuwa mwekundu kama nyanya kwa hasira. Hata huo muda haukuwa ni muda wake ambao Bella alimtarajia pale nyumba. Bella alijua kile kinachoendelea kichwani mwa Masha. Alijua wazi wivu na hofu juu yake, ndivyo vinavyomsumbua Mzee huyo. Alijaribu kwa kadiri ya uwezo wake kumuhakikishia kuwa hatathubutu kumsaliti, lakini kila Masha alipokuwa akikumbuka uzuri wa Bella na umri wake, alijua hawezi kuepuka kulizwa mjini.

Bella alikimbilia simu yake kwa haraka kabla hajaendelea kuharibu vitu pale nje na kujiumiza yeye mwenyewe, akampigia simu huku anamchungulia dirishani. Akamuona jinsi alivyopokea simu yake kwa haraka. “Vipi T?” “Safi tu.” “Nilikuwa nasoma hapa, lakini naona hata sielewi.” “Nini tena?” Masha aliuliza kwa wasiwasi kidogo.  “Sijui. Labda nikikuona akili yangu itafanya kazi vizuri. Hamna ninachoelewa hapa hata kidogo.” Bella alimuona jinsi Masha alivyoanza kujikusanya na tabasamu usoni. “Na nimekuandalia masaji nzuri kweli T, sio ile ya kila siku. Unajua nitafanyaje?” Bella alikuwa akimuuliza kwa utaratibu sana. “Utafanyaje?” Masha alianza kutabasamu huku akiondoka katikati ya wafanyakazi wake na kujisogeza pembeni. “Sitakwambia mpaka uje uone kwa vitendo. Siunanijua nilivyo mzuri kwa vitendo?” Masha alicheka, akisikika ametulia kabisa. “Unajua nipo hapa nje?” Masha aliuliza. “Mbona sasa huingii ndani? Huna hamu na mimi?” Bella aliuliza kwa deko kidogo. “Hapana, nimekuja kwa ajili yako Bella. Ila kuna mambo nilikuwa naweka sawa hapa nje.” Bella alimuona anawageukia wafanyakazi wote na kuwaambia waendelee na kazi na wale wa ndani waondoke mpaka kesho, Bella ataongea nao, yeye amepata dharula kidogo.

“Bella! Bella!” Masha alimuita, kutaka kujua kama alishakata simu. “Nipo T, nakusubiri.” Bella alijibu, haraka sana akakusanya madaftari yake na kompyuta, akaweka pembeni ili kumpokea Masha, aliyekuwa akiingia ndani kwa haraka sana. Alikaa hapo chumbani na Bella, akifurahia mapenzi mpaka usiku sana alipoona Bella amepitiwa na usingizi mzito, ndipo aliporudi kwa familia yake, akiwa ametulia kabisa. Kama kawaida yake, Bella hakutaka kumuuliza alikuwa wapi na kwa nini alipotea kwa siku hizo mbili, bila kuonekana wala kupiga simu. Alimfurahisha tu huyo mzee, na kuacha mambo mengine kama yalivyo, kitu alichokifurahia sana Masha, kwani hakujua ni jinsi gani atajitetea kwake.

***********************************************

Mama Masha alipoona ndoa yake inakwenda kuvunjika kabisa, na Masha hakusikia la mtu, na waziwazi alionyesha yupo tayari kwa lolote, lakini si kumpoteza Bella, akaamua kwenda kulalamika kwa wazee wenzake Masha. Aliwasihi sana wazungumze na mumewe. Alionyesha uthamani wa ndoa yake, jinsi anavyo ihitaji hiyo ndoa na wakati huo yupo tayari kufanya lolote ili kunusuru ndoa hiyo. Hata kama itamlazimu kuachia ngazi kwenye hiyo nafasi ya ubalozi, mama huyo aliwaambia wazee hao, yupo tayari kulipa garama hiyo, ilimradi tu, kunusuru ndoa yake. Japokuwa hakuwa akimaanisha lolote alilokuwa akisema kwa machozi kwa wazee hao, lakini Mama Masha alihakikisha anavuta jamii nzima iwe upande wake, wamuhurumie na kumsaidia ili ndoa hiyo isivunjike. Wale wazee walimuhurumia sana mama huyo, wakaamua kumwitisha Masha ili wazungumze naye.

*Je Ni siri ipi hiyo Masha ameigundua ya mkewe?
*Japokuwa si mapenzi yanayomuhangaisha Mama Masha kulilia ndoa yake, nini anachotaka kutoka kwa mumewe?
*Je Wazee wenzake Masha wataweza kunusuru ndoa ya Masha, aliyekuwa amechanganya na Bella kiasi cha kushindwa hata kujitambua tena?

“Kweli wanawake ni viumbe vinavyoonekana dhaifu sana, lakini Mungu amewapendelea nguvu ya ajabu sana.” Dereva wa Masha, aliyekuwa akimfahamu Masha kwa miaka mingi sana, alirudia rudia sana usemi huo kila wakati alipokuwa na marafiki zake. Kila alipokuwa akimfikiria bosi wake jinsi alivyobadilishwa na penzi la Bella na kuwa kama mjinga! Hakuwa akiamini. Masha aliyekuwa akiogopewa na kila kiumbe aliyemfahamu, alibadilika akawa kama mjinga kwa Bella. Mbele ya Bella, Masha alikuwa kama ombaomba mbele ya tajiri mkubwa sana duniani, au mtumwa mbele ya mtwana. Kama si kufungiwa ndani masaa 24 au ulinzi mkubwa aliojua unamzunguka Bella, yule dereva angejua Bella anamloga sana Masha. Alisharudi mara kadhaa kwa yule mama aliyemtafutia Masha ili amfundishe Bella, akimuuliza alimfundisha nini binti huyo, au kama kuna dawa alimpa Bella ili amuwekee Masha, basi angalau amdokeze yeye, lakini yule mama alikuwa akicheka sana, huku akimpa maneno ya kuwakejeli wanaume huku akimsisitizia yule dereva kwamba, hakuna kiumbe kirahisi kuishi nacho hapa duniani kama mwanaume’.

Usikose sehemu ya 4.0 comments: